ANDIKO
LA UCHUNGU
(Kwa
shemeji zangu na wanangu)
NYAMBUYA OGUCHU,
S.L.P 777666,
MPWAKACHUU,
NYAGAMBA.
Alpha H.Mayengo.
2017
Utangulizi:
Sifa na Utukufu apewe Mwenye
Enzi Mungu atujaliaye uzima na amani katika Taifa letu teule la
Tanzania; ama kwa hakika unastahili ee Mfalme wetu wa Enzi. Kitabu
hiki kimetokana na barua ambayo; hapo awali sikuona umuhimu wa
kuitolea chapa barua hii kwani ilikuwa ni ya siri na iliwahusu
wanafamilia mbili tu, yaani koo hizi mbili ambazo ziliunganishwa na
ndoa ya vijana wao kabla ya kuingia katika mgogoro mkubwa wa
ukandamizaji uliofanywa na mashemeji dhidi ya familia ya moja
iliyotengwa na kuonewa kwa mengi... Niliamua kuanza kuiandika barua
hii baada ya kuona kuwa kulikuwa na mafundisho ya namna fulani hasa
kwa kuzingatia malengo ya mwandishi wa barua hiyo kama alivyokusudia
kuweka wazi lawama na mafundisho aliyolenga kuwapatia watoto wake na
hata shemeji zake.
Nia ya kuandika hii barua kwa
sasa ni kutaka kuichokoza jamii katika fikra pana ili kutambua na
kutoruhusu hali kama hii iliyotokea katika barua kutotokea kwani
hupelekea kutoelewana na hata kuharibu mahusiano na maendeleo ya
familia husika...
Alpha H. Mayengo
0767229249
ANDIKO LA
UCHUNGU
Agwee shemeji; ni matumaini
yangu kuwa u mzima wa njema, wewe na familia yako ikiwa ni pamoja na
majirani zako ambao hawana hata muda wa kukutakia siku njema kila
kukicha.
Mbali na hayo; bwana shemeji,
naomba kutoa maelezo ya ukweli na uwazi kutoka moyoni. Shemeji zangu
, ni kwa muda mrefu sana mmekua mkinishtumu na kunilaumu, kunitenga
na kunihukumu kwa kosa langu la kutohudhuria msiba wa baba yetu
mpendwa(baba mkwe) pindi alipofariki. Kutokana na dhana hiyo
nikaonekana kua mbaya hata bila kuzingatia sababu za mimi
kutohudhuria mazishi hayo ambayo nilitamani sana kuhudhuria. Ingawa
kulikuwa na sababu iliyokuwa nje ya uwezo wangu lakini niliratibu
safari ya familia yangu kuhudhuria kwani mi nilikuwa safarini
kikazi(nje ya nchi).Mbali ya yote niliyofanya kipindi cha msiba huo;
ingawa sikuepo, MUNGU, nyie, pamoja na majirani wote ni mashahidi wa
yote, hata kama siku zote nimekuwa nikibebebeshwa lawama kiasi
ambacho hata mke wangu alikua akiniambia kuwa nilifanya vibaya kwa
kutofika kwenye msiba wa mzee wetu mpendwa... haijalishi nilitoa
mchango gani. Kila siku alinikumbusha habari niliyowahi kumsimulia
wakati wa nyuma; kuhusu, kisa cha Dokta mmoja ambaye alikuwa na tabia
ya kutoa tu mchango kwenye misiba ya watu na kuondoka bila kuhudhuria
mambo mengine yahusuhuyo msiba. Tabia hiyo iliwachukiza sana watu na
kuamua kumwachia msiba wa mama yake kwani kila aliyeenda kumpa pole;
alitoa mchango na kuondoka kama alivyokua akifanya yeye kwenye misiba
ya watu, hivyo walimwachia shughuli zote azifanye kwa kutumia ule
mchango waliotoa kama yeye alivyozoea kuwafanyia wafiwa kitu
kiichomletea majonzi makubwa.
Kwa muda mrefu nilikaa kimya
ili ufike wakati mkumbuke kua hata kama ingekua ni kulalamika wa
kwanza kufanya hivyo ningekua ni mimi... nasema kama ingekua ni
kulalamika wa kwanza kufanya hivyo ningekua mie; lakini hamkusikia
kulalama wala kuwashtumu kwa lolote, kwani hakuna siku hata moja
niliyofungua kinywa changu kuongea kuhusu kutofika kwenu kwenye
misiba iliyoyonikuta … narudia tena ili kuongeza uelewa kwenu kua
nazungumzia misiba na si msiba kama nyie mnavyonilaumu kwa
kutohudhuria msiba wa baba mpendwa(baba mkwe) tena kwa sababu
mliyoifahamu.
Nimefungua kinywa changu sasa
baada ya kuona malalamiko yamezidi kwani sielewi ni nini hasa chanzo
cha lalamiko hizo au kuna kitu cha ziada ambacho mi sikijui ilhali
nimemuoa dada yenu? Bwana ee hata punda alinena wakati Balaki na
Balaam tazama maarifa katika biblia takahai.
Baada ya kusikia malalamiko
kwa muda mrefu; nilikaa na waifu na kuongea nae kuhusu mzigo huu wa
lawama ambao nimebebeshwa kwa muda mrefu,kwani nilianza kuhisi moyo
wangu umekinaishwa kama si kuumizwa kwa lawama ambazo si za kweli na
niliamini kuwa lawama hizo zilikua zikipanda mbegu zenye sumu mbaya
kwa wanangu na jamii iliyowazunguka wanangu pamoja na huduma yangu .
Nilianza kumuuliza waifu kwa
kuorodhesha baadhi tu ya misiba iliyotokea upande wangu ambayo
iligusa wengi na kuniumiza sana:
mimi: “waifu; ivi kwenye
msiba wa kakaangu(1981) nani alihudhuria kutoka
kwenu”?
Waifu: “hakuna”.
Mimi: “wakweo, je”?(mama
yangu mzazi, 1982; na baba 1989).
waifu: “hamna”.
Mimi: “na je kwenye kifo
cha Ka'changwe(1986) Nani alifika!” pamoja na kifo cha kaka
Mgassa(1993) ;kaka Msanga(2008); na Ndalu je (2009) nani alifika
kutoka kwenu?
Waifu: “hakuna... hakuna...
tusamee”....(kwa uchungu na aibu huku machozi yakimtembelea bwana
mashavu kuomba njia kabla ya kufika kule yaendako).
Mimi: “Sasa; kumbe ni
misiba mingi tu ambayo hawakuja ndugu kutoka upande wenu, lakini mi
sikuona sababu ya kuwalaumu wala kuwakumbusheni ilhali nyie ndio
imekuwa fimbo mujalabu kwangu na hata kufikia hatua ya kunichambua
vibaya kwa watu ambao kila siku waja kuniambia malalamiko yenu...
TAFAKURI
Mbali na hayo; kabla ya msiba wa baba (babamkwe) uliotokea mwaka 1996, nilishapata misiba
zaidi ya mitano lakini hakuja mtu hata mmoja na hata baada ya hapo
kuna mambo mengi sana ambayo hamkutaka kushiriki kwa maksudi kabisa .
Na bora mngekaa kimya tofauti na kuwa ndo wa kwanza kutangaza rumazi
kwa mtaa. Kumbukeni nilivyohangaika na mwanangu alipokua anaumwa bila
hata kujaliwa tena nilitengwa hata kupewa faraja ya kindugu ilikuwa
shida zaidi ya kuongezewa maumivu kutokana na maneno yenu yenye
kuvunja moyo. Kiukweli sihitaji sana msaada na hata ushiriki wenu na
pia sipendi kuhesabiwa ubaya ambao mwausambaza na kuupandikiza kwa
kizazi changu na chenu.
Hivi kuna sababu gani kuwe na
chuki kati ya pande ambazo ziliungana kwa furaha. Nakumbuka kua
mlisema mmenitenga wakati namuuguza mwanangu Ufudu; hospitali ya
rufaa kwa miezi kadhaa si KCMC wala Muhimbili wasikomjua mwanangu Ufudu
na hakuna hata mmoja wenu aliyethubutu kuja kumjulia hali kama si
hata kuwasiliana ilikua tatizo. Mbali na hayo; nilipata ajali mbaya
ya pikipiki almanusra kufa lakini hakuna aliyekuja ila kunitupia
lawama na kufurahia anguko langu. Daima mwajitahidi kutafuta lawama
ili mnilaumu na kunifanya mnyonge kama ilivyo ada kwenu.
Kumbukeni mambo niliyofanya
kwa ajili yenu ingawa mwaendelea kunishtumu na kunilaumu:
- nilishiriki mazishi ya bibi yenu kule makale 1982
- nilisimamia tohara ya shemeji zangu tena mi ndo nilitafuta na kuongoza muziki asilia katika shughuli ile.
- Nilishiriki harusi ya mama mezbii kule idodomya
- nilisaidia kumuuguza baba mkwe na hata mazishi nilimtuma familia yangu na kutoa msaada kila ulipohitajika.
- Elimu ya kaka yenu wa pekee na mndogo wenu huyo leo anayenitukana pia niliisimamia mie.
- Matibabu na mazishi ya mjomba wenu niliwezesha mimi na mengine mengi mwakumbuka sina haja ya kuyataja yote. Hivi kweli mwanihukumu kwa haki?
JIBU LA
TAFAKURI
Kwa mawazo yangu mafupi,
yaso-busara niligindua kitu baada ya nyie kuhudhuria mazishi ya kaka
yangu ambaye mwanae ameoa pia katika hii familia yenu kitu ambacho
mlifanya ili kuuteka ukoo wetu na kuumiliki kwa kila kitu. Maana si
kawaida vijana wa ukoo mmoja kwenda kuoa ukoo mmoja maana kuna koo
nyingi tu tena zenye maadili kuliko hata ukoo wenu ambao mambo yake
mwayajua wenyewe . Hebu tafakarini ni kwa nini hamkutaka kuhudhuria
misiba iliyonigusa mimi na kijana wa kaka yangu mana sisi sote tumeoa
hapo kwenu; lakini mnahudhuria mazishi ya kaka yangu ambaye ndiye
aliyemzaa kijana wangu. Sasa basi kupitia kitendo hiki niligundua kua
kuna sababu iliyowafanya msihudhurie misiba inihusuyo sana na kuja kwa
ajili ya kuonesha kua kuna upande mwingine ambao hamjaamua kuutenga
kwani upande huo mmeshautawala.
Jambo hili naomba vijana
wangu na dunia itambue kua kitendo cha nyie kutokuja kwenye misiba
iliyowagusa wengi kwenye ukoo; na kuja kwenye huo msiba mmoja, mlilenga kutugawanya ili mtutawale vizuri kwani ukoo mzima mwauona kua wabaya ila mlango mmoja tu ndio mwaupenda... ama
kweli uigaji wa mambo ya kigeni hautaisha... kumbuka divide and rule
ya wakoloni...
sikieni shemeji kama si
dharau na ukandamizaji ni nini?
Ninyi hamkufika kwenye misiba
mingi tu lakini mi kutokufika kwa ule msiba tena kwa sababu
mliyoitambua ni kosa?
Hebu jihojini kidogo; je kuna
ajenda gani ya siri kati yenu na waifu maana ana tabia za kinyonga...
ivi inawezekana kweli mi nisijue mambo yake anayofanya?
Nilimpatia hela afanyie
biashara ili ajiwezeshe kwa mambo yake madogomadogo... lakini cha
kushangaza aliamua kuleta mzozo ili tugombane na hivyo kukimbilia kwa
wanangu Arusha ambako aliadai ameondoka bila hela na baada ya
mie kumwita arudi; alikuja bila fedha hizo ilhali nauli ya kwenda
alipewa na wanangu na ya kurudi nilimpa mie, sasa aliifanyia nini
pesa hiyo na ilikua nyingi muno.
Licha ya hayo; nilimmtuma
kukununua nafaka kijijini lakini alirudi bila mzigo akidai amemwachia
dadake lakini hadi leo sijui na kuuliza ndo mwanzo wa makelele, lakini pia; biashara ya viazi ilikoishia sikujua kabisa.
Kwa nini watoto wangu wote yeye
ndo amekua chanzo cha wao kuondoka nyumbani na hata kushirikiana na
watoto wa dada na wadogoze kuwanyanyasa wanangu wapendwa...
kwa nini shemeji zangu
mshirikiane na waifu kunidanganya? Mfano wale kuku niliokamata tenga
likipelekwa sokoni bila mi kujua na hata hivyo nilidanganywa pia...
na kunigombanisha na wanangu...
Tangu mama(mama mkwe)
alipohamia Idodomya; yaani kuanza kuishi hapa karibu nasi, ilipelekea
kutoa mwanya wa ndugu wengi kuanza kuja hapa kwangu na ndio muda
ambao nilianza kuona tabia za waifu zikibadilika hadi kufikia
kutoelewana hasa kwa mambo madogo sana ambayo hapo awali
hayakuonekana. Kwa mfano:
- kuongezeka kwa matatizo na magomvi yaso maana wala umuhimu.
- Kuongezeka kwa wimbi la kutoka vitu ndani ya nyumba yangu bila mi kupewa taarifa yoyote na hata matumizi ya pesa ambayo hayaeleweki kabisa.
- Wanangu kuanza kuteswa na ndugu wa mama hata kufikia hatua ya mtoto mdogo wa kike tena ambaye si mrithi wangu kumuamulia mwanangu mkubwa wa kiume kuhamia vyumba vya ndani akiwa na mewe ili alale huko bila kujali heshima ya mama kulala nyumba moja na mwanae ambaye tayari ameshaoa... ivi ni heshima gani mtoto wa kike kutaka kulala vyumba vya nje na kumlazimisha mmrithi wangu kulala nyumba moja na mama wakati nia yangu ya kujenga vyumba vya nje ni kutowafanya wanangu kuwa wanyonge hasa wajapo na wakwe zangu na ni kutunza utu wao... Sasa swali kwa Remavurugu alikua anataka nini kung'ang'ania kulala kwenye vyumba vya nje ambako niliwajengea wanangu wa kiume? Na hiyo nguvu ya kujiamulia kwenye malango yangu aliipata wapi? Na ni wapi uliona mkaribishwa akawa mtawala? Au kwa kua alianza kulala nje kwa hawala na alifanya hivyo ili apate uhuru?
- Kama haitoshi dada yake Remavurugu(Nyakwehe) alimtukana mrithi wangu kwa kosa la kuhoji nguo ya msimamizi iliyopotea mikononi mwake; akiziandaa wakati wa harusi ya mrithi wangu, na kuambulia matusi tena zaidi ya sms 30 zote alizotumiwa zilikusudia kufikisha matusi tena yaliyotuchanganya wote yaani; mimi, pamoja na familia nzima. Sasa mwanangu alikua amekodi hilo vazi na lilipotea kwake asiulize? Na je mbona baada ya muda kupita linaonekana kwa Nyakwehe ambaye alitukana akidai hana shida kama hizo ? Je tungemchukulia sheria ingekuaje wakati meseji zake zote za kukana na matusi zipo? Au je kama mrithi wangu asingevumilia na kumpiga Nyakwehe tungemlaumu nani?Kama ni hivi nina mashaka na baadaye...kama leo kila kitu kinachotokea naundiwa timu ya wanafamilia na watu baki na pia mambo ya familia kukimbiziwa kwa kundi fulani tena kwa kusukwa ili mimi nionekane mbaya na mwenye matatizo katika familia hii; hasa ninaposimama kupinga mambo yasiyofaa katika familia yangu...?Sasa; tujiulize, ndoa itakua salama kwa kutegemea ndugu; serikali; magazeti ya udaku; au uongozi wa dini?Kati ya yote nitakayoeleza mjue nimelazimika kuyasema maana megundua kua kunyamaza kwangu kumemfanya waifu apate nafasi ya kunisema kwao; hata, kuniundia njama na tuhuma ambazo zakusudia kunivunjia heshima na utu wangu; kiasi ambacho nakosa heshima kabisa kutokana na tabia yake ya kujiasafisha kwa kunisema bila kuzingatia heshima yangu na utumishi wangu ambao huwafanya waonekane kama wanavyoonekana leo kwa jamii hiyo hiyo wanisemako.Yafuatayo ni mambo ambayo niliamua kuyafanya siri yangu ili kuitunza heshima ya waifu mbele ya hao hao ambao yeye hunisema kwao na kunichafua kwa mambo ambayo si ya kweli:
- aibu niliyoipata chuoni tukisoma mimi na waifu mara baada ya waifu kugombana na vibaya na mke wa lekchara wetu kitendo ambacho kilileta machafuko makubwa ya mahusiano kati yetu na familia ya lekchara huyo ambaye baadaye alikuja kuwa mkuu wa kazi katika eneo letu la kazi.
- Taarifa ya mkuu wa chuo pindi tumalizapo chuo ambayo ilibeba furaha na huzuni; kwani, mimi nilipewa cheti cha nidhamu/tabia njema ilhali waifu kuonekana kuwa na kiburi na ukorofi na hii ilikua ni kwa mujibu wa kikao cha waalimu; hivyo, wakanionya kuwa lazima nimkanye waifu ili asiye akaifanya kazi yetu kuwa ngumu na iso mafanikio.
- Waifu kunitupia meza wakati tunafunga vitu nyumbani kwao mara baada ya kutoka masomoni kwa sababu niliiulizia hiyo meza kumbe yeye alishamgawia ndugu yake hivyo nilimuudhi kuiulizia na kuitaka ndo maana kwa hasira nyingi aliamua kunitupia na kuniponda nayo tena mbele ya wazazi wake ambao hawakusema lolote ingawa waliona tukio zima. Jioni hiyo ndio ilikuwa siku pekee ya maagano kwani sisi tulikua tunaelekea sehemu ya kazi hivyo niliamua kuwa na mazungumzo na wazazi kwa kuwaeleza hali iliyotokea chuoni kwa waifu kushambuliwa vikali kwa tabia yake ya ujeuri lakini wazazi walikaa kimya ingawa hata tukio la mchana la kupondwa na meza walilishuhudia...kiukweli nilitegemea msaada kutoka kwa baba lakini sikuambulia kitu.
- Kuiacha nyumba yangu ya kwanza kuijenga maishani mwangu ambayo ilikuwa kijiji kimoja na ukweni ni jambo ambalo hakuna hata mtu mmoja aliyeelewa ni kwa nini niliamua kuiacha nyumba hiyo. Ila wao waliamini kua ni moyo wangu tu wa upendo ndio ulionifanya niwaachie na kutoitaka tena wala kuiulizia...nilifanya hivyo kwa sababu niligundua kua kuishi karibu na wazazi wake kungepelekea kuongezeka kwa makelele maana sikuwa na mtetezi katika eneo hilo.
- Pia kutoroka kwa Mwasuga mwaka 1996 ilikuwa ni kwa sababu ya magomvi yaliyozidi ya waifu hadi kupelekea mwanangu tena wa kike kutoroka usiku wa manane kwa kutembea kilomita 18 hadi mji mwingine ambako aliomba kupanda gari na kutimkia kwa mjomba ake. Huko alifanywa kijakazi wa bila malipo na mwisho wa siku kufukuzwa kama mbwa kwa kosa la wizi kama wafanyakazi wengine wengi tu ambao walishaondolewa kwa staili hiyo hiyo. Kaka yenu ndiye huwapa kiburi hawa wadogo zake akiwemo waifu ambaye kiburi chake chote hutoka kwa huyo kaka yenu aliyebarikiwa utajiri ambao wafanya kazi wake wote hufukuzwa pale bila malipo eti kwa madai ya kuiba fedha kama ilivyotokea kwa mwanangu Mwasuga. Alafu bila aibu, waifu anaungana na wewe(kaka yake) na wapinzani wangu kutaka kuniabisha kwa kunisukia mpango ambao wao ndio chanzo cha matatizo yote yanayompata Mwasuga leo kwa kutaka kunipost kwenye magazeti ya udaku eti mie sina malezi bora na upendo kwa watoto?
- Hakuishia hapo tu; bali, hata mwanangu Dahamimz; waifu alimfukuza nyumbani, kwa kosa la kuonekana akiingia kwenye chumba cha mwanaume ilhali mimi nikiwa sipo... Baada ya kurudi niliuliza na baaada ya maelezo yake, nilimuunga mkono kwa maamuzi yale; lakini kesho yake alinigeuka na kumuita dahamimz akashinda naye nyumbani na kumwondoa kwa siri mara tu baada ya mimi kurudi sikujua walichokuwa wanapanga na nilijiuliza sana baada ya kufahamu kuwa kuna mawasiliano ya siri kati yao waifu na Dahamimz ilhali yeye ndiye aliyemfukuza Dahamimz.
- Waifu kugombana na Phinawheh hadi kupelekea mwanangu kukimbilia mkoa jirani ambako aliishi kwa muda hadi kaka yake alipofanikiwa kujua alikojificha na kumfuata ili arudi shule... kama hiyo haitoshi baadaye mwanangu aliondoka tena na kutimkia kusikojulikana hadi leo.
- Ugomvi wa waifu na Zeetela ambao ulitokea wakati mimi sipo na kwa mujibu wa waifu na majirani ni kwamba waifu aliponea pafinyu sana kipigwa na Zeetela ambaye aliwaka kwa kusema, “mama nina moto sana na wewe koz tumechoka kunyanyasika kwenye nyumba yetu wenyewe, tukaishi wapi?...ka shida ni kukaa hapa home; sasa nasepa bimkubwa ni gudi nikaishi kwa kuhangaika popote kuliko hapa nyumbani”.
- Nilivyomuokoa waifu na kupelekwa mahakamani baada ya kumtukana vibaya jirani yake pindi nilipokua prinsipowa chuo lakini nililazimika kuomba msamaha tena kwa magoti kwani waifu alimtukana jirani yake kuwa amekondeana kama ana ukimwi tena ni kipindi ambacho unyanyapaa ndio ulikuwa umeshika kasi katika kupigwa marufuku.
- Kutupiwa pete ya ndoa na waifu tena mbele ya watoto wangu na majirani zangu na kukimbilia kwa Eddyhep... hii ilitokea baada ya kelele kati ya waifu na Mrithi wangu baada ya mrithi wangu kutukanwa na Remavurugu. Mbali na hayo ndugu zake waifu walianza kunitumia jumbe kali hadi watoto wadogo ambao wako sawa na wanangu .
- Suala la kuhalalisha ndoa ya mwanangu(Mwasuga) na mtoto wa kaka yake(Elishadai) tena kwa kuvunja ndoa halali ya Mwasuga bila kuogopa viapo vya wawili hao na hata Mungu.
Kwa kuzingatia hayo na mengine mengi tu ambayo sikuwa na haja kuyaongelea katika waraka huu nawaombeni mtambue kuwa:Tangu nimuoe waifu sijawahi kupeleka neno lolote kwa upande wangu; upande wao; kwa balozi; kwa vyombo vya dini wala kwa watu wenye hekima ili kuficha na kuitunza heshima ya nyumba yangu. Lakini sasa nimeamua kuyaweka wazi kwani naona tumefika pabaya mpaka tunataka kurushana kwenye magazeti? Na ni wazi kuwa upande wa kwetu watashangaa sana kwani waliamini kuwa mimi na waifu twaishi kama paradiso.Je; kichwa, kinaweza kuwa mkia?
ANGALIZO KWENU
Angalizo ni kua nyumba yangu
si nyumba ya kuchezea na kuhalalisha mambo ya kishenzi; kwani, huyo
Remavurugu hadi anakuja kwangu alishafukuzwa na mumewe lakini mi kwa
ujinga wangu nikampa hifadhi bila kujua kua atajiona ni mtawala wa
wanangu ambao bila wao nisingekua na sababu ya kujenga hiyo nyumba
ambayo aliitumia kuwatesea wanangu. Kutokana na hilo niliamua kumtimua
ili asiendelee kuwafadhaisha wanangu katika utawala wao. Ebu fikiri
kwa nini Remavurugu ampangie mwanangu mahali pa kulala tena bila
kuzingatia maadili yetu ya kiafrika? Maana yake ni nini?
Ndio maana nauliza kwa nini
wanangu wafanywe wanyonge katika utawala wao na katika nyumba yao
tena na watoto ambao hawana haki yoyote kwangu zaidi ya kukaribishwa
tu? Nani asimame kuwatetea ? Kwa nini waonewe na kutukanwa wakati
makosa si yao?
Nanukuu maneno ya Remavurugu
dhidi ya mtoto wa dada yake ambaye ni mrithi wangu
“mwajidai mmna nyumba, nyumba,... nyooooo... kwani
hii ndo nzuri kupita zote na mtakufa nayo?... mlisema mi nalala nje
kwa wanaume... ndo maana hutaki kuhamia nnnyumba kubwa mie nkae hapo
nje... ili nisiende kwa hao wanaume wangu; je, mtanilala
ninyi?...haya njoo basi unilale!...njoooo!... Njoooo!...”. Hivi ni
sawa mtoto kuongea hivyo mbele ya wazazi?
Na iumbukwe kua hata siku
nimewaita kupata suluhu alikiri kumtukana mrithi wangu na
nilipomkemea na kumwambia nitamfukuza endapo atarudia alienda
kunichambua huko kwa majirani tena bila hata kumuogopa waifu ambaye
alikua naye wakati akinitukana mi na familia yangu bila kujali
wadhifa na heshima nipewayo na wanajamii … labda alidhamiria
kuharibu utumishi wangu na heshima yangu?
Je, hali hii ilimsikitisha
waifu na nyie au mliona sawa tu, na ni kweli mnakubali mtoto wa
upande wenu aitukane familia yangu kiasi hiki ilhali mmekaa kimya?
Sina uhakika, lakini kama
ndio mtindo wenu; watoto kutukanana kiasi hiki,tena bila kujali kama
huyu ni kaka au yule ni dada naomba msiipandikize hali hiyo maana
kwangu hainaga nafasi... tambueni kua mkubwa ni mkubwa tu na mdogo
atabaki kua mdogo tu; hivyo, lazima maji yafuate mkondo. Nawaombeni tuwaongoze wanetu ili
waheshimiane; wapendane; wajaliane na hata kushirikiana... nasema
hivi lazima wanetu waheshimiane; mbona hata barabarani kuna alama
ziongozazo magari yaende kwa usalama na lazima alama hizo
zizingatiwe. Awekaye alama ni sisi wazazi na madereva ni watoto ambao
lazima tuwabane kuzifuata alama hizo.
Ombi langu ni kua matusi
yaishie hukohuko lakini si kwenye malango yangu; maana sikuwahi kusikia
hata siku moja matusi ya ndugu kwa ndugu kwenye malango ya baba yangu
na ni lazima nizue yasijeyakaanzia kwenye malango yangu, sisi
tulifundishwa kuheshimiana; na kupendana nami najitahidi kuufundisha
uzao wangu so please iacheni familia yangu...
KWA WENYE HEKIMA
Wakati mtu hujaoa au kuolewa
kila kitu upatacho unasema ni kitu changu yaani chako peke yako;
lakini mambo hubadilika pindi unapooa au kuolewa kwani kila
kinachopatikana mtakiita chetu... hapa ubinafsi huisha na tena mkishapta
watoto, wazo hupanuka zaidi na kukiita kila mkipatacho kua ni ni
urithi wa watoto maana hao ndio warithi wa mali zilizochumwa na baba
na mama wala si maneno yangu bali ni toka zamani za uhenguni. Hivyo
basi; si baba wala mama, ambaye anaweza kurithi mali yoyote waliyochuma
pamoja ila watoto pekee.
Sasa basi mimi kama baba;
nikiona nimeshindwa kuishi na waifu, ninatakiwa kuondoka bila kitu
chochote na kuziacha mali zote chini ya waifu na watoto ili waitunze
mali hiyo na kuitumia mpaka Mwenye enzi Mungu wetu atakapoamua
kumchukua waifu na ndipo mali yote itakua ni urithi wa watoto na vivyo
hivyo ikitokea waifu akashindwa kuishi nami na watoto ataondoka na
kuacha mali kwa watoto chini ya uangalizi wangu hadi hapo
nitakapoishiwa pumzi ndipo watoto watarithi mali. Hii ina maana
kwamba baba hana ruksa wala haki, hali kadhalika waifu hana ruksa wala
haki hiyo ya kuchukua mali ya watoto na kama wote wanaondoka ni
dhahiri kuwa wataondoka na kuacha mali zote kwani hizo mali ni urithi
wa watoto tu na si vinginevyo... maana kama wazazi wetu wangefanya
hivyo sisi tungerithi nini wakati kumbe kama ikitokea mzozo wowote
mume au mke anasomba vitu vyote? Na kama mmoja kati yetu ataamua
kuoa(mimi); kuolewa(waifu); au akibaki na watoto azingatie mambo
yafuatayo:
- asijaribu kumleta mwenzi wake katika nyumba ya watoto ili kuepuka manyanyaso yatakayojitokeza
- vitu vyote na nyumba awaachie watoto yeye akaanze maisha mapya na mwenzi wake kwani mali ni ya watoto tu na si vinginevyo.
- Alinde na kuitunza mali yote kwani ni urithi wa watoto.
- Asichukue wala kutoa kitu bila idhini ya watoto wote yaani baada ya kikao cha maridhiano na watoto.
- Asiingize vitu ndani ya nyumba bila watoto kujua maana siku wakiona vinatoka itakua vita kama si shida.
Licha ya hayo nawaomba
wanangu tuache ubinafsi maana nilipitia magumu mengi hadi kuwapatia
elimu nzuri; ambayo, leo hata nikiishiwa pumzi sijutii kwani
nimejithidi kuwapa elimu bora kabisa tena inayoendana na ushindani wa
dunia ya leo. Kila mtu aache kuita vitu vya familia vyangu kama waifu
apendavyo kuviita bali vyenu na mwisho wa siku ni urithi wenu wote...msije kumtupa waifu maana pasipo yeye msingeliona jua na hata kufikia
hapo mlipo... mheshimuni tena mheshimuni sana, maana mzazi ni jiwe
kwani hata likikuangukia litakuumiza na ukiliangukia utaumia vivyo
hivyo.
Nimeamua kusema mapema maana
ninaona wenzangu wako bize kunishambulia kwa maneno na vitendo sasa
ili kuepusha zozo litakalotokea pindi nikilala milele maana kama bado
nipo, wanangu wameshaanza kuteswa na ndugu itakuaje nikikaa kimya
kwenye nyumba ya milele? Nawaachia wosia huu mapema ili kuepusha fujo
endapo wanangu mtachachamaa kudai haki yenu... nisiposema sasa
naamini nitasababisha fujo na uadui. Nawaomba wanangu muwe na
busara endapo itatokea hivyo na huu waraka utakua ndio nguzo na kinga
ya haki yenu tuliyowatafutia na waifu kipndi chote cha maisha yetu ya
furaha. Huu ni wosia wangu kwenu … take care my children...
nawapenda sana.
KUMBUKENI
Familia nyingi ; baada ya
vifo vya baba zao, mtoto mkubwa wa kiume huweka kitini na kupewa
madaraka ya kuiongoza familia. Lakini mara nyingi vijana hawa
hukutana na vikwazo mbalimbali kutoka kwa mama zao; ndugu na hata
watu wengine wa karibu ili kusambaratisha familia hizo. Watu hawa
hutumia mbinu mbalimbali kuwachanganya; kuwagombanisha; na hata
kuwagawa watoto wa familia hizo kwa kupandikiza chuki kati yao, hasa
kwa kutumia uongo ili kuwatawala na pengine kumiliki mali zilizoachwa
na wazazi zao. Nawaomba wanangu msije ruhusu jambo ka hilo kuwakuta naomba
mkadumishe umoja wenu niliowaachia na kuwasisitiza ili muishi kwa
amani tena kwa kupendana sana.
Kwa kumalizia napenda
kukuulizeni shemeji zangu;
- je,kwa maelezo hayo yote niliyokufafanulia nani alipaswa klaumiwa kuhusu misiba?
- Je umegundua kua dada zako(waifu na mavurugu) uhusiano wao si wa nuru?
- Je hao wajomba zako(Remavurugu na Nyakwehe) ambao wanawasumbua wanangu kwa matusi hayo madili unakubaliana nayo?
- Na nina haki yoyote kupinga matendo yenu?
Vyovyote ufikiriavyo; mimi
kama baba wa familia hii,nitasimama imara kuitetea familia yangu na
vitu vyake. Na pia nawaomba wanangu msimame pamoja nami... tambueni
kuwa wema ni akiba na ubaya ni akiba pia. Mungu yupo awainuaye
wanyonge; na kwa uwezo wake nasi tutainuka kwa maana Yeye hamtupi
mjoli wake.
ZINGATIENI WANANGU
Wanangu katika andiko hili
nawaagiza na kuwaomba mpendane;
mheshimiane;
mthaminiane;mhurumiane; msaidiane; mlindane; na muwe na
umoja wenye nia moja, lugha
moja, sauti moja na uamuzi mmoja. Mkifanya
hivyo hakuna hata mmoja
atakayewachezea au kujaribu kuwatenganisha
kwani mtaheshimiwa na
kuogopwa kupitia umoja wenu; na hata, siku
nikiondoka hapa duniani
mtabaki na waifu ambaye atakuwa ndiye mshauri
wenu kabla na yeye
kuchukuliwa na Mwenye enzi Mungu maana naamini
hatutawazika wenetu ila nyie
ndo mtuzike sie. Kumbukeni kuwa kiongozi
wa familia ni yule mtoto
atakayepewa madaraka kwa kuketishwa kitini na
wazee wa mila au wa ukoo na
lazima wanangu wote mmheshimu huyo kwani
ndio atakayekua baba yenu
badala yangu... kila tukio katika familia
lazima liongozwe na kiongozi
huyo ambaye ndiye atakuwa mwenyekiti wa
kila kikao na watoto wengine
watakua wajumbe wakati waifu atakuwa
mshauri wenu na mmheshimu
sana kwa ushauri mzuri na mrekebisheni kwa
heshima na hekima pale atoapo
ushauri usiofaa. Kiongozi wa familia
unatakiwa kuwaheshimu wajumbe
pamoja na waifu ikiwa ni pamoja na
kuwasahihisha; kuwashauri na
kuwaonya kwa heshima na hekima ikiwa
imefikia wakati umeshindwa
kuwaunganisha ndugu zako, washirikishe wazee
wenye hekima watakuongoza
njia nzuri ya kutatua aina yoyote ya mapito
yako.
Nawakumbuka pia wanangu wa
kike ambao ni dada zenu kuwa haki zao ni
sawa kabisa na nyie hata kama
walishaolewa zamani sana na kutoshiriki
kikamilifu katika kuinua
uchumi wa familia yenu. Naamini kwa ukarimu
na upendo niliwaonesha
wanangu hamtaweza kuwanyanyasa dada zenu hasa
pale wanapokuwa na
uhitaji...kwa sababu ninyi watoto wa kiume
mmeshiriki kwa kiasi kikubwa
kuifikisha familia yenu hapo ilipo; mna
mamlaka makubwa kutokana na
jasho lenu kumwagika kwa kiasi
kilichowezesha sisi kuwa na
hali hii kiuchumi.
Hivyo basi kama dada zenu
wakiomba kupewa haki yoyote wanapaswa kuomba kwa adabu na utii na
wakifanya hivyo, nawaomba muwafikirie maana
nao ni damu yenu na wana haki ya kurithi
mali ila watambue kuwa
mmewapa haki hiyo kwa neema tu maana
niliwapatia elimu nzuri
ambayo wamepeleka matunda yake huko
walikoolewa... na tambueni
kuwa mnatakiwa kuwalinda dada zenu na
mhakikishe mnawatembelea
kujua kama wanaishi kwa amani maana mwajua
kuishi nje ya nchi ni sawa na
utumwa. Zingatieni maneno haya maana
yawezekana sitakuja bahatika
kutoa wosia wangu kwenu maana hakuna
anayetambua ni lini kifo
kitampata. Mkijenga upendo kati yenu
mtabarikiwa sana... maana
Mungu hubariki nyumba yenye amani; furaha;
upendo;utulivu na maelewano.
Kila mkipatacho gawaneni kwa amani;
upendo; haki na usawa ili
kuepuka magomvi na kukaribisha baraka na
rehema za Mungu , na hakika
kupitia hayo mtabarikiwa. Wenye busara
wanadai kua atafutaye mali au
kufanikiwa kwa kuwasukuma wenzake;
kuwadunisha; au kwa njia
zisizo halali na zile za kishirikina hung'aa
kwa muda na baadaye huwa
masikini kuliko watu wote na ataondoka kwa aibu
duniani hapa. Tena kumbukeni
maneno yangu niliyowaeleza tangu mkiwa bado wadogo, kipindi kile ni mwalimu; kuwa
muepuke kujenga karibukaribu kama inavyojionesha katika picha .
Kielelezo picha kutoka
jamiiforum(google.com)
tena sitaki kabisa mkae
karibu na ndugu zenu ili kuepusha magomvi ya waifu
na wake zenu hata kelele za
mawifi... nyie wenyewe ni mashahidi kilichotokea kwa
mwalimu mwezangu ambaye kila
siku alisuluhisha magomvi kati ya watoto (wao kwa
wao); mama mkwe na wakwe zake pamoja na
mawifi dhidi ya mawifi hadi
kupelekea familia ile kusambaratika kwa
aibu kubwa. Kutokaka na nyie
kutosikia na mkaamua kukaa karibu karibu na ndugu zenu tena hao wenye
kuwachukia ni wazi kuwa mtafarakanishwa na kugombanishwa kitu
kitakachopelekea kutoelewana katika maisha yenu. Hivyo basi
nawaombeni mkasikie maneno yangu kwani nayanena ili kuwafanya muelewe
kuwa ni sharti mpendane na kuthaminiana bila kuwepo kwa chuki wala
masimango yasomaana. Mkizingatia hayo hamtofika katika mafarakano ila
kupendana na kuheshimiana kama nilivyowaamuru na kuwahusia.
Zingatieni hayo mkaishi kwa
amani na upendo ili msiishe kuilinda amani ya ukoo wenu.
Kama isemavyo biblia takahai
katika wakolosai 3 na 4 na haya ni baadhi tu maneno katika sura hizo
yawafaayo ninyi:
“Elekezeni mioyo yenu
kwenye mambo ya juu, alikokaa Kristo, upande wa
kulia wa Mungu. Yafikirini
mambo ya juu na siyo mambo ya hapa duniani.
Basi, yaangamizeni kabisa
mambo yote yanayotokana na asili yenu ya
kidunia: uasherati, mawazo
machafu, tamaa mbaya, nia mbaya na choyo
ambayo ni ibada ya sanamu.
Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu
inakuja. Ninyi mlikuwa
mkitenda mambo haya katika maisha yenu ya
zamani. Lakini sasa ni
lazima mwachane kabisa na mambo kama haya:
hasira, ghadhabu, nia
mbaya, matukano na maneno machafu kutoka
vinywani mwenu. Msiambiane
uongo kwa maana mmekwisha vua utu wenu wa
zamani pamoja na matendo
yake na kuvaa utu upya ambao unaendelea
kufanywa upya katika
ufahamu ili ufanane na Muumba wake. Katika hali
hii hakuna tena tofauti
kati ya... aliyetahiriwa na
asiyetahiriwa, mtu
aliyesoma na asiyesoma, mtumwa na mtu huru. Bali
Mfalme ni yote na
yumo ndani ya wote. Basi, kwa kuwa ninyi ni wateule
wa Mungu, wapendwa na
watakauhai, vaeni moyo wa huruma, wema,
unyenyekevu, upole na
uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana kama mtu
ana malalamiko kuhusu
mwenzake. Sameheni kama Bwana alivyokwisha
kuwasamehe. Juu ya haya
yote, vaeni upendo ambao unaunganisha mambo
haya kuwa kitu kimoja
kilicho kikamilifu.
Ruhusuni amani ya Mfalme
itawale mioyoni mwenu kwa kuwa ninyi kama
viungo vya mwili mmoja
mmeitiwa amani. Tena muwe na shukrani. Neno la
Mfalme lidumu ndani
yenu kwa wingi, mki fundisha na na kuonyana katika
hekima yote; na huku
mkiimba zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni na
mkiwa na shukrani kwa
Mungu mioyoni mwenu. Na lolote mtakalofanya,
ikiwa kwa neno au kwa
tendo, fanyeni yote katika jina la Mfalme,
mkimshukuru Mungu Baba
kupitia kwake.
Mtu atendaye uovu atalipwa
kwa uovu wake, wala hakuna
atakayependelewa. Ninyi
mabwana, watendeeni watumwa wenu haki na
ilivyo sawa mkitambua ya
kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.
Dumuni katika maombi,
mkikesha na kushukuru. Muwe na hekima katika
uhusiano wenu na watu
wasioamini, mkiutumia wakati wenu vizuri.
Mazungumzo yenu yawe ya
unyenyekevu wakati wote, yawe ya kuvutia, ili
mjue jinsi ya kumjibu kila
mtu.”
Hayo ni maneno yangu kwenu wanangu nikiwahusia mema katika dunia hii
ya mateso kwa wale waaminio na raha sana kwa wale wasoimani ya Mfalme
wa kweli... Pia nawaombeni wanangu muwe makini sana na ibada za
machukizo na makufuru ambazo nyingi zao twazifanya hali tukiamini
kuwa twamwabudu Mfalme wa kweli kumbe si kweli... nawasihi wanangu
kusoma sana neno la Mwenye enzi Mungu ili kuitafuta sauti yake na
kuisikiliza hiyo baada ya kuipata...hali mkijua kusamehe na
kujihurumia na ile hukumu ya Mfalme ibebayo ghadhabu ya Mwenye
kutuumba....
Na pia nawatakia mashemeji zangu maisha yenye baraka tele kwani mimi
nilishawasamehe zamani sana ndio maana nilikuwa kimya kwa muda mrefu
saana mlipokuwa mkinilaumu na kunishutumu...
Mungu awajalie hekima katika kuishi na watu na ninawaomba mnisamehe
pale nilipowakosea ikiwa ni pamoja na kusimama katika kweli ya Mwenye
enzi Mungu wetu mwenye kutubariki na kutujaalia amani yake...msiache
kumpenda na kumuabudu Yeye maana pasi yeye hakuna
liwezekanalo...tubuni maana hukumu yake ipitayo fahamu zote yaja
upesi; kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri ya kuwa hukumu yake
Mfalme ni ya kweli na haki baasi tuyaache maoovu yetu … wala
tusiabudu mali kwani mali si kitu wala chochote mbele za Mwenye enzi
Mungu...
Pia
naihusia familia yangu kuwa zingatieni mafundisho yangu na mkaishi
kwayo. Kwa kuwa na lugha moja; sauti moja; nia moja; usemi mmoja; na
uamuzi wa pamoja... Mkiishi katika hayo mtafanikiwa katika
dunia hii...
Nawatakia
kheri na fanaka katika maisha yenu .
Asanteni saaaaana..
Ni mimi Sa Masalu.
Asanteni saaaaana..
Ni mimi Sa Masalu.
Alpha Hezron Mayengo ni muhitimu katika kitivo cha elimu; akijihusisha na masomo ya historia na kiswahili katika ndaki ya Mtakatifu Agustino-Mwanza Tanzania. Alihitimu elimu yake mwaka 2016, na kuanza kujishughulisha na uandishi wa vitabu kabla ya kujihusisha na kazi nyingine. Ni mmiliki wa blog pia inayojulikana kama alphamayengoh@blogspot.com ambayo imejaza mambo mengi yanayokuza lugha yetu ya Kiswahili.
Nawatakia kheri na fanaka katika maisha yenu .
Asanteni saaaaana..