Tofauti kati ya nadharia ya fonolojia asilia na nadharia ya fonolojia zalishi.
Nadharia ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya
au kutekeleza jambo Fulani (Mdee na wenzake, 2011 katika Matinde, 2012:247)
Massamba, D.P.B. (2004:64) anasema kuwa nadharia ni kanuni na misingi ambayo
hujengwa katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa kama kiolezo ya kueleza
jambo. Kutokana na maelezo hayo tunaweza kusema kwamba nadharia ziliibuliwa na
wanafonolojia katika jitihada zao za kujaribu kuelewa na kufafanua sarufi majumui.
Kwa ujumla, nadharia huweza kufafanuliwa kama maelezo ya jambo yaliyofungamana
na vigezo vilivyowekwa au vilivyozalishwa kutokana na uchunguzi uliofanywa. Katika
utekelezaji wa uchunguzi wa jambo sharti mwanaisimu aongozwe na mwongozo maalumu
unaoogozwa na vigezo vilivyowekwa na wataalamu mbalimbali.
Nadharia za fonolojia ni mwongozo unaomuelekeza mwanaismu au mtu anayefundisha
fonolojia au mwanangenzi wa fonolojia kuifahamu fonolojia ya lugha katika vipengele vyake
vyote ili kujijengea utaratibu maalumu utakaomwezesha kuchunguza ubora na udhaifu
unaojitokeza katika nadharia nyingine za fonolojia. Katika uchanganuzi wa vipengele vya
kifonolojia lazima tuongozwe na mwongozo maalumu uliokubaliwa kwa vigezo vilivyowekwa
katika utekelezaji wa jambo hilo.Nadharia zijulikanazo katika uwanja huu wa fonolojia ni kama
vile fonolojia zalishi, fonolojia asilia, fonolojia zalishi asilia, fonolojia vipande sauti huru,
fonolojia umbo upeo, fonolojia mizani, fonolojia atomiki na fonolojia leksika.
Sababu za kuibuka kwa nadharia za fonolojia.
Kwanza, hakuna nadharia inayojitokeza katika ombwe bali nadharia yoyote mpya
itakuwa ama imeboresha nadharia iliyokuwepo hapo awali au inaikataa na kuipinga ile ya awali.
Katika uboreshaji wa nadharia ya awali ni muhimu kuelewa kwanza kipi kinafanyiwa maboresho
katika nadharia husika na kwa upande wa kupinga ni vyema kufahamu vipengele gani
vinapingwa na nadharia mpya katika nadharia ya awali kwa kutoa mifano kuntu.
Pili, si rahisi kuielewa nadharia mpya kinagaubaga bila kuielewa au kuzielewa nadharia
zilizotangulia kwani ubora na uelewa wa hiyo mpya unategemea kuielewa vizuri nadharia ya
awali.
Fonolojia zalishi ni mkabala wa kinadharia unaochunguza kanuni na sheria za
kimajumui zinazoonesha jinsi gani umbo la ndani na la nje yalivyokuwa yanahusiana
(Massamba, 2011:274). Waasisi wa nadharia ya fonolojia zalishi ni Noam Chomsky na Morris
Halle ambao wametililia mkazo katika uwepo wa umbo la ndani na umbo la nje katika
uwakilishi wa vipengele vya kifonolojia na kuonesha uhusiano uliopo baina ya maumbo haya.
Chomky na Halle wametoa sheria bunifu zinazo ongoza ukokotoajia wa maumbo hayo na kuziita
michakato ya kifonolojia. Fonolojia zalishi imechunguzwa na waasisi hao katika kitabu chao
maarufu kiitwacho Sound Pattern of English yaani “Ruwaza ya sauti katika lugha ya kiingereza
1968”. Fonolojia zalishi imejengwa na misingi ifuatayo:
(i) Maumbo na miundo yote ya lugha ya binadamu hutokana na umbo la ndani ambayo
hujengeka taratibu katika akili ya msemaji mzawa tangu anapoanza kujifunza lugha
akiwa mtoto mdogo mpaka anapopata umilisi kamilifu wa lugha yake.
(ii) Maumbo na miundo ya maneno tutamkayo katika vinywa vyetu huwakilisha umbo la nje
umbo ambalo kwa kiasi kikubwa huakisi umbo la ndani ama moja kwa moja au baada
ya kufanyiwa marekebisho kidogo.
(iii)Sauti zote zitumikazo katika lugha asilia za binadamu hutokana na mifumo ya
mkondohewa ambayo ama inakwenda ndani ya mapafu au inatoka nje ya mapafu ya
mzungumzaji. Mkondohewa hudhibitiwa na ala za matamshi katika jinsi na mahali pa
kutolewa au kuingia kwa hewa mapafuni.
Fonolojia asilia ni nadharia inayochunguza sulubu za sauti zitumikazo katika lugha ya
binadamu zilizomo katika maumbile ya binadamu yanayohusu usemaji na masikizi; kwamba
nguvu za kifonetiki katika sauti hujitokeza kupitia michakato ambayo inahusiana na
ubadilishanaji wa sauti katika akili na bongo zetu, Massamba (2011:117) Nadharia hii iliibuliwa
na David Stampe (1973) na baadaye kuungwa mkono na Donegan Patricia (1979). Pia
wanafonolojia hao wanatoa maoni kuwa michakato inayofanyika katika nadharia hii haitegemei
sheria wala kanuni bali huwa ni michakato asilia iliyo katika maumbile ya binadamu. Nadharia
hii iliibuka kushughulikia matatizo yaliyosababishwa na Kiunzi Rasmi cha Fonoloja Zalishi
kama vile udhahania na urasmi kanuni katika uwakikishi wa kifonolojia kwa malengo ya
kuboresha nadharia hiyo kwa kuifanyia marekebisho. Fonolojia asilia ina misingi ifuatayo:
(i) Fonolojia asilia inaelezea kipengele cha kifonoloja kama mwitikio asilia wa mahitaji,
uwezo na ulimwengu wa watumiaji wake.
(ii) Nadharia hii inaonesha hali halisi jinsi mambo yalivyo, kwa maana kwamba imekusudia
kuifafanua mada yake yenyewe.
(iii)Kipengele asili cha fonetiki katika fonolojia ni tofauti kabisa na kiengele cha kikaida cha
kifonetiki, kimaumbile, kimageuko, kisaikolojia na kiutokeaji wake.
(iv)Nguvu za kifonetiki katika sauti hujitokeza kupitia michakato ambayo inahusiana na
ubadilishanaji wa sauti katika akili na ubongo wa binadamu.
Tofauti kati ya fonolojia asilia na ile ya Chomsky na Halle (Fonolojia zalishi)
Kutokana na matatizo yaliyojitokeza katika Kiunzi Rasmi cha Fonolojia Zalishi (KRFZ), kuhusu
udhahania na urasmi kanuni wa uwakilishi wa vipengele vya kifonolojia, Davd Stampe na
Donegan Patricia waliibua nadharia ya fonolojia asilia (natural phonology) inayotofautiana na
nadharia ya fonolojia zalishi katika vipengele mbalimbali kama inaelezwa na Massamba(2011)
katika kazi yake ya Maendeleo Katika Nadharia ya Fonolojia.
Fonolojia zalishi hujikita katika kuelezea umbo la ndani na la nje ilhali fonolojia
asilia huelezea umbo la ndani tu. Fonolojia zalishi imejikita katika kuchunguza pamoja na
kuonesha uhusiano uliopo baina ya umbo la nje na umbo la ndani. Katika kuelezea hayo, waasisi
wa fonolojia zalishi walibuni mbinu mbalimbali au sheria na kanuni za ukokotoaji wa umbo la
nje kutokana na umbo la ndani, kwa mujibu wa TUKI (1990) wakinukuliwa na Matinde,
(2012:226) wanasema “Umbo la ndani katika taaluma ya sarufi geuzamaumbo zalishi ni
mshikamano dhahania wa vipashio vya tungo ambao ndio msingi wa tafsiri maana kamili ya
sentensi. Wanaendelea kusema umbo hili hujitokeza katika sentensi kabla sentensi haijafanyiwa
mageuzi yoyote. Pia Matinde, (2012:226) anasema “umbo la nje hutokea baada umbo la ndani
kufanyiwa marekebisho au mageuzi muhimu hadi kufikia kiwango cha usemaji sahihi na
unaokubalika.” Umbo hili kwa mujibu wa Matinde hudhihirika kimatamshi na kiothografia
(kimaandishi). Kinyume na ilivyo katika fonolojia asilia ambayo hujikita zaidi kuelezea umbo la
ndani tu. Kwa mfano katika katika badiliko la vokali kuwa nusu vokali.
[u]----- [w]/--- [v] (isiyo [u])
Ikiwa na maana kuwa [u] hubadilika kuwa nusu irabu [w] katika mazingira ya kutanguliwa na na
irabu isiyo [u] yenyewe, katika maneno haya:
Umbo la ndani Umbo la nje
Muana Mwana
{Mu+a+na}
Mualimu {Mu+alimu} Mwalimu
Muema {Mu+ema} Mwema
Hivyo umbo la nje hutokea baada ya mchakato wa ukokotozi katika umbo la ndani na kupelekea
kuzaliwa kwa umbo hilo.
Waasisi wa fonolojia zalishi wanaaminin kwamba mabadiliko ya kifonetiki ni suala
la kujifunza ilhali waasisi wa fonolojia asilia wao huamini mabadiliko hayo si ya kujifunza.
Katika fonolojia zalishi, Chomky na Halle wanaamini kwamba mabadiliko ya kifonetiki ni suala
la kijifunza. Hii ina maana kwamba mabadiliko ambayo yanatokea katika sauti mbalimbali za
binadamu, mtu hujifunza ili kuyaelewa mabadiliko hayo mfano wa mabadiliko ni kama vile
ukaakaishaji, tangamano la irabu, mvutano wa irabu, kudhoofika na kuimarika kwa fonimu na
mengnine lakini katika fonolojia asilia Stampe na Donegan waanaamini kwamba mabadiliko
hayo mtu hajifunzi bali ni mwitikio asilia wa nguvu za kifonetiki za kutoa na kuingiza ambazo
zimo katika uwezo alionao binadamu katika kuelewa usemaji.
Katika fonolojia zalishi mtoto ana sheria nyingi kuliko mtu mzima lakini katika
fonolojia asilia hizi si sheria bali ni michakato asilia ambayo inachombezwa na uthibiti
anaozaliwa nao mtoto uliomo katika umbo la kifonetiki. Katika fonolojia zalishi hii inatokana
na kwamba mtoto anapozungumza na mtu mzima hutumia umbo la ndani ambalo kwa wana
fonolojia zalishi ili kupata umbo la nje lazima kuwe na sheria maalumu ya kupata umbo la nje na
hapo ndipo mtoto huzalisha sheria nyingi zaidi. Kwa mfano, katika badiliko hili la kudhoofika
kwa fonimu
[d] ---- [z]/---- [i]
Ikiwa na maana kuwa sauti [d] hubadilika kuwa sauti [z] katika mazingira ya kutanguliwa na
vokali [i] katika neno haya:
Umbo ndani Fonimu dhoofika Umbo la nje
Mpendi [d--- z] Mpenzi
Mlindi [d--- z] Mlinzi Mpandi [d--- z] Mpanzi
Lakini kwa upande wa fonolojia asilia wao kwao hizo si sheria bali ni michakato asilia ambayo
inachombezwa na uthibiti anaozaliwa nao mtoto uliomo katika umbo la kifonetiki.
Lengo la fonolojia zalishi ni kuchunguza umilisi wa lugha halisi lakini fonolojia
asilia inaamini kuwa hiyo siyo lugha halisi kwani kwa kufanya hivyo unaichunguza lugha
hiyo kimajumui. Chomsky na Halle wanaamini kwamba lengo la mwanaisimu ni kuchunguza
umilisi wa lugha alionao binadamu kama lugha yake halisi. Mtu anapokuwa na umilisi wa lugha
atakuwa anatumia sauti ambazo zinakubalika katika lugha yake na hiyo ndiyo lugha halisi kwake
lakini wanafonolojia asilia wanasema unapochunguza lugha katika umilisi utakuwa unachunguza
lugha hiyo kimajumui katika masuala ya kifonetiki kwa hiyo mwelekeo wa mawazo yao ni kuwa
hiyo si lugha halisi. Ingawa Stampe na Donegan hawajatuonesha kuwa lugha halisi ni ipi lakini
mawazo yao yanaelekea katika mtazamo kwamba lugha halisi ni lugha ambayo hutumiwa na
mtoto kabla hata kupata umilisi wa lugha hiyo anayoitumia.
Fonolojia zalishi iliegemea zaidi katika urasimi wa mashartizuizi ilhali fonolojia
asilia haina mashartizuizi ambayo ni rasmi kwani yenyewe si nadharia ya kikaida.
Fonolojia zalishi inafuata taratibu, kanuni na sheria mbalimbali katika kuunda na kuzalisha
maneno mbalimbali ambayo ni lazima kuwepo na sheria rasmi zinazokokotoa umbo la ndani
kwenda umbo la nje. Kwa mfano, katika badiliko la mvutano wa irabu wumbo la ndani la neno
Juu mbele |i| + chini kati |a|------ mbele kati |e|
Ikiwa na maana kuwa irabu ya mbele juu |i| huvutana na irabu ya chini kati |a| na kuunda irabu
mbele chini |e| katika maneno haya:
Umbo la ndani Umbo la n je
Maino (ma+ino) Meno
Waizi (wa+izi) Wezi
Waingi (wa+ingi) Wengi
Maiko (ma+iko) Meko
katika lugha ya Kiswahili badiliko hili limetokana a na sheria na si kinasibu tu. Katika badiliko
hili, irabu ya juu mbele |i| huvutana na irabu ya chini kati |a| na kuunda irabu ya mbele kati |e|.
kwa upande wa nadharia ya fonolojia asilia si ya kikaida kwa sababu imekusudia kuifafanua
mada yake yenyewe na kwa kufanya hivyo inaonesha kwamba nadharia hii inaonesha hali haisi
jinsi maumbo ya maneno yalivyo.
Katika fonolojia zalishi fonimu ya mtoto hukua hatua kwa hatua kadri anavyozidi
kutambua ukinzani wa sauti ilhali katika fonolojia asilia huwa kuna usawazishaji wa
fonimu hizo. Kwa mfano, katika fonolojia zalishi mtu ambaye hajabalehe katika lugha hutamka
fonimu ambazo hazijakomaa kama vile:
(i) Ugali vamvu badala ya ugali kisamvu
(ii) Mama omba mma kunya badala ya mama naomba maji ya kunywa.
(iii) Nataka jojoa badala ya nataka kukojoa
Mtoto hutumia sauti hizo kwasababu bado hajatambua matumizi sahihi.Lakini kwa upande wa fonolojia asilia kuna ukinzani wa sauti hizo lakini kadrianavyozidi kuwa mkubwa anaanza kuthibiti ukinzani huo kwa kuanza kutumia sautizinazoelekea kuwa sahihi hadi kuthibiti ukinzani huo vizuri. Kwa upande wa fonolojia asiliafonimu hizo hazikui hatua kwa hatua bali nai usawazishaji wa matamshi ambao unakaribaina nawa mtu mzima, sauti hizo husawazishwa kulingana na zile za watu wazima hadi zile tofauti zakimatamshi zitakapopotea kulingana na fonimu ya mtu mzima.
Hivyo basi, mapinduzi yaliyoletwa na Chomky na Halle katika uwanja wa fonolojia
yalikuwa ni makubwa sana lakini wanazuoni wa fonolojia waliibuka na kuona kuwa mabadiliko
hayo yamekuwa na matatizo mawili, kwanza udhahania, pili urasimi kanuni katika uwakishaji
wa vipengele vya kifonolojia. Madai hayo yalipelekea kuibuka kwa mikabala mingine ya
kinadharia kuelezea jinsi ya kuondokana na matatizo hayo na baadhi ya mikabala hiyo
ilionekana kupinga kabisa na mingine kuboresha kiunzi rasmi cha fonolojia zalishi. Mojawapo
ya mkabala wa kinadharia ulioiburiwa ni fonolojia asilia ambayo inachunguza sulubu za sauti za
binadamu zinazojikita katika usemaji na masikizi, kwa kuangalia zaidi umbo la ndani ambalo
hubadilika kuwa umbo la nje. Pia ieleweke kwamba Chomky na Halle hawakubuni uhusianao wa
umbo la ndani na umbo la nje bali wao walikuja kuelezea sheria na michakato inayofanyika
katika kuunda umbo la nje ambalo kwa kiasi kikubwa huaksi umbo la ndani. Sheria walizozibuni
kuelezea fonolojia majumui ni pamoja na michakato ya kiusilimisho (assimilatory processes) na
michakato isousilimisho (non-assimilatory processes).
MAREJELEO
Massamba, D.P.B. (2011). Maendeleo Katika Nadharia ya Fonolojia. Taasisi ya Taaluma za
Kiswahili chuo Kikuu cha Dar es salaam. Dar es salaam: TUKI.
Massamba, D.P.B. (2004). Fonolojia ya Kiswahili Sanifu (FOKISA), Sekondari na Vyuo.
Dar es salaam. TUKI
Matinde, R.S. (2012) Dafina ya lugha, Isimu na Nadharia Sekondari Vyuo vya kati na vyuo
Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publisher (T) Ltd.
PONGEZI
Kwa Enlightenment group
SAUT-Mwanza.
(2013/2016)