Utangulizi
Kisa hiki cha BABA MKATILI: NDOTO YA KATUNGU; ni kisa kinachojaribu kueleza ndoto ya kijana mmoja aliyekuwa na nia ya kuwa kiongozi wa Familia yao tangu akiwa bado mdogo. Kijana huyu alijikuta akiwa na mawazo hayo kutokana na ukweli kuwa Familia yao ilikuwa ikiandamwa na ukuandamizaji, pamoja na dhuluma zilizokuwa zikifanywa na makundi fulani dhidi ya Wanafamilia yao. Uonevu na dhuluma hizo zilikita mizizi yao katika Famila hii kwa sababu Wanafamilia walikubali kuwa na uhusiano na Wajanja. Uhusiano huu haukuwa mzuri maana Wajanja walilenga kuitawala Familia hii kwa kuwafanya tegemezi na pia kuwafanya wsipende vitu vyao( wanafamilia) na badala yake wapende vitu vya Wajanja hao tu. Katika kisa hiki tunamuona Katungu akifanya jitihada nyingi za kuikomboa Familia hii kutoka katika mikono ya Wajanja na hata Wanafamilia waliokuwa wakiwadhulumu wenzao kwa kutumia madaraka yao... Ungana nami katika kisa hiki ili uweze kupata na kuelewa ni nini hasa kilichozungumziawa katika kitabu hiki... ila nikuombe ufungue jicho la tatu katika ufasiri wa kila neno katika kisa hiki ili uweze kuipata maana kama ilivyokusudiwa vuinginevyo utatoka kapa.
Asanteni sana; ungana nami ili kukuza fikra katika kufikiri na kutambua mambo.
MUNGU AKUBARIKINI NA AKUZIDISHIENI HEKIMA NA MAARIFA.
Na Alpha H. Mayengo
dibaji...,..,
shukrani.
Shukrani ziende kwa wadau wote wa kiswahili; waalimu wangu; na wenye kupigania ukuaji wa kiswahili adhimu ikiwa ni pamoja na wazalendo wa lugha hii.
Mbali na hayo naomba kuwashukru wale wote waliochangia mawazo yao katika uandishi wa kisa hiki.
Kwanza kabisa nimshukuru baba yangu ambaye kila siku alinihimiza kuituliza akili yangu mara niamuapo kuandika makala kama hii. Nashukuru kwa mchango wako sambamba na mama yangu namshukuru pia.
Lakini pia; nawashukuru kikundi changu cha majadiliano katika ndaki ya Mtakatifu Agustino yaani Enlightenment 2013/2016; na wanakiswahili wote.
Napenda kumshukuru Sasha aka mama askofu kwa ukaribu wake na hata kufanya mapitio ya mwisho yaliyowezesha kupatikana kwa kazi nzuri ninayoileta kwenu leo.
Mbali na wote napenda kuwashukuru marafiki zangu walionishika mkono katika kufanikisha zoezi hili; kama vile, Rasta aka Ze Don, Six, Alex, brian tracy, na wengine wote nisiowataja ila milishiriki kwa kiasi fulani katika kunipa mawazo na moyo wa kuishughulikia kazi hii. Mungu awabariki na kuwazidishia.
Asanteni sana.
BABA MKATILI:NDOTO YA KATUNGU
sehemu ya kwanza
UCHAGUZI: BABA WA FAMILIA
Akiwa
katika mavazi ya kupendeza meupe na wanafamilia wengine wakiwa wamevalia mavazi meusi; Katungu alijiona mwenye simanzi kubwa
huku akiwa amezungukwa na ndugu ; jamaa na marafiki katika makaburi
ya familia yao, wakimpumzisha Baba yao mpendwa katika nyumba ya
milele. Katungu alikuwa ni mtoto wa tano kati ya watoto saba wa Mzee
Ipoto; alipata kuliona jua mnamo miaka mingi iliyopita katika familia ya Kilimatinde iliyokuwa ni muunganiko wa koo kubwa mbili yaani ukoo wa kilima cha majini na ule ukoo wa tinde pa kavu maji... Koo hizi ziliungana kutokana na sababu mbalimbali ila ya msingi ilikuwa kuimarisha ulinzi na ukaribu wao...Kijana Katungu alipata elimu yake ya msingi na hatimaye kuhitimu elimu ya juu katika chuo kikuu maarufu cha Wajanja nchini mwao. Mbali na elimu hiyo; Katungu alijikita zaidi katika elimu ya kwao, kwani mara nyingi alisikika akiulaumu mfumo wa elimu ambao ulishabikiwa na Wajanja kwa madai kuwa ulikuwa ukimkandamiza Wanafamilia kwa kuuinua maslahi ya Wajanja... Aliamini kuwa Wajanja hutumia elimu hiyo ili kuwatawala Wanafamilia kwa lengo la kuwanyonya ili kuinua uchumi wa wa familia zao.
Kutokana na dhana hiyo iliyokuwa ikikua akilini mwa Katungu tangu akiwa bado mdogo ilimpelekea kuchukia kila kitu kilichokuwa kikifanywa na Wajanja hawa hasa vile ambavyo aliviona vinapelekea kuibua unyonyaji na wizi wa mali na haki zao.Mzee Ipoto (Baba wa Familia), alijaaliwa kupata watoto saba ambao kati yao kuna watoto wawili wa kike na watoto watano wa kiume. Mzee huyu aliazimia kuwapatia wanawe wote elimu faafu kwa wakati wao; kitu kilichopelekea kuibuka kwa Katungu ambaye alikuja na ndoto ambayo ilimtesa tangu akiwa mdogo kwa lengo la kuondoa ukandamizaji wa Wajanja na pia kuikata mizizi iliyokuwa ikipandikizwa na Wajanja hao, kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanainyonya familia na wataendelea kuinyonya hata kama itaelimika kwa kiasi gani... Lakini pia alilenga kuwa na familia lenye usawa na haki ili kila mtu afurahie maisha ya hapa duniani. Akiwa bado mdogo; Katungu alilelewa katika mazingira ya kuishi karibu sana na Wajanja; kwani, babaye alikuwa akifanya kazi kwa niaba ya Wajanja, kitu ambacho kilimpelekea Katungu kujifunza sana dini ya Wajanja kabla hajapata misingi yake binafsi ya imani ambayo hadi leo ndiyo imuongozayo. Akiwa skuli Katungu anakutana na watu mbalimbali ambao walimsaidia kutambua uwepo wa matabaka ambayo hakuyaona pindi alipokuwa mdogo akisoma katika shule hizo za Wajanja kwani wote walisaidiwa sare za shule na madaftari kitu kilichomwaminisha Katungu kuwa watu wote wana maisha sawa. Lakini pia mambo yanakuja kubadilika zaidi pale alipoanza kusoma historia hasa ya Familia yake ambayo imegubikwa na simanzi na mateso ambayo waliyapata babu zake na hata unyang'anyi pamoja na dhuluma iliyofanywa na Wajanja dhidi ya haki zao.
Kila siku aliumia sana kuona waomba msaada kwa Wajanja ambao waliendesha biashara haramu na isiyo usawa, kwa kubadilisha vitu vya thamani kubwa kwa vitu viso-thamani. Ni wazi kuwa familia yao ilikuwa gizani... tena giza totoro...lakini sasa kwani mwanga haupo? Mbona bado wahangaika kuomba msaada kwa wale wale waliowafikisha hapa walipo? Haya ndo maswali yaliyopelekea kukua kwa ukatili uliyopata kukaa kwa miaka mingi sana hadi pale Katungu alipokuwa baba wa familia yao, ili kuitimiza ndoto yake ya kuiongoza familia hiyo kusikojulikana.
Ilikuwa ni kazi ngumu kuwashawishi wazee ili waweze kulikubali jina la Katungu kuwa miongoni mwa wanaume watakopigiwa upatu kuchukua mke na hivyo kuwa baba wa familia ile yenye utajiri wa kila aina ambao iliachwa baada ya kifo cha babaake.. Baada ya kampeni na uchaguzi mzee ; Katungu aliibuka mshindi na kuwa baba mteule wa familia, na hivyo kuapishwa baadaye ili kushikilia wadhifa alioulilia kwa muda sana akiwa na lengo la kuitimiza ndoto yake iliyoutesa moyo wake. Katungu aliwashangaza wengi kwa mawazo yake kwani alivunjavunja mfumo uliokuwepo na kuanzisha mfumo mpya tena ambao haukuwahi kutokea katika familia yoyote duniani...
Alianza kwa kuvunja baraza la wanafamilia wote, waliokuwepo madarakani katika uongozi wa baba yake; kwa kua aliamini walishindwa kufanya lolote ndio maana akaamua kulivunja na kuteuwa baraza jipya ambalo lilikua na idadi ndogo ya wateule tofauti na ilivyotangulia kabla yake...katika maelezo yake siku aliyokua akilitambulisha rasmi baraza hilo; alijinadi kuwa ameamua kupunguza idadi hiyo ili kupunguza lundo la viongozi ambao wanajazana kufanya kazi chache ilhali wanakula maslahi mazito....katika ufafanuzi wake alidai kuwawajibisha viongozi wateule endapo watarithi matendo ya viongozi waliotangulia... mbali ya hayo alivunja vikao vya wanafamilia na kuwaomba wote waliochaguliwa kufanya kazi ya kujitolea yaani bila malipo... kwani yeye aliamini mtu yoyote anayetaka kuwatumikia watu ni sharti ajitoe kwa moyo wote... pia alivunja kabati lililopokewa na baba yake kutoka kwa Wajanja; pindi alipokuwa madarakani kwa kuzingatia maendeleo ya umma na wanafamilia...na kuwaasa wanafamilia kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kufikia malengo ambayo kila siku viongozi huhubiri habari hizo hizo bila mafanikio... Katika hotuba yake alikuwa na haya ya kuongea kama alivyonukuliwa na wanahabari wa nchi ya kilimatinde waliokuwa na uchu wa maendeleo ya familia yao;
"Nimeamua kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa familia kwanza ili kuhakikisha kuwa tuna uongozi bora kwanza, ndipo tuangalie mambo yanayo
isumbua familia hii;... Naapa kuweka sera mpya kabisa ambazo hata nikifa leo zitalisaidia familia yetu na hivyo kuifanya familia yetu kuwa miongoni mwa zile chache zenye maendeleo na kwazo(sera) zitaweza kulisukuma gurudumu la maendeleo hapa Kilimatinde. Ni lazima tuwaheshimu Wanafamilia wetu na pia kuwathamini kuliko hata tunavyojithamini.. wanangu hoye!"
"hoyeeeeeee.... sema baba we ndo tuliyekusubiri...."
"hakutakuwa na misafara ya viongozi zaidi ya watatu tena hakutakuwa na matumizi ya misafara ya magari kunzia leo... hata mimi nitatumia usafiri usio na msafara ili kupunguza matumizi yasiyo na lazima ya mafuta na fedha pia...hebu fikirieni muda ambao twaupotezaga kusubiri msafara wa viongozi kupita... ni maaskari wangapi huacha kazi na kusimama barabarani wakiozuia magari kutembea hata zaidi ya saa wakati mwingine... Hebu nikuulizeni nyie familia ya Usobadiliko; je, kama kuna wagonjwa wangapi kwenye magari ya abiria na binafsi; ambao, msafara huo utasababisha kuwachelewesha katika matibabuau hata vifo vyao? au je kama mtu anaelekea sehemu na muda umembana afanyaje? kama anawahi eapoti au stendini na akachelewa usafiri hasara itakuwa ya nani? lakini pia mambo ya upendeleo na msamaha wa kulipa kodi uishie sasa maana masikini ndio hawasamehewi ilhali viongozi na matajiri ndio huneemeka, ...Wanangu najua mmechoka kuteseka katika nchi na ardhi hii yenye vyanzo na utajiri mkubwa; hebu fikirini familia yetu lina mali kiasi gani; kuna madini ya kutosha; ardhi nzuri; maji; na vyanzo vingine vingi tu vya kuliwezesha familia yetu kuondokana na umasikini unaowafedhehesha wanangu watuwekao madarakani wakati viongozi wa familia wanufaika na ubinafsi wao... uongozi wangu hautaruhusu wanangu kupata shida tena kutokana na unyonyaji wa viongozi wa familia; pamoja na, hao waendelezao unyonyaji huo kwa kuwapa nguvu wanyonyaji katika familia yetu, tena kwa manufaa ya Wajanja...naagiza kuwa kila mtu afanye kazi na kuijali familia yetu ili tuachane na utegemezi uliokuwa umetengenezwa na Wajanja na kupokewa na viongozi wa familia yetu ambao walivaa vazi moja lisilotufaa tulio wengi...wanangu hoyeeee.."
"ooooooyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee! uishi milele baba...!
Ilisikika burudani ya muziki mzuri kutoka kusikojulikana ukiwa na maneno mazuri kwa wanyonge na machungu kwa wale waliokumbatia ubinafsi na uzinzi uliokuwa unapingwa vikali na Baba Mteule.
wimbo kwa mbali ukisikika
familia yetu ni ya amani,
wanafamilia mwagombania nini,
mlishawahi jiuliza kwa nini,
eti familia yetu iko juu kiumasikini,
kama hujawahi jaribu tazama vitabuni,
kaa tafakari elewa nasema nini,
tulikuwa sawa ila mi najua kwa nini,
tazama nguo za njano, bluu na kijani,
alafu kaa ujue kabati nilimaanisha nini,
ni maadui wadogo waliotushika akilini,
tamaduni ikatupwa wakidai ilikuwa duni,
sala zetu tulipiga popote hata mibuyuni,
wanafamilia pagawa na neoutamaduni,
ikawa new era with mpya imani,
wote wenye ubunifu hatia ikaja mikononi,
na mwanzo wa utegemezi toka ujanjani,
wakaitwa manyani, ukweli umewekwa moyoni
Kwa kweli baba mteule alizungumzia mengi ambayo yalionesha matumaini kwa wanafamilia hasa wale waliokuwa wakinyanyasika na mfumo mbovu wa baba aliyengulia kwa kuwakumbatia wenye nacho na kuwatupilia mbali wahitaji ambao kila siku walijikuta wakiilaani familia yao kwa kutowajali ila kuwaongezea matatizo katika huduma za kijamii na hata unyonywaji uliokithiri... Hivyo wanafamilia hii kubwa walipata tumaini jipya na kusubiri kwa hamu utekelezaji wake bila kujali ingekuwa na madhara gani...
sehemu ya pili
MWAKA WA KWANZA
Suala la kodi ndilo lililokuwa la kwanza kuanza kushughulikiwa kwani; Katungu, aliagiza kuondolewa kwa misamaha yote ya kodi kwa kila mtu haijalishi mtu huyo ni nani na ana wadhifa gani... alieleza kuwa hata yeye atakuwa analipa kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT kwa vitu vyote visivyokuwa na umuhimu kwa maisha ya mwanadamu ila aliondoa kodi kwa vitu muhimu kwa matumizi ya kila siku kama vile; huduma muhimu yaani chakula; mavazi; na malazi binafsi...pia aliongeza kodi kwa vitu vinavyotoka kwa Wajanja ili kupunguza uingizwaji wa vitu vyao na kuongeza uzalishaji wa ndani kwani uzalishaji wa ndani ulipewa msamaha wa kodi na kuungwa mkono kwa kuwapa wazalishaji mikopo ili kuzalisha zaidi na kuinua kipato cha wanafamilia kwa kuzalisha wenyewe... Baada ya malalamiko kuhusu kuongezwa kwa kodi ya vitu vya kigeni kutoka kwa wanafamilia; Katungu alikemea vikali na kuweka sheria ya kukamata wale wote watakaonekana wakivitukuza vitu vya Wajanja na kufungwa ili kuwa mfano kwa wengine.....Kwa nini kodi ilitiliwa kipa-umbele ? haya ndio yalikuwa maswali makuu ya wanafamilia kwani waliamini kuwa baba wa familia angeruhusu watu wasilipe kodi; lakini, walishangaa na kuanza kumchukia baba yao huyo ambaye mwanzo waliyakubali sana mawazo yake yalojaa busara na hekima...Kumbe alilamua hivyo ili kuinua kipato cha Wanafamilia kwa kuzikusanya kodi na kuzirudisha kwao kwa njia ya mikopo ambayo haikuwa na riba yoyote. Kupitia mikopo hiyo Wanafamilia waliweza kujiwekezea wenyewe katika shughuli mbalimbali ambazo ziliwaondolea utegemezi na kuifanya Familia yao kuwa na maendeleo endelevu.
Pia alivunja vikao vya viongozi wa Wanafamilia na kuwataka wateule wote wafanye kazi ya kujitolea na kuhudhuria kikao cha wanafamilia kwa wiki moja tu kila mwisho wa mwaka ili kufikisha matatizo ya Wanafamilia na njia za kuyatatua matatizo hayo... Mzee Chakubunya alikuja juu kwani hakutaka kuachia uongozi na kumtaka Baba Mteule kueleza sababu za kuondosha kikombe chao kilichowapatia kula ya kila siku. Baba Mteule hakusita kueleza sababu ya kuvunja au kuzuia vikao hivyo, kuwa ilikuwa na nia moja tu ya kuzielekeza fedha za posho na mambo mengine ya vikao hivyo katika maendeleo kwani aliamini fedha hizo zaweza kuinua gurudumu la maendeleo ya wanafamilia wa Kilimatinde....Kabla ya kuteuliwa kuwa baba wa familia; Katungu alikuwa na ndoto ya kusimamisha vikao vyote vya familia...kwani, alitambua kiasi cha fedha kilichokuwa kikitumika katika kufanikisha vikao hivyo kuwa ni kubwa. Lakini pia, aliamini vikao hivyo vilichochea chuki baina ya viongozi ambao walikuwa na mitazamo tofauti katika utendaji wa kazi. Hii ilikuwa inajidhihirisha pale zilipokuwa zikitokea pande mbili yaani upande mmoja uliegemea katika kuonesha uovu wa upande mwingine hadi kufikia kugombana kwa viongozi hao hali Wanafamilia wengine wakiwa wanafuatilia vikao hivyo na kuendelezwa kwa ushabiki wa makundi hadi kwa Wanafamilia ambao walikuwa wanafuata upande mmoja au mwingine. Kutokana na sababu hiyo ; Baba Mteule, aliamua hivyo ili kuondoa malumbano yaso msingi na kuwataka viongozi wote wafanye kazi ya kuendeleza majimbo yao na kuandaa ripoti ambayo wataituma kwa tume maalumu ya watu wachache ambao wataipitia na kuyafanyia kazi mapendekezo yote kwa nia ya kuiendeleza familia hii. Alinukuliwa akidai kuwa, "Nilipatwa na uchungu sana kuona watu wakigombana katika kikao cha viongozi wa familia; tena hata bila kujali kuwa wanagombana mbele ya Wanafamilia ambao waliwaamini na kuwapa dhamana ya kuwawakilishia mawazo yao, lakini cha kushangaza viongozi hawa wa familia wanagombana na kurushiana vijembe kila siku badala ya kuziacha tofauti zao na kuzungumzia masuluhisho ya matatizo?... Sasa suala la kujiuliza ni kwamba, hivi wanagombana kwa maslahi gani na ya nani? Na je Wanafamilia ndio huwatuma wakagombane na kutoelewana kila siku ilhali wanakula posho ambayo ni jasho la Wanafamilia?
Aliwastaafisha viongozi wote waliokuwepo na kulipa jeshi la familia suala zima la kuongoza kila sehemu; kwa kuwapanga viongozi wa jeshi kushika hatamu ya uongozi huku akiwataka kushirikiana na viongozi waliotolewa madarakani... kwa kufanya hivyo familia nzima ilijikuta ikiongozwa na Wanajeshi ambao walikuwa wakifuata maagizo ya amiri jeshi mkuu(baba wa familia). Kutokana na dhana ya amri tu, iliyoko jeshini; hakuna kitu alichoagiza amiri jeshi mkuu na kusuasua katika utekelezwaji wake...Wanajeshi waliongoza kwa kila amri iliyokuwa ikitolewa na Mh. Baba wa Familia...Wakati Baba Mteule anatangaza kuwa viongozi wote wameondolewa madarakani; Wanafamilia walishangaa sana na kuanza kuhisi kuwa anajivika madaraka yote ili awatese Wanafamilia bila kuwepo kwa mtetezi... Yaliongewa mengi sana ambayo kwa hakika yalikuwa yanaingia akilini kwa kila Mwanafamilia na wote walianza kumpinga kitu kilichopelekea kwa Baba Mteule kufanya kazi kwa upingamizi mkubwa sana kutoka kwa Wanafamilia, waliorubuniwa na viongozi wastaafu ambao kila siku walimtupia lawama kwa uongozi wa mabavu tena unaowanyanyasa Wanafamilia kwa kuwalipisha kodi; kuwafanyisha kazi za kilimo na hata kuzuia vitu vizuri vilivyokuwa vikiletwa na Wajanja... Hakuna aliyekuwa na hamu na uongozi huu ambao ulijikita katika uzalishaji na uzalendo; ambao, ulitakiwa kuenziwa na kila mtu bila kujali chochote kiletwacho na Wajanja. Chuki hizi za Wanafamilia zilitiwa mori na wale viongozi wa familia ambao walitolewa katika uongozi wao; kwani, waliona kana kwamba wamenyang'anywa uongozi ambao uliwapa nafasi kubwa ya kuwatawala Wanafamilia wenzao kwa kuwanyonya kile kidogo walichokipata baada ya kuwa tayari Wajanja wameshafanya yao. Kutokana na kupoteza chanzo chao hicho cha kujipatia kipato; viongozi hawa, waliamua kuanzisha vuguvugu la kumpinga Baba Mteule ili aondoke madarakani na kuzirejesha nafasi zao za dhuluma kwa Wanafamilia...Iginorante alisikika siku moja akidai kuwa hakufikiria kama ingetokea kiongozi kama huyu ambaye amejikita katika kuwatesa na kuzuia kila kitu kinacholetwa na Wajanja ilhali hatuna uwezo wa kuvizalisha vitu vyenye ubora, na pia kwa nini amejivika madaraka yote na kutuondoa sisi katika baraza la familia wakati hakuna lililoweza kufanyika bila ya ushauri wetu? Huyu mtoto lazima tumuondoshe katika madaraka kwa sababu anatudharau wakati sisi ndio tuliomweka katika kiti hicho anachokitumia kuiharibu familia hii... lazima afundishwe adabu kuwa kile kiti kina misingi yake ambayo lazima ifuatwe, na kila anayepata bahati ya kukikalia na si kufanya yale anayofikiri yafaa wakati hayako katika lile likitabu analoliita likitabu libovu... Mwisho wa siku walijikuta wakishindwa kumtoa madarakani kwani aliimarisha uhusiano wake na jeshi la familia na kulieleza ndoto zake anazitaka kuzifikia kabla ya kutoka madarakani. Baada ya kuaminiwa na jeshi Baba Mteule aliamua kuwatunza vizuri wanajeshi kwani aliamini kuwa jeshi ndio kila kitu kwa ulinzi wa familia. Kwa kufanya hivyo; aliweza kudhibiti uongozi mbovu uliokuwa ukiwakandamiza Wanafamilia, na pia aliwajengea woga Wanajeshi wa familia; kutokana na jinsi alivyokuwa akiyafanya mambo yake yaliyolenga maendeleo ya familia tu na si vinginevyo. Alitenda mengi sana ambayo yalikuwa ni machukizo kwa wale waliokuwa wameshikilia mfumo wa Wajanja na hata wakaanzisha vuguvugu za hapa na pale ili kumfanya Baba Mteule aonekane si mtu mwema kwa wanafamilia na eti alilenga kuiangamiza kabisa Familia yao iliyokuwa ikiufurahia ushirikiano wao na Wajanja ambao waliwatendea mengi mazuri tangu kuanza kwa ukaribu wao. Haikuwa ngumu kutambua mambo hayo kwani Wanafamilia wote walipata kusimuliwa matendo ya Wajanja, dhidi ya Familia yetu... Chapema alisikika akikosoa mambo mengi ambayo aliyahisi ni kinyume na maadili ya Baba kuiongoza Familia kwa madai kuwa alijipendelea na kuwatesa Wanafamilia kwa mipango ambayo inakiuka uhuru wa Wanafamilia... Lakini pia; hata watoto wa Mzee Ipoto, ambao walikuwa ni kaka na wadogo zake Baba Mteule walijikuta wakimpinga eti kwa madai kuwa anakiuka mwongozo wa kuiongoza Familia yao... walisema kuwa hata baba aliyetangulia hakuwahi kufanya madudu kama yale, na kuongeza kwa kufanya mambo yanayopingana na uongozi wa zamani ni kukosa adabu kama si kutafuta laana isiyoisha....lakini; Akili aliyekuwa mdogo wa mwisho wa Baba Mteule, aliwashangaza wengi, pale aliposimama na kumpongeza Baba Mteule kwa kusema yafuatayo, "Nawaombeni Wanafamila wenzangu tuwe na subira, maana yamesemwa mengi sana kuhusu Baba Mteule... hebu tusubiri tuone ni nini mwisho wa matendo yake haya. Kiukweli mwenzenu naona kuna kitu kikubwa sana kinakuja hasa maendeleo ya Familia yetu... tujiulize ni nani alikuwa na ndoto ama maono kama haya ambayo leo yanaiinua Familia yetu?... Ni Baba yupi ambaye aliamua kuishi maisha yafananayo na yale waiishiyo Wanafamilia?... wapi uliona Baba wa Familia anajihusha kama alivyofanya Baba yetu? mkiisha kutafakari hayo naamini mtaelewa nachoomaanisha... na mwisho niwaombee tushirikiane na kuyafata yale yafanywayo na viongozi wetu ili kufanikisha nia ya Baba yetu mpendwa... alipigiwa kelele na kikundi kidogo kilichokuwa kimeundwa na baadhi ya viongozi wa Familia waliokuwa na nia ya kuchafua kila kifanywacho na Baba na uongozi wake ili kuondoa imani ya Wanafamilia dhidi ya Baba Mteule.
sehemu ya tatu
MWAKA ULIOFUATA
Jambo lililowashangaza wengi katika mwaka huu, ilikuwa ni kuuza mali nyingi za familia kwa wanafamilia binafsi; kwani, baba; chini ya uangalizi wa jeshi lake aliloliimarisha vizuri, alitangaza kuuza magari mengi ya familia na mali za familia ikiwa ni pamoja na kupangisha nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na viongozi wa familia; kwani, aliaminini kuwa zilihujumiwa kutoka katika familia, lakini pia aliwanyang'anya Wajanja kila kitu walichokuwa wamejimilikisha na hata kuwekeza akaviuza kwa Wanafamilia na kisha kuwataka wasirejee kufanya chochote katika familia yetu...na fedha zilizopatikana alizielekeza katika kuinua uchumi wa wanafamilia kwa kuongeza kazi kwa vijana; kwani, baadhi ya viwanda vilianzishwa ambavyo viliazimia kuongeza soko la ajira kwa Wanakilimatinde. Katika utekelezaji wa zoezi hili, Katungu aliwaeleza wanafamilia kuwa kwa kawaida si sawa kufikiria kuwa yeye anaelekea kuchanganyikiwa kama wanafamilia wengi wanavyoendelea kumsema nyuma ya pazia. Yeye ameamua kuuza mali za familia kwa wanafamilia ili kuongeza umakini katika kuvitunza vitu hivyo kwa wale watakaovinunua... alidai kuwa mali ambayo si yako yaani ya umma mtu lazima utapunguza kiwango cha uangalizi kwani si chako na ndio maana tunaona vyombo vingi vya familia yetu vyaharibika sana tofauti na vile vya wanafamilia binafsi... hii ni kutokana na uchungu kuwa ukiharibu wewe ndo muhusika wa matengenezo, wakati vya wanafamilia vitasubiri jasho la wanafamilia hata kama hawakuhusika katika huduma yake... kwa kufanya hivi nimeamua kubakiza mali chache tu ambazo zitatumika bila gharama kubwa hivyo kupunguza fedha za matumizi... pia mali zisizohamishika zitabaki ambazo zitakidhi haja ya matumizi tu kulingana na uhitaji wetu... kwa mfano ile nyumba ambayo baba angu alikuwa akipumzika wakati wa baridi, nimeamua kuifanya kiwanda cha ngozi; halikadhalika, pale ufukweli alipokuwa akipumzika mara kwa mara pia nimeanzisha kiwanda cha samaki...ile nyumba ndogo alipokuwa analala mzee akihudhuria kikao cha wanafamilia ndipo yamekuwa makao yangu makuu na hapa pamekuwa sehemu ya wazi ambayo kila mtu anaruhusiwa kuja kusema lolote linalomkwaza tena ongea kwa uhuru hata kunikosoa mimi Baba yenu fanyeni hivyo kwa amri yangu; maana, nataka kujua fikra na matatizo ya kila mtu. Nitawaweka watu hapa ambao watafanya kazi usiku na mchana kuwasikilizeni ili kunifikishia fikra zenu kuhusu maendeleo ya familia yetu ya Kilimatinde. Lakini sio kuja hapa na kuongea mambo yaso- maadili; la hasha, ila kuongea yale yenye tija na yenye kusitri maadili yetu maana tunantaka kuijenga familia mpya yeny maadili; haki na usawa kwa kila Mwanafamili.
Mfumo wa ujifunzaji pia aliubadilisha kwa kurejesha mfumo wa zamani wa kujifunza kwa vitendo tena kwa kutumia muda mfupi katika kujifunza maarifa fulani...alibadili mfumo ulioigwa kutoka katika koo za kigeni na kuanzisha mfumo mpya ambao ni 2:3:3:5. Mfumo huu uliolenga kuzalisha wahitimu ambao wako tayari kuajiriwa au kujiajiri; na, ujuzi ndio kitu pekee kilichopewa kipaumbele kwa wanafunzi na shule zote ambazo ziliwekwa chini ya uongozi wa jeshi. Pia mfumo huu ulisisitiza na kumakinika katika suala zima la uhamishaji wa maadili mema kwa kila mjifunzaji; ili kujenga familia misingi ya maadili mema na hivyo kuwa na wanafamilia waadilifu na wachapakazi. Ili kufanikisha hilo baba wa familia aliamuru kila familia kuwapeleka watoto wao shule kwani elimu ilitolewa bila malipo na ilikuwa ni lazima kwa kila mtu ambaye hakupata elimu...Katika kuhakikisha kuwa elimu inamkomboa kila Mwanafamilia; Baba Mteule, alianzisha mtaala mpya wenye masomo machache na tena aliwaomba walimu wawafundishe watoto kulingana na vitu walivyokuwa na uwezo na tena walivyovipenda. Wale waliokuwa hawapendi ksoma walifundisha kazi mbalimbali za mikono na wengine walipelekwa jeshi ambako walipewa mafunzo na maadili ya kuwa na uzalendo... Uzalendo aliokuwa akiutaka Baba Mteule; ulikuwa ni kupenda maisha ambayo si ya kigeni; kutoutukuza utamaduni wowote wa kigeni ikiwa ni pamoja na kujivuna kuwa ni mwanafamila wa familia ya Kilimatinde. Alihimiza umoja na mshikamano kuwa ndizo ziwe nguzo pekee za uzalendo kwa Wanafamilia wote.
sehemu ya nne
MWAKA WA KILIMO NA UZALENDO
Kuanzishwa kwa shughuli za kilimo ambazo alizianzisha katika sehemu ya kati ya miliki ya Wanakilimatinde; kwa kizingatia tafiti mbalimbali zilizokwisha fanywa na wajanja... alianza na sehemu ya kati kwa sababu, sehemu hizo zilikuwa na ukame wa hali ya juu; hivyo aliamuru uchimbaji wa visima vya kudumu ili kufasnikisha zoezi la umwagiliaji... kwa kufanya hivyo alijikuta akifanikisha mpango huu kwa kutumia bajeti ya vikao vya viongozi wa wanafamilia ambayo ingewezesha vikao kwa miaka miwili tu...Baada ya mpango huu wa kwanza kufanikiwa aliongeza juhudi katika kuusimamia mpango huu ili usije ukahujumiwa na Wajanja ambao kila siku walijitahidi kuuangusha... hata hivyo walishindwa kwani uhamiaji uliwekewa mipaka na hata waliojaaliwa kuingia katika ukoo huu wa Kilimatinde; walipewa uangalizi mkubwa ili wasijaribu kuuhujumu mpango huo... Kila kitu kilitakiwa kufanywa na Wanakuilimatinde ili kuongeza ajira na kuondoa utegemezi kutoka kwa wajanja ambao hauna maana kwani hakuna kitu ambacho wanafamilia wasingeweza fanya wenyewe...Kwa hakika kilimo kilifanyika kwa nguvu zote kwani baba alisisitiza wanafamilia wote kuwa na mashamba yao ambayo walitakiwa kuyahudumia kwa siku mbili ndani ya juma; lakini pia, walitakiwa kuhudhuria kwenye mashamba ya umoja wa wanafamilia kwa kwa siku tatu na endapo mtu hakufuata ratiba husika aliadhibiwa vikali na jeshi bila kujali yeye ni nani...Kilmo kilfanikiwa kwani wanafamilia kwa kuogopa jeshi walijikuta wakitimiza ratiba zao kwa ufasaha kwani waliogopa adhabu za za kijeshi...Mwanzo wanafamilia walienda kwa kuogopa kichapo lakini baada ya mwaka mmoja walijikuta wakizoea kazi hizo na hivyo kuzifanya kwa bidii kitu kilichopelekea kuongezeka kwa uzalishaji katika familia ya Kilimatinde na hivyo kuondoa kabisa suala la njaa katika familia yao... Baada ya kuona kuwa sasa wametokomeza njaa katika familia waliamua kulima zaidi kwa ajili ya kuwauzia koo za jirani yao ili kuongeza kipato cha familia kwa kuuza chakula cha ziada...Kutokana na kuzalisha chakula cha ziada Baba wa familia aliamua kuboresha uzalishaji kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa kwa kuiga hatua zilizokuwa zikitumiwa na wajanja katika mashamba yao waliyokuwa wakiwatumikisha wanafamilia kwa ujira mdogo, zamani za zamani kabla ya utawala wa babu mzaa babu wa babu yake...Kwa kutumia mbinu hizo za kisasa familia hii ilijikuta ikifanya mapinduzi halisi ya uzalishaji na kuwa mfano wa kuigwa na koo za karibu yao zilizokuwa zimeanza kuwachukia wajanja waliokuwa wakiwanyonya na wao kama ilivyokuwa kilimatinde kabla hawajapata uongozi wa baba walimwita baba mkatili...Wanafamilia wanaanza kufurahia mavuno yao na hata kuanza kuwauzia majirani zao na kujulikana sana kwa uzalishaji bora na wenye kutunza mazingira. Kumbuka kuwa kilimo katika familia hiki kilihusisha upandaji miti katika maeneo yote yaliyokuwa yakiizunguka familia ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa matunda ambao ulifana kuliko hata kilimo cha nafaka. Na hivyo familia hii ikawa ndio wazalishaji wakuu wa mazao yote ya kilimo hata Wajanja wakaja kuuziwa vitu mbalimbali kutoka katika familia hii ya Baba Mkatili.
Mbali na hayo; baba huyo mteule; aliagiza watu kuachana na utamaduni wa kuiga kutoka koo za kigeni na kuwataka watu wote kuutukuza Ukilimatinde kwa kupenda lugha zao za asili; kupenda kuishi maisha ya babu na baba zao; kuwa wazalendo na pia kuwa na uchungu na familia yao ya Kilimatinde...Baada ya baba wa familia kuona kuwa bado wanafamilia wanaupenda utamaduni wa wajanja ambao walijitahidi kujaza vitu vilivyolenga kutokomeza utamaduni wa wanafamilia; kwani, wajanja walileta vitu ambavyo vilikuwa na matumizi ya lugha zao ili kuipoteza lugha asili ya wanafamilia, ikiwa ni pamoja na kuonesha mambo mbalimbali ambayo yalikashifu utamaduni wa wanafamilia na kuonyesha ubora wa utamaduni wao kwa kuukweza kuliko ule wa wanafamilia...hivyo basi, baba wa familia aliamua kupiga marufuku matumizi ya lugha ya wajanja ikiwa ni pamoja na kuhimiza uhifadhi wa utamaduni wetu kwa kuanza kula vyakula vyenye asili na chimbuko la familia, pia alikataza matumizi ya vitu vilivyokuwa na asili ya wajanja ili kuwafanya wanafamilia wasivione tena vitu vya wajanja na kurithi matumizi ya vitu vyao vilivyotengenezwa na wanafamilia... Iliwekwa sheria ambaayo ingemshughulikia kila mkaidi wa maagizo hayo ya baba chini ya uangalizi wa jeshi..
sehemu ya tano MWAKA MKUU WA MABADILIKO
Likitabu bovu lililoacha na baba yake kama alivyolipokea kutoka kwa babu yake aliyepokezwa na Wajanja tena bila hata kutaka kuliweka sehemu nzuri au kuliandika vizuri tena kwa lugha inayoendana na mabadiliko yaliyopo katika Familia; wateule wote waliotangulia, hawakutaka labda waliona linafaa na kulifanyia marekebisho ilikuwa ni ufujaji tu wa pesa za familia... Lakini bila kulijali likitabu hilo bovu; baba mteule, aliamua kulibadili jalada na kulipa maandishi mapya na kuzibadili kwa kiasi fulani hadithi zilizoandikwa kizamani...Baba huyu Mteule aliazimia likitabu ile lilochukiwa; lisomeke kwa uzuri maana Wanafamilia wa sasa waliokuwa wanashindwa kulisoma likitabu hilo kwa kuwa liliandikwa kwa maandishi ya kizamani, na yaliifaa jamii ya zamani sana ambayo yalikuwa hayaeleweki kwa hawa Wanafamilia wapya waliokuwa wanataka mabadiliko katika familia yao. Hivyo basi; Baba Mteule, aliamua kulitengeneza likitabu hilo bovu ili kuhakikisha kuwa litawafaa Wanafamilia kwa maandishi na hadithi zake ili liweze kusomeka na kueleweka hata kuendana na familia ya sasa, ambayo ilijikuta ikiwa na maswali mengi tena ya msingi kuhusu likitabu hilo bovu ambalo lilishindikana kufanyiwa marekebisho kata uhifadhi wake... Baada ya mwonekano mpya wa likitabu bovu; Wanafamilia wengi ndipo walipoanza kumuelewa Baba Mteule, kwani lile likitabu bovu baada ya kupewa maandishi waliyoweza kuyasoma na kuyaelewa walitambua kuwa lile liktabu bovu liliwafaaa sana.. Ingawa walikuwa wakimshutumu kwa kuwatesa Wanafamilia kwa kuwafanyisha kazi za nguvu tangu aangie madarakani, lakini sasa walianza kutambua nini ilikuwa malengo ya baba yao kwani sasa kila Mwanafamilia alianza kuishi kwa haki, usawa na amani tofauti na walivyotegemea hapo mwanzo kwani walimuona Baba yao kuwa ni mkatili na asiyependa maendeleo hata kidogo... Kutokana na maandishi mapya katika hadithi za lile likitabu libovu, kila Mwanafamilia aliweza kuishi akiwa na imani na Baba yao kwani aliwasaidia sana hata kuweza kuliandika upya lie liktabu bovu ambalo lilikuwa na hadithi nzuri zilizoweza kuwaponya wale waliokuwa na shida mbalimbbali katika familia na hivyo kuongeza afya ya Wanafamilia na hata uwajibikaaji. Wanafamilia walijikuta wakilipenda likitabu libovu; kwani, baada ya kuandikwa katika maandishi ya kisasa waliweza sasa kizielewa hadithi zilizokuwemo katika likitabu lile... Hapo mwanzo likitabu hili bovu lilikuwa na hadithi ambazo ziliandikwa maalumu kwa ajili ya Wanafamilia wa zamani na kwa kweli hadithi zile ziliwafaa wao ingawa zingine hawakuzielewa kabisa. Hadithi zilizoandikwa katika likitabu hili kumbe zilikuwa nzuri sana ila ziliandikwa na Wajanja ili kuwawezesha wao kuwa karibu nao na hata hivyo hadithi hizo zililenga kueleweka na watu wachache tu tena wale waliokuwa wapenzi wa Wajanja yaani wenye tabia za kijanja. Lakini pia; likitabu hili lililenga kutooleweka kwa Wanafamilia wengi ambao hawakuwa na uwezo wa kuzielewa hadithi za likitabu lile bovu lililopendwa na viongozi wengi wa familia ambao walijaribu kulifanya lisomeke na kueleweka kwa unafiki ila walitaraji kutozifunua hadithi za kweli za lile likitabu ambalo familia nyingi duniani huwa na lao lenye hadithi zizifaazo familia zao tu.. Kutokana na mabadiliko hayo kutokea, kulipelekea Wanafamilia wengi kuwa na hamu ya kulisoma likitabu lile na kulitumia katika kuwasaidia Wanafamilia wenzao pale walipokuwa wanatakiwa kujifariji hasa walipokutwa na matatizo ambayo tiba zao zilipatikana katika hadithi zilizoandikwa katika likitabu lile lenye mwonekano mpya. Ama kwa hakika Familia nzima ilijikuta ikilitafuta likitabu hili ili kulitumia katika matatizo yao ambayo hapo awali yalishindikana kutibika kiufasaha ingawa likitabu hilo lilikuwepo ila halikuwa na fariji ziwafaazo Wanafamilia; kitu kilichopelekea likitabu hilo kuonekana halina maana kwa Wanafamilia ila Wajanja na waso-maadili tu... Ilifikia hata Matonya akazipenda hadithi za lile likitabu na akawa akilisoma katika kazi yake ya kuomba omba mtaani ingawa Mkwasi alichukia sana hadithi nyingi za lile likitabu kwani liliwatibia wengi aliokuwa akiwasababishia maradhi ambayo yalihadithiwa katika likitabu lile lenye mwonekano mpya na hadithi nyingi zilizolenga kuwafurahisha Wanafamilia wote na si kikundi fulani cha watu tu
Suala la uzinzi pia lilikemewa vikali na Baba Mteule; kwani aliona Familia na Wanafamilia wote walikuwa wakijihusisha na uzinzi ambao ulileta madhara makubwa sana katika maendeleo ya Familia. Alichukia kuona uzinzi ulikuwa unafanywa na Wanafamilia, ambao walijikuta wakiwa na wapenzi wengi tena wale ambao hawana mapenzi ya dhati kwao na hata kwa Familia. Wanafamilia walijihusisha na mapenzi tena yaso salama kwa kutojali kuwa walikuwa wanasababishiwa kujijengea utegemezi ambao hauwezi isha; kwani, walijijengea tabia ya kuwategemea hao wapenzi wao wa kigeni kwa kila kitu hata kile ambacho wangeweza kukifanya wao wenyewe. Kutokana na dhana hiyo Wanafamilia walijikuta wakiwapenda sana wapenzi wao hao wa kigeni na kupenda kila kilichofanywa na Wageni wapenzi wao hao. Lakini chanzo cha uzinzi wa Familia hii, ulitokana na dhana iliyopandikizwa na mababu wa zamani za zamani; ambao waliwakaribisha Wajanja na kuwafanya kama watu muhimu na mashuhuri ingawa walikuja na ujanja wao wa kutaka kuliacha kabati lao lenye zile nguo ambazo tuliachiwa kwa masharti ya kutozitumia ila kwa usaidizi wao. Uzinzi huu ulijikitia mizizi yake pale, Familia yetu ilipokubali kusaidiwa katika shughuli za kuijenga familia ya Kilimatinde; kitu kilichopelekea kuhamia kwa Wajanja na uharamu wa mabadilishano. Sasa kumbe ; uzinzi huu, ulitokana na tamaa ya zile nguo ambazo tulikuwa nazo ila baada ya kurudisha toka kwa Wajanja zikiwa zimebadilishwa mwonekano ziliwapagawisha Wanafamilia na hivyo kujikuta wakijiingiza katika uzinzi na Wajanja ambao walilenga kuinyonya familia hii ili kuwaachia kabati lile liso-faida kwa Wanafamilia na hivyo kuendelea kuwaelekeza wanafamilia jinsi ya kuzivaa zile nguo zilizowavutia wengi.
Kuvunjwa kwa kabati zuri lililotunzwa vizuri na baba waliomtangulia pia ilikuwa ni kazi kubwa iliyofanywa na Baba mteule; kwani, baada ya mwaka mmoja wa utawala wake, aliamua kuwaita wanafamilia wote na kuwauliza kuhusu kabati alilolikuta ndani kwa baba yake ambalo alikuwa akilisikia tu ila hakuwahi kulitia machoni pake hata siku moja.. Aliwauliza wanafamilia kama baba yao aliwahi kulifungua mbele yao wakajua kilichopo; lakini, aliambiwa kuwa haikuwahi kutokea likafunguliwa hilo kabati kwani lina nguo za wajanja ambazo alipewa kiongozi wa familia tu na ye pekee ndiye aliyekuwa na uwezo wa kuzipokea na si kuzitumia maana ziliwapendeza wajanja tu, pamoja na kuziangalia nguo hizo na kuzitunza pia... Baba mteule aliomba kulifungua kabati hilo mbele ya wanafamilia , lakini alionywa vikali na viongozi wa familia waliokuwa katika utawala wa baba yake kabla ya kifo chake... Kutokana na hali aliyokuwa nayo Baba mteule hakuvitaka tena vitu kutoka kwa wajanja; hivyo, aliamua kulivunja kabati hilo mbele ya wanafamilia na kuwaomba wanafamilia kumuunga mkono wakati wa kuwaeleza wajanja kuwa kabati hilo lilivunjwa na wanafamilia na kuwaambia kuwa nguo zote zilizokuwemo zitatumiwa na wanafamilia ingawa kabati hilo limechomwa moto, na halitakiwi tena na hata kabati litakalofanana na hilo walilolileta halitakuwa na nafasi tena hata kama wajanja wataamua kulitumia tena kabati hilo kwani waliowapa yaani viongozi wa familia waliotangulia walishaondoka; na familia hii chini ya uongozi mpya hawatakuwa na haja na kabati hilo tena. Lakini Baba Mteule pamoja na wanafamilia walistaajabu kukuta nguo zenye uzuri wa ajabu katika kabati hilo. Nguo hizo zilikuwa ni zenye kumsitiri vizuri kabisa mwanafamilia na kuondokana kabisa na taabu alizokuwa akikutana nazokwani zilikuwa zimehifadhiwa katika kabati ambalo lilikuwa linamsaidia Mjanja ambaye alikuwa anataka kupendeza yeye tu na Mwanafamilia kuyavaa mavazi hayo ambayo kwa hakika yangepunguza masononeko ya Wanafamilia ambao walikuwa na uhitaji mkubwa wa kuyatumia mavazi hayo ingawa Wajanja walijitunzia wenyewe katika kabati ambalo walimpatia kiongozi wa familia. Kiukweli nguo zile zingewafaa sana wanafamilia kwani kulikuwa na nguo zenye matumizi faafu kwa wanafamilia; kwa mfano, kulikuwa vna nguo ya manjano ambayo ingewafaa wanafamilia na ndiyo pekee ambayo wangeweza kuitumia katika ujenzi wa famila yao kwani ilikuwa na uwezo mkubwa wa kufanikisha hilo. Lakini pia; kulikuwa na nguo ya kijani ambayo wangeweza kuitumia katika kilimo na hivyo wangeweza kuchukua uwezo kidogo uliokuwepo katika nguo ya manjano na kuutumia katika suala la kilimo na kuiondoa njaa kabisa katika familia yao. Mbali na hizo, kulikuwa na nguo za bluu nyingi ambazo babu wa babu wa Baba Mteule aliwatunzia Wajanja ili wazitumie kwa kuwasifia kuwa ziliwapendeza sana Wajanja hao kuliko Wanafamilia ambao walizitunza tangu enzi za mababu. Nguo hizi ama kwa hakika zilikuwa ni za kupendeza sana kitu ambacho kilipelekea koo nyingi kutoka sehemu mbalimbali kuja kuziona na hata kupumzika karibu ya nguo hizi ili ziwaguse kidogo na mng'ao wao wa ajabu ambao ulivutia wengi na kuwapa hitaji lao muhimu lililolainisha mlo wao; ambalo kwa wingi lilipatikana humo. Kama haitoshi kabati lile liliwekewa pia kitu kilichokuwa cha pekee kabisa ambacho kila mtu aliyesikia habari zake alitamani kufika kuona kitu hicho kilikuwa na upekee gani? Kwa hakika kabati hili lilikuwa na vitu ambavyo vilikuwa ni zawadi ya Wanafamilia lakini Wajanja walijifanya kama walivimiliki na kuvigundua vitu hivyo na ndio maana viongozi tangulizi wa Familia walilazimishwa kuwatunzia na tena hata wao hawakuruhusiwa kuzivaa wala kuvitumia sana ila kwa niaba ya Wajanja pekee.... Kwa ushauri; Baba Mteule; aliwaomba Wajanja watafute sehemu nyingine wanakoweza omba kutunziwa kabati lao ambalo limetupunguzia nafasi ya kulimiliki eneo letu kwani lilichukua nafasi kubwa katika chumba cha Baba wa familia na hivyo kuishi bila amani maana lilikuwepo tu ndani halafu halina faida kwetu.
sehemu ya sita
KUACHIA MADARAKA:BABA MTEULE
Mambo yote hayo yalifanyika ndani ya kipindi cha miaka minne tu, ya uongozi wa Baba Mteule. Baada ya kuona kuwa; mambo yamefikia pale alipopataka, aliamua kuitisha kikao cha wanafamilia ili kuzungumza nao kuhusu mustakabali wa familia yao ambayo sasa ilikuwa inajitegemea yenyewe kwa kila kitu... Alianza kwa kuwapongeza wanafamilia na pi kuwapa pole kwa yale yote waliyokumbana navyo tangu aaingie madarakani... Mara baada ya salamu hizo za pole na pongezi; Baba mteule aliwaambia Wanafamilia kuwa, anarudisha vikao vya viongozi wa familia ili kuendelea na utaratibu uliokuwepo zamani wa vikao vya kila mwaka ikiwa ni pamoja na kumjadili kwa yale aliyoweza kuyafanya kinyume na kama kumwajibisha itabidi wafanye hivyo; wakati, yeye akiachia uongozi wa familia hadi hapo watakapomaliza kumjadili na kutoa maamuzi yake kuhusu utendaji wake katika baraza la familia ambalo lilizuiwa kukutana kwa takribani miaka mitatu na huu ni wa nne... Kila mtu alishangaa kusikia maneno yale yaliyomtoka Baba Mteule; kwani, kila mwanafamilia alikuwa ameona kazi nzuri iliyofanywa na uongozi wake na hakukuwa na yoyote aliyetaka Baba Mteule kuachia uongozi wake wakati bado alikuwa na nguvu na pia ni lazima apatwe na kifo ndipo wachague baba mwingine. Aliwaeleza kuwa ameamua kufanya hivyo, ili kuwapa Wanafamilia nafasi ya kuangalia mapungufu yake na kwa sababu alitumia mabavu ya jeshi katika kuiongoza familia ile; hivyo haikuwa vibaya kama angewaachia utawala wao wa zamani ambao ulikuwa hauna mabavu ya kuongoza bali mabavu ya unyonyaji wa mali na haki za Wanafamilia uliokuwa ukiendelezwa na Wajanja kwa kuwatumia viongozi wa familia hali hawakunufaika kwa lolote ila kuwatesa Wanafamilia wenzao kwa kuhujumu mali na haki hadi za vizazi vijavyo... Baba Mteule alihitimisha kwa kuwataka kuwa makini na Familia; lakini pia, kuzingatia misingi alozijenga hasa katika suala la uongozi na uzalendo ili kuenzi na kuutukuza Ufamilia wao na kuongeza kuwa anawaomba kama wataona hafai tena kuwaongoza, wahakikishe wanajaribu kuleta muungano wa familia yao na koo zingine zenye asili kama yao ili kuimarisha mipaka yote katika uwanja wa koo hizi ambao ulijaliwa zawadi nyingi za asili zenye kuwashangaza wengi ambao kila kukicha wanajaribu kuzifarakanisha koo hizi zenye wanawake wasiopenda rangi zao na kutaka kuipata rangi iso-yao... Pigeni vita ujanja ambao una malengo mabaya kwa vizazi vyetu na urithi wao... nawatakia maamuzi mazuri tena yalo-busara na hekima ili kufika mahali penye usawa na haki sawa kwa kila mwanafamilia.
Mungu wa babu na baba zetu akujalieni heri na baraka na mafanikio kwa kila mfanyalo...
Mara Katungu alizinduka kutoka usingizini na kutambua kuwa alikuwa akiota. Alikaa juu ya kitanda chake na kutafakari kwa kina ni nini ilikuwa maana ya ndoto ile kwani iliigusa sana akili yake. Aliamua kusogea katika meza yake ya kusomea na kuanza kuiandika ndoto ile ili apate kuisimulia kwa wenye hekima na kutaka kujua ni nini maana ya ndoto ile kwani hakuielewa kabisa ilikuwa na maaa gani... Baada ya kuwasimulia wengi alijikua akielewa maana ya ndoto ile kumbe ilikuwa na mafumbo mengi tena yenye kuzungumzia maisha yaliyomuhusu yeye na jamii yake ambayo inakumbwa na mambo yanayoendana na hayo yaliyotukia katika ndoto ile . Aliamua kuiweka ndoto ile katika maandishi akiamini kuwa ipo siku anaweza kuja kuona ndoto ile ikitokea.
MWISHO
nyuma ya kitabu
wasifu
Alpha Hezron Mayengo ni muhitimu katika kitivo cha elimu; akijihusisha na masomo ya historia na kiswahili katika ndaki ya Mtakatifu Agustino-Mwanza Tanzania. Alihitimu elimu yake mwaka 2016, na kuanza kujishughulisha na uandishi wa vitabu kabla ya kujihusisha na kazi nyingine. Ni mmiliki wa blog pia inayojulikana kama alphamayengoh@blogspot.com ambayo imejaza mambo mengi yanayokuza lugha yetu ya Kiswahili.
Katika kijitabu hiki amejaribu kuelezea ndoto ya kijana Katungu aliyoiota kuhusu kifo cha baba yake aliyekuwa kiongozi wa familia yao... Katika ndoto ile; Katungu anajikuta, akishindwa kuelewa ni nini maana ya ile ndoto... ilhali alihisi ilikuwa na maana fulani n uhusiano fulani na jamii yake....
Fuatilia Kisa hiki cha kusisimua cha BABA MKATILI: NDOTO YA KATUNGU.
No comments:
Post a Comment