Monday, August 1, 2016

Maana ya fasihi simulizi na tanzu zake kwa mujibu wa wataalam mbalimbali


Maana ya fasihi simulizi
Fasihi simulizi ni sanaa ya matumizi ya lugha ya kubuni inayosambazwa kwa mdomo kwa njia ya kuimbwa, kughaniwa, kuigizwa, kusimuliwa, kuumbwa, kufumba au kutegeana mafumbo na vitendawili (Syambo na Mazrui, 1992:2) katika King’ei na Kisozi, (2005:7).
Mulokozi, (1996:24) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni fasihi iliyotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi. Ni tukio linalofungamana na muktadha (mazingira) fulani wa kijamii au wa kutawaliwa na mwingiliano wa mambo kadhaa wa kadhaa kama vile, fanani, hadhira, fani, na maudhui yaliyokisudiwa na mwasilishaji.
TUKI, (2004) fasihi simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile, hadithi, ngoma na vitendawili. Aidha, fasihi simulizi ni ile ambayo inapitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kupitia neno la mdomo (Ngure, 2003:1).
Kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo ambapo kuna uambatanishaji wa utendaji katika uwasilishaji huo. Fanani na hadhira huonana ana kwa ana jambo ambalo huwafanya hadhira kushiriki katika baadhi ya utendaji. Kwa mfano, kuimba, kucheza, au kupiga makofi na vigelegele.
Tanzu za fasihi simulizi
Wamitila, (2003) anadai kuwa tanzu ni istilahi inayotumika kuelezea au kurejelea aina za kazi mbalimbali za kifasihi.
Hivyo basi, kutokana na maana ya tanzu iliyotolewa na Wamitila, (2003) tunaweza kusema kuwa tanzu ni istilahi ya kifasihi inayotumika kumaanisha matawi au mafungu katika kazi za fasihi. Tanzu za fasihi simulizi zimeainishwa kwa namna tofauti tofauti kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali kama ifuatavvyo:


Wamitila, (2008) katika uainishaji wake wa fasihi simulizi anazigawa tanzu za fasihi simulizi katika makundi yafuatayo:
Simulizi au hadithi; huu ni utngo wenye visa vya kubuni au halisi unaowasilishwa kwa lugha ya nathari kwa kusudi la kuburudisha, kukuza maadili na kuunganisha jamii. Katika usimuliaji wa hadithi fanani huwa mfaraguzi ili asiwachoshe watazamaji wake kwa kuingiza utendaji unaowashirikisha watazamaji wake.
Maigizo; ni sanaa inayotumia utendaji kuiga tabia au matendo ya watu wengine au viumbe wengine ili kuburudisha au kutoa ujumbe kwa jamii. Maigizo ni sanaa inayopatikana katika makabila mengi ya kiafrika na huambatana na utambaji wa ngoma. Kwa mfano, jando na unyago, malumabno ya watani na vichekesho.
Ushairi (nyimbo); ni sanaa ya uimbaji inayoambatana na mdundo wa ngoma au mziki ili kufikisha ujumbe kwa hadhira. Katika fasihi simulizi nyimbo huambatana na mdundo wa ngoma na mara nyingi nyimbo hizi huwa na mkutdha kulingana na ujumbe uliolengwa. Hivyo basi, tunapata nyimbo za ndoa/arusi, jando/tohara, hodiya, kimai, nyimbo za mazishi, nyimbo za kidini, nyimbo za kizalendo na nyimbo na mapenzi.
Semi; ni mafungu ya maneno ambayo hutumiwa kuleta maana nyingine badala ya maneno halisi ya maneno yaliyotumika. Katika fasihi ya Kiswahili semi hujumuisha nahau, misemo na methali. Kwa mfano, tukisema mtu amegonga mwamba hatumanishi kwamba amepiga jiwe kubwa kwa mkono au kwa kifaa chochote, bali tunamanisha kwamba ameshindwa kuendelea katika jambo fulani.





Mazrui & Syambo, (1992) wanasema kuwa fasihi simulizi ina tanzu zake ambazo ni tofauti na zile za fasihi andishi ingawa kuna baadhi amabazo zinafanana na zile za fasihi andishi. Fasihi simulizi ina tanzu kuu nne ambazo tunaziainisha kama ifuatavyo:
Ngano au hadithi; ni tungo yoyote ya kubuni inayosimuliwa kwa lugha ya nathari. Katika fasihi ya Kiswahili ngano ni za aina nyingi lakini zote huanza kwa njia inayofuata mtindo huu:
Msimulizi : Paukwa!
Msikilizaji : Pakawa!
Msimulizi : hapo zamani za kale palitokea…
Nyimbo au mashairi; kuna nyimbo za aina nyingi katika fasihi ya Kiswahili lakini zinazokusudiwa hapa ni zile zilizotungwa kwa mdomo (bila maandishi) na kusambazwa kwa mdomo. Nyimbo za aina hii zimeenea katika maisha ya Kiswahili na huwafata tangu wanapozaliwa mpaka kufa kwao. Nyimbo hizi kwa kawaida huwa zinafungamana na ngoma au michezo fulani na mara nyingine huimbwa pamoja na mziki kwa mfano, nyimbo za sherehe, nyimbo za watoto, nyimbo za taarabu na bembezi.
Methali; hii ni misemo mifupi yenye hekima fulani ndani yake. Methali hudhihirisha mkusanyiko wa mafunzo waliopata watu wa vizazi vingi vya jumuia fulani katika maisha yao. Methali hutumiwa sana katika mazungumzo ya kawaida ya waswahili na ni sehemu moja muhimu katika fasihi simulizi ya Kiswahili. Methali nyingi za Kiswahili huwa na mdundo maalumu wa kishairi na mara nyingine huwa na vina.
Vitendawili; ni tungo fupi ambazo huwa na swali fupi lisili wasi na jibu kwa makusudi ya kupima ufahamu wa hadhira kuhusu mazingira yake. Anayetoa kitendawili huuliza swali lake kwa kutoa maelezo mafupi yanayorejelea umbo la kitu hicho, sauti harufu au kukifananisha na kitu kingine. Anayejibu huhitaji kufkiria haraka na kutoa jawabu ambalo huwa na neno moja au maneno mawili hivi. Vitendawili huwa na mianzo maalumu kulingana na jamii yake. Katika fasihi simulizi vitendawili huwalenga watoto ili kuchochea fikra na kuwazoeaza mazingira yanayowazunguka.
Mulokozi katika makala yake ya tanzu za fasihi simulizi iliyo katika jarida la Mulika Na 21 (1989) amezigawa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kwa kutumia vigezo viwili ambavyo ni:
  1. Umbile na tabia ya kazi inayohusika; katika kigezo hiki, Mulokozi ameangalia vipengele vya ndani vinavyounda sanaa hiyo na kuipa mwelekeo au mwenendo. Baadhi ya vipengele hivyo vya ndani ni namna lugha inavyotumika kishairi, kinathari, kimafumbo, kiwingo au kughani, muundo wa fani hiyo na wahusika.
  2. Muktadha; ambapo amezingatia kuwa fasihi simulizi ni tukio, hivyo huambatana na mwingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha, watu na mahali. Mwingiliano huu ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio unaoamua fani fulani ya fasihi simulizi ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi kwa hadhira kwenye wakati na mahali hapo. Hivyo hadithi inaweza kugeuzwa wimbo, utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo unaweza kugeuzwa ghani au usemi kutegemea muktadha unaohusika. Kwa hiyo, Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kama ifuatavyo:
Masimulizi; hii ni tanzu ya fasihi simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha iliyotumika katika masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo cha muundo kimetumika mara nyingi masimulizi huwa na muundo unaojitofautisha na tanzu nyingine kama vile ushairi. Mara nyingi katika masimulizi muundo wake huwa ni wa moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio. Vile vile kigezo kingine ni cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusishwa wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji na watendwaji. Kigezo kingine ni kigezo cha namna ya uwasilishwaji. Katika uwasilishwaji, huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni mandhari ambayo huwa ni maalumu kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika muda maalumu, kwa mfano baada ya kazi. Masimulizi yamegawnyika katika tanzu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu za kisa huwa (kihistoria).
Utanzu wa semi; semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mkato na kigezo kingine ni cha kidhima ambacho hufunza. Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo: methali, vitendawili, misimu, mafumbo na lakabu.
Ushairi; huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vinavyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji wa ughani. Vipera vya utanzu huu ni nyimbo na maghani.
Utanzu wa mazungumzo; mazungumzo ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi, ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii fulani. Vigezo vinavyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayolojia. Vipera vya utanzu huu ni hotuba, soga, mawaidha, malumbano ya watani na ulumbi.
Maigizo; ni michezo ambayo hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na hutoa ujumbe fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu na wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha, kuelimisha au kuonya. Pia kinatumika kigezo cha mandhari ambapo maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe fulani na katika matukio ya kijamii.
Ngomezi; ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo vinavyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Kwa mfano, taarifa hiyo yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.
Vile vile Okpewho, (1992) amazigawa tanzu za fasihi simulizi kwa kuzingatia vigezo vinne kama ifuatavyo:
  1. Kigezo cha unguli; katika kigezo hiki kuna jitokeza ngano zosozohusu wanadamu. Kuna ngano za wanyama, ngano za vichimbakazi na ngano za miungo. Hata hivyo kigezo hiki kinaonekana kuwa na matatizo kadha wa kadha kama vile kufanana kitabia kati ya jamii moja na nyingine, kupuuza namna mbalimbali katika ngano ambazo vichimbakazi, wanadamu na wanyama huhusiana.
  2. Kigezo cha lengo la ngano husika; katika kigezo hiki ngano zinaainishwa kwa kuzingatia lengo la simulizi husika. Hapa panajitokeza ngano za kimaadili, ngano za kuhimiza kazi na zinginenzo.
  3. Kigezo cha sifa ya ubora wa ngano; ni kigezo ambacho ndicho kinaonekana kubeba kundi kubwa la ngano. Katika kigezo hiki kuna ngano ayari (ambazo huambatana na uelevu au ulaghai wa wahusika) ngano za mtanziko kama vile zinazohusu vita , vizazi, mashujaa na zinginezo.
  4. Kigezo cha muktadha au utendaji wa ngano husika; katika kigezo hiki kinachoangaliwa ni ngano inatendwa wakati gani na katika mazingira gani. Kwa mfano, kwa kutumia kigezo hiki tunaweza kupata ngano za mbalamwezi, ngano za ibada, ngano zinazotendwa wakati wa mapumziko ya wawindaji na zinginezo.
Hivyo basi, Okpewho, (1992) amezigawa tanzu za fasihi simulizi katika makundi yafuatayo:
Nyimbo na maghani; ni sanaa ya kuwasilisha ujumbe kwa hadhira inayoambatana na mdundo wa ngoma au mziki. Katika uimbaji fanani hutoa sauti inayoendana na mapigo ya ngoma au mziki. Aghalabu nyimbo hizi huweza kuimbwa katika tukio maalumu. Hivyo basi, tunaweza kuainisha nyimbo katika makundi mablimbali kama vile bembezi, mbolezi, sifo na zinginezo.
Masimulizi; ni visa vya kubuni au halisi vinavyowasilishwa kwa hadhira kwa kutukia lugha ya nathari. Katika masimulizi fanani huwasilisha ujumbe wake kwa njia ya kuisimulia hadhira yake kwa kutumia mbinu mbalimbali zinazoambatana na utendaji.
Semi; ni tungo fupi fupi zenye hekima na busara ndani yake. Mara nyingi kinachozungumzwa ni tofauti na kilichokusudiwa. Wakati mwingine tungo hizi hutumika ili kuipa adabu lugha ya mzungumzaji. Kwa mfano, Juma ana mkono wa birika katika tungo hii tukifasili kuwa juma anamkono unaofanana na wa birika tunapoteza maana ya tungo hiyo.
Ngonjera; ni nyimbo ambazo huhusisha waimbaji zaidi ya mmoja, uimbaji wao huwa katika mfumo wa majibizano. Aidha utanzu huu huweza kuitwa kuwa ni ushairi wa maigizo maan huwa kuna jambo ambalo waimbaji hawa hulumbana ingawa mwishoni hufika hitimisho kwa mmjo wao kukubaliana na mawazo yaw engine.
Aidha, Balisidya, (1987) anaigawa fasihi simulizi katika tanzu tatu kama ifuatavyo:
Nathari; katika nathari anatoa vipera kama vile ngano-istiara, harafa na hekaya, tarihi-kumbukumbu, shajara, hadithi za kihistoria pamoja na epiki, visaasili- kumbukumbu na tenzi.
Ushairi; katika ushairi kuna vipera kama vile nyimbo-tahlili, bembea, tumbuizo, ngoma, miviga, watoto na kwaya, maghani, majigambo, vijighani, shajara, pamoja na tenzi.
Semi; katika utanzu huu kuna vipera kama vitendawili, misimu, mafumbo, methali-msemo na nahau, misimu-utani, masaguo na soga.
Tukiwaangalia wataalamu hawa wanatofautina katika ugawaji wa tanzu za fasihi simulizi jambo ambalo linaleta mkanganyo mkubwa sana kwa wagenzi na wasomi wa fasihi simulizi. Hata hivyo mtazamao unaoelekea kuwa na mshiko zaidi ni ule wa Mulokozi ambaye anazigawa tanzu za fasihi simulizi katika aina sita ambazo ni masimulizi (hadithi), semi, ushairi, mazungumzo ya kisanaa, maigizo na ngomezi.

Utata katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi
Vigezo vya uainishaji; baadhi ya wataalamu wametumia vigezo vya uainishajia mbavyo vinatofautina kati ya mwandishi mmoja na mwingine. Lakini pia watalaamu weingine kama kama vile Wamitila, (2008), mazrui & Syambo, (1992) hawajaonesha vigezo vyovyote vya uanishaji wa tanzu za fasihi simulizi jambo ambalo linaleta utata katika uainishaji kwani ni vigumu kubaini ni yupi uainishaji wake upo sahihi.
Utofauti wa Idadi katika tanzu zinazoainishwa; uainishaji wa tanzu hizi unatofautiana katika idadi wanazoainshisha wataalamu mbalimbali. Kwa mfano, Mulokozi katika jarida la Mulika Na 21 (1989) anadai kuna tanzu sita (6), Balisidya, Matteru(1987) anainisha tanzu tatu (3), Wamitila, (2008) na Okpewho, (1992) wanaainisha tanzu nne (4) za fasihi simulizi. Hivyo kutofautina kwa idadi za tanzu zinazoainishwa na watalaamu mbalimbali kunazua utata kwani ni vigumu kuhitimisha kuwa ni nani yupo sahihi.
Kuingiliana kwa tanzu; katika uainishaji wa watalamu mbalimbali baadhi ya tanzu zinaingiliana ingawa hutofautiana katika vigezo vya uainishaji wao na wengine kukosa vigezo kabisa. Hivyo basi kuingiliana kwa tanzu hizo huweza kuleta utata. Kwa mfano, Okpewho, (1992) ameainisha utanzu wa ngojera ambao unaingia katika utanzu wa ushairi kama ilivyoainishwa na Wamitila, (2008), Mulokozi, (1989). Lakini pia utanzu wa semi umeonekana katika kila uainishaji ingawa kuna utofati unaojitokeza katika uainishaji wao.
Utofauti wa isitlahi za uainishaji; baadhi ya wataalamu wametofautina katika isitilahi za uainishaji ingawa hurejelea utanzu mmoja au dhana moja. Kwa mfano, Balisidya & Matteru, (1987) anatumia istlahi nathari, Wamitila, (2008) ametumia hadithi, Okpewho, (1992) na Mulokozi, (1989) ametumia istilahi masimulizi. Tukichunguza istalahi hizo, tunapata dhana moja tu inayorejelewa na kuleta utata katika uainishaji.
Tanzu za fasihi simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui; baadhi ya tanzu za fasihi na vipera vyake huweza kubadilika kulingana na wakati. Kwa mfano utanzu wa hadithi katika kipindi cha sasa huwasilishwa tofauti na ulivyowasilishwa zamani, hivyo basi hukosa uhalithia wa hadithi kama utanzu wa fasihi simulizi kitendo ambacho waainshaji hushindwa kutengeza kigezo cha kuainisha utanzu huu.
Hivyo basi, tunahitimisha kwa kusema kuwa, fasihi simulizi kama fasihi zingine ina dhima muhimu katika jamii. Dhima za fasihi simulizi ni kama vile kuelimisha jamii, kufundisha jamii, kutabirii na kutoa mwelekeo wa jamii, kuhifadhi historia ya jamii na kuonya jamii. Pia kupitia fasihi simulizi wasimuliaji hukuza ubunifu wao kwa kutongoa masimulizi au hadithi mbalimbali. Fasihi simulizi ni chanzo kikubwa cha fasihi andishi kwani karibu vipengee au tanzu zote za fasihi andishi zimetokana na fasihi simulizi. Kwa mfano, riwaya chanzo chake ni hadithi, tamthiliya hutokana na sanaa za maonesho, semi mbalimbali za fasihi simulizi hupatikana katika fasihi andishi. Utanzu wa ushairi umetokana na ushairi simulizi ambao zamani ulikuwa ukiwasilishwa kwa uimbaji au kughani fasihi simulizi hukuza upeo wa kufikiri na ubunifu kwa hadhira kupitia elimu inayopatikana kupitia masimulizi mbalimbali.




MAREJELEO
Balisidya, M. L (1987). Tanzu na Fasihi Simulizi Katika Mulika Nambari 19. Dar es salaam:
TUKI
Kirumbi, P. S (1975). Misingi ya Fasihi Simulizi. Nairobi: Shungwaya Publishers Ltd
Mazrui, A & Syambo, B (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational
Publishers.
Masebo, J. A & Nyangwine, N (2008). Nadharia ya Fasihi. Dar es salaa: Nyambari Nyangwine
Publishers.
Msokile, M (1992). Kunga za Fasihi na Lugha. Dar es salaam: DUP
Mulokozi, M. M (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi Katika Mulika 21. Dar es salaam: TUKI
Mulokozi, M. M (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. Dar es salaam: TUKI
Ngure, A (2003). Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Toleo la pili). East Africa:
Oxford University Press na TUKI
Wamitila, K. W (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobo: Focus Publication Ltd
Wamitila, K. W (2008) Kanzi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi: Vide-
Muwa Publishers Ltd.
Okpewho, I (1992) African Oral Literature. Backgrounds Character and Coninuity.
Bloomington: Indian University Press.

1 comment:

  1. Mbona hakuna maana ya Tanzu za Fasihi simulizi kwa mujibu wa mtaalamu hata mmoja ?

    ReplyDelete

hakiki na tuma maoni au mapendekezo kuhusu makala hii ya andiko langu la uchunguandiko langu

ANDIKO LA UCHUNGU (Kwa shemeji zangu na wanangu)           NYAMBUYA OGUCHU,                            S.L.P 777666,       ...