Monday, August 1, 2016

Chimbuko la Tamthiliya.


Dhana ya Tamthiliya.
Neno tamthiliya limetokana na kitenzi mithilisha kwa maana ya kufananisha au kulinganisha. Katika kiswahili, tamthiliya inatumika kwa maana ya michezo ya kuigiza. Katika tamthiliya huwa kuna ufananishaji ambapo mwigizaji hujifananisha na mhusika wa mchezo wa kuigiza.
Mazrui na Syambo (1992) wanaieleza tamthiliya kuwa ni utungo wa fasihi ambao umebuniwa kwa kiasi kikubwa kwa lugha ya mazungumzo yenye kuzua na kuendeleza matukio ya hadithi ya utungo huo.
TUKI (2004) nao wanafasili tamthiliya kuwa ni utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo.
Kwa ujumla tamthiliya huweza kufasiliwa kama ni utungo wa kisanaa ambao huwasilishwa jukwaani kwa njia ya mazungumzo yanayoambatana na matendo/utendaji ambao husawiri matukio halisi katika jamii husika.
Chimbuko la Tamthiliya.
Kauli inayodai kuwa chimbuko la tamthiliya linahusishwa na tamthiliya kuzingatia sanaa au mwigo tu na kuacha matendo ya dhati si kweli kwani chimbuko la tamthiliya linahusisha pia matendo ya dhati (miviga). Tunaweza kudhihirisha chimbuko la tamthiliya duniani kote kwa kuzingatia mambo matatu ambayo ni; Miviga, Mwigo/umithilishaji pamoja na Sanaa za maonyesho.
Miviga.
Miviga ni dhana inayotumiwa kuelezea sherehe ambazo aghalabu hufanywa katika kipindi maalumu katika jamii fulani. Miviga ilihusiana na vitendo vya dhati kama ibada, matambiko, jando na unyago. Miviga hurejelea mihula miwili muhimu katika kuelzea chimbuko la sanaa za maonyesho – muhula wa mpito (liminal phase) na muhula wa liminoid.
.
Katika liminal phase; mtu wa kale katika juhudi zake za kutawala mazingira yake aligundua kuwa kuna matukio ambayo hakuyafahamu na ambayo yalimpumbaza. Baadhi ya matukio haya ni pamoja na majira, uhai, kifo, na maumbile ya dunia kama vile radi,na mafuriko. Ili kupambana na mambo hayo yaliyokuwa yakimpumbaza, aliomba msaada wa miungu kupitia ibada na kutambika. Matendo ambayo aliyaona yanafaa aliyarudiarudia hadi kuwa matendo ya kuaminika na ya kudumu yaani miviga. Matendo hayo ya dhati yalijitokeza katika sehemu mbalimbali za ulimwengu mfano katika nchi ya Ugiriki-Ulaya magharibi, matendo haya alifanyiwa Dionysus ambaye alikuwa mungu wa mvinyo na neema. Inamaanisha kuwa Dionysus alikuwa mtoto wa Zeus (mungu mkuu) na ambaye aliuawa na kufufuka. Wagiriki walilinganisha hadithi hii ya kufa na kufufuka kwa Dionysus na mzunguko wa majira kama masika ambayo yalileta neema.
Barani Afrika matukio haya yalionekana miongoni mwa makabila fulanifulani, mfano Wakamba nchini Kenya ambapo inaaminika kuwa na matambiko kwa miungu yao tangu jadi na hasa wanapokabiliwa na hali ngumu ya maisha hususani ukame na pia wanapopata neema kama mvua humshukuru mungu wao kupitia matambiko.Mfano mwingine ni kutoka kwa jamii ya Wazinza nchini Tanzania ambapo walikuwa na mungu wao aitwaye Msambwa ambapo walikuwa wakifanya matambiko yaliyoambatana na ngoma inayoitwa mlekule. Kutokana na maendeleo katika jamii mbalimbali duniani, jamii baadhi zilipiga hatua na kuendelea kutoka hatua ya liminal phase hadi muhula wa pili unaoitwa liminoid phase .
Katika kipindi cha liminoid phase; kumekuwa na mgawanyiko maalum wa kazi kama vile wakulima, wafugaji, wafua vyuma, wasanii na maseremala. Kutokana na mgawanyiko huu wa kazi, chakula cha ziada kikazalishwa ambacho kiliruhusu watu wengine kufanya sanaa za maonesho, kitendo ambacho hakizalishi na kukidhi mahitaji yao na kusababisha watu wenye uwezo kuwadhamini wasanii. Sanaa za maonesho zilikuwa hasa na lengo la kuburudisha.Watu wa aina hii (wadhamini) walipotokea walifanya chimbuko la sanaa za maonesho kufikia hatima yake na kuzaliwa kwa sanaa za maonesho yaliyokamilika yaani Tamthiliya. Hivyo tamthiliya inahusisha matendo ya dhati na yasiyo ya dhati na hayawezi kutenganishwa.


Mwigo/umilithishaji wa maisha ya kawaida.
Kwa mujibu wa Aristotle katika kitabu chake poetics anaeleza kuwa mwigo ni tendo la kufanya au kufuatisha jambo lililofanywa na mtu mwingine kabla yake au uumbaji upya wa kile kilichopo kwa ajili kukifanya bora zaidi. Aristotle aliona asili ya sanaa za maonesho inatokana na mwigo. Maandishi yake katika Poetics yalifafanua sheria au kanuni za utunzi wa tamthiliya, ambazo kwa muda mrefu sana zilichukuliwa na wanasanaa wengi wa michezo ya kuigiza kama mwongozo karibu kote ulaya. Mwigo huwepo maishani mwa binadamu kwa sababu mbalimbali kama vile; binadamu hufurahia kuiga wengine, binadamu hufurahia kuona maigizo. Mara nyingi mtu anapomuiga mtu mwingine hutenda kama yeye. Pia kuiga ni moja kati ya mbinu kubwa ya kujifunza juu ya ulimwengu wake. Kwahiyo ni dhahiri kuwa chimbuko la tamthiliya pia linahusiana kwa karibu sana na uigaji au mwigo.
Nadharia ya Sanaa za maonyesho.
Sanaa za maonyesho; ni uoneshaji wa maisha kisanaa ambapo mwoneshaji na hadhira huwepo mahali pamoja kwa wakati mmoja. Kwa mfano maonesho ya ngoma za kijadi,dansa na majigambo. Sanaa za maonesho ulimwenguni zilichipuka katika kipindi cha “liminoid phase” ambapo kulikuwa na wadhamini mbalimbali wa maonesho hayo hasa Ulaya Magharibi. Ulaya magharibi ndiyo inayosemekana kuwa ya kwanza kufikia kipindi cha “liminoid phase” kutokana na mgawanyiko wa kazi ndani ya jamii.
Tunaposema sanaa za maonesho za kijadi tuna maana ya zile ambazo zimechipuka katika jamii. Sanaa hizo ni pamoja na ngoma, majigambo, miviga, mashairi, na zingine.Hizi zilikuwa zikiambatana na lugha na matendo ya mwili. Mfano maonesho ya “dithyramb” ambayo yalikuwa maalumu kwa mungu wa Wagiriki kwa jina la “Dionysus” ndiyo hasa asili ya tamthiliya huko Ugiriki. Maonesho hayo yaliambatana na itikio (chorus) ambayo iliimba hadithi. Kadri muda ulivyokuwa unapita, itikio lilitoweka na hadithi ikawa inatambwa mfano mtambaji Arion aliziandika kwa ufasaha na huu ukawa mwanzo wa tamthiliya.
Nchini Uingereza, tamthiliya ilianza kujengeka karne ya 10-13BKM tofauti na Ugiriki ambapo tamthiliya zilianzia na maonesho aliyokuwa akifanyiwa Dionysus (mungu wao), nchini Uingereza tamthiliya zilianzia makanisani ambapo misa zilikuwa zikiigizwa (liturgical drama). Haya yalikuwa maigizo ya pasaka ya mwaka 995BKM ambayo inasemekana yaliandikwa kwa misingi ya tamthiliya. Sababu hasa ya kuigiza misa ilikuwa ni kurahisisha ili ieleweke vizuri kwa waumini. Katika maigizo haya baadhi ya sehemu za biblia pia ziliigizwa.
Baadaye nje ya Ulaya hususani Japan, mambo yalikuwa tofauti ambapo kuna drama ziitwazo“Kabuki”ambazo ni mseto wa utambaji wa hadithi, ngoma na shani (spectacle) – kichekesho.Kuna aina nyingine ya drama ya Kijapan iitwayo Noh huchanganya dansa, ushairi, muziki, uigizaji wa kawaida, seti na maleba maalumu yasiyokuwa na uhalisia ili kusawiri miviga (rituals) au matendo ya kidini.
Nchini China (Uchina) drama ilitokana na sherehe za kidini zilizotendwa na makuhani wa kibudha kwa kutumia nyimbo, dansa, na maigizo bubu. Maigizo haya kama ya Kijapan ilikuwa ni faraguzi yaani hapakuwa na mswada wa mchezo mzima bali muhtasari tu ambao ulijawa na uigizaji wenyewe wakati wa maonesho.
Maigizo yaliyokuwa yakifanyika makanisani mfano Uingereza, Uchina na Japan polepole yakaanza kutoka kanisani na kuanza kusawiri maisha ya vijijini ambapo maisha yalianza kuigizwa na huo ndio mwanzo wa tamthiliya kuingia vijijini na kuanza kuzungumzia mambo mengine tofauti na ya kidini.
Barani Afrika, chimbuko la tamthiliya linahusishwa na maigizo ya kitamthiliya ya Misri ambako michezo ya miviga iliyohusu kufa na kufufuka kwa mungu wao aliyeitwa Osiris iliyokuwa ikichezwa kwa miaka kama 2000 kuanzia mwaka 2500KM (Brockett, 1979:04) .Baadhi ya wataalamu wanakubali kuwa drama hizo za kimisri ziliathiri maigizo ya mwanzo ya Wayunani. Mbali na drama za kimisri ambazo huenda ziliandikwa, maigizo yasiyoandikwa hapa Afrika yalikuwa ni sehemu ya matendo yanayosawiri jamii hasa katika miviga ya watoto na maigizo ya watani tangu zamani.
Dhana ya sanaa ya maigizo na hata tamthiliya ikiwa na maana ya utendaji wa dhana, haikuanza tu na majilio ya wakoloni hapa Afrika. Baadhi ya ngoma, burudani, dansi, sherehe kama vile mavuno, matanga na harusi, majigambo ya kiasili na simulizi mbalimbali za Mwafrika zilizaliwa na matambiko katika jamii mbalimbali.
HISTORIA YA FASIHI YA KISWAHILI
Kwa upande wa utamaduni wa waswahili kwa mfano, kabla ya ujilio wa wageni (watu kutoka Ulaya magharibi) na kuleta drama yao, waswahili walikuwa wakitunga na kughani tendi ambazo baadhi zilipata kuandikwa kwa hati za Kiarabu. Tendi hizo ziliwasilishwa kwa namna ya maigizo, matendo na kutofautisha maneno ya wahusika mbalimbali na ya wasimulizi, masuala mbalimbali ya utamaduni wa Waswahili. Maigizo hayo hutoa maelezo kuhusu mandhari, mavazi na vifaa vingine – maelezo ambayo yanafanana na jukwaa la kisasa tunalosoma na kutumia katika michezo ya kuigiza. Drama hizi zilifungamana na fasihi simulizi, hazikuwa za kibiashara, hazikurasimishwa na hazikuandikwa.
Tamthiliya zilizoandikwa ili ziigizwe rasmi jukwaani ni matokeo ya tamhiliya za Ulaya- yaani athari za kimagharibi. Hata hivyo tamthiliya za Kiswahili zilienzi desturi na mila za kijadi pamoja na mielekeo yake. Hii hudhihirishwa kupitia miktadha iliyotumiwa na wasanii katika kazi zao. Mfano tamthiliya kama vile Kinjeketile na Mashetani(E.Hussein), Pambo (P.Muando), Mkwawa wa Uhehe (Mulokozi), Aliyeonja Pepo (C.Topan), Kilio cha Haki (Mazrui .A), Mzalendo Kimath (Ngugi wa Thiongo), na Wingu Jeusi (Chacha.N) ni vielelezo vya uhuishaji wa utamaduni na imani za asili za mwafrika.
Kwa ujumla chimbuko la tamthiliya hujumuisha sanaa za maonesho, mwigo pamoja na miviga (matendo ya dhati), ambapo miviga ilizaa sanaa za maonesho na mwigo. Hii haimanishi kuwa matendo ya dhati yalipotea bali bado yanatumika katika ujenzi wa tamthiliya kwani bado kuna jamii ambazo zipo kwenye kipindi cha mpito- yaani liminal phase, ambao bado hutumia miviga mfano Wamasai, Wakurya ,Wakamba, Wakalejin, Wasukuma, Wairaq, Wabarbaik wote wa Afrika mashariki.
Ukilinganishwa na tanzu nyingine za fasihi ya Kiswahili, utanzu wa tamthiliya ndio mchanga zaidi. Hata hivyo, chimbuko lake kwa upande wa sanaa-tendaji ni la kale mno. Chimbuko lake hasa ni katika fasihi simulizi ya Kiswahili – katika mawasilianao ya moja kwa moja baina ya msimulizi wa ngano na hadhira, katika maigizo mbalimbali ya msimulizi wa ngano, katika ushirikiano wa moja kwa moja baina ya msimulizi na hadhira yake, katika majibizano ya kishairi yanayotokea katika hafla mbalimbali, katika nyimbo na ngoma za watoto na watu wazima, katika michezo ya sarakasi na kadhalika. Kwa hiyo, historia na maendeleo ya tamthiliya nchini Tanzania inaweza kuelezwa kwa kurejelea vipindi vitatu muhimu: Kabla ya Ukoloni, Kipindi cha Ukoloni na Kipindi cha Uhuru.
KABLA YA UKOLONI
 Tamthiliya zilizoandikwa ili ziigizwe jukwaani hazikuwepo kabla ya ukoloni. Mchezo wa kuigiza ulioandikwa ulikuja na wakoloni (Bertoncini, 1989). Aina za sanaa za maonyesho zilizokuwepo zilitofautiana na tamthiliya hii iliyoingizwa na tamaduni ngeni. Zilikuwepo tamthiliya zisizoandikwa, zilizogezwa au kufaraguzwa (improvised) kwa ajili ya kuonyeshwa kwenye shughuli maalumu, kwa mfano sherehe za jando na unyago, mazishi, kutawazwa kwa mtemi, arusi na michezo ya watoto. Tamthiliya hizo zilikuwa na sifa kadha za tamthiliya, yaani hadithi, vitendo, wahusika na waigizaji wao, na dialojia. Isitoshe, zilikuwa na sifa za Sanaa za Maonyesho kama vile: Dhana Inayotendeka, Uwanja Unaotendewa, Watendaji, Hadhira, Kusudio la Kisanaa, Muktadha wa Kisanaa na Ubunifu (Umithilishaji). Tamthiliya hizo hazikuwa na ploti ya ki-Aristotle wala matini yaliyoandikwa. Hivyo hizi zilikuwa tamthiliya-simulizi.
Kipindi Cha Ukoloni (1890–1960) 
Tamthiliya ilianza Tanzania wakati ukoloni ulipoingia hasa kuanzia miaka ya 1920. Ukoloni unahusu jamii mbili ambapo jamii moja yenye nguvu huitawala jamii nyingine. Katika hali kama hii, hutokea tamaduni mbili – utamaduni unaokandamiza na ule unaokandamizwa. Katika kipindi hiki palikuwepo: Tamthiliya za Kizungu, Vichekesho naTamthiliya ya Kiswahili.
Tamthiliya za Kizungu
Tamthiliya za kizungu zilikusudiwa ama kuwaburudisha maofisa na walowezi (masetla) wa kizungu, au kufundisha Bibilia na imani ya Kikristo.Tamthiliya hizi ziliigizwa kuanzia miaka ya 1920, nyingi zilichezwa mashuleni. Shule ndio hasa zilitumika kuonyeshea tamthiliya zilizojaa ujumi, amali na itikadi ya Kibepari. Kwa sababu tamthiliya inahitaji kusomwa na kukaririwa kabla ya kuonyeshwa kwenye jukwaa, basi usomi ulikuwa kigezo kikubwa cha kufanikisha tamthiliya. Hali hii iliwafanya wala tu waliojua kusoma na kuandika Kiingereza waimudu fani hii. Hawa walipatikana shuleni tu ukiondoa wakoloni wenyewe. St. Joseph Convent School, hivi sasa Forodhani, ilianza kuonyesha tamthiliya za Kiingereza kuanzia 1922. Tamthiliya hizo ni kama vile The Sherrif’s Kitchen, The Ugly Duckling ya Milne na The Birds of a Feather ya Francis. Nyingi katika tamthiliya hizi zilikuwa zile za wakati wa Victoria huko Uingereza (1893-1914). Tamthiliya hizi zilijulikana kama ‘Drawing Room Drama’. Zilijishughulisha na masuala ya kinyumbani, yaani jinsi familia ya Kiingereza huishi, matazamio yake na mambo yafafanayo na hayo. Kwa kifupi, tamthiliya hizi zilitakiwa kuwa na ujumi-taaluma wa tamthiliya, yaani lugha na mtindo wa uonyeshaji uliotakiwa Uingereza wakati huo – ‘Four Wall-Bourgeois Theatre’Tamthiliya zote zilikuwa kwenye Kiingereza. Baadhi ya tamthiliya zilitokana na michezo iliyoandikwa na Waingereza, kwa mfano Shakespeare, na baadhi zilikuwa ni za dini ya
Kikristo.
Takriban tamthiliya zote za kipindi hiki zilikuwa ni za kibwanyenye, yaani zisizopingana na mfumo wa ubepari na ukoloni uliokuwepo. Tamthiliya chache mno zilitafsiriwa kwa Kiswahili, kwa mfano, tamthiliya ya Moliere, ‘Le Medecin Malge Lui’ “Tabibu Asiyependa Utabibu”. Mbali na shule, zilianzishwa taasisi zingine zilizojishughulisha na tamthiliya. Hindu Volunteer Corps ambayo ilionyesha tamthiliya za Kihindi ilianzishwa mnamo 1938. Baadaye, vilianzishwa vikundi vya kuigiza tamthiliya za kizungu: Dar es Salaam players (Little Theatre, 1947) na Arusha Little Theatre, 1953 (Lihamba, 1985:38). Tamthiliya katika lugha ya Kiingereza ilizidi kushamiri baada ya kufanyika mkutano wa wakoloni wa Kiingereza huko Cambridge mwaka wa 1948 uliojulikana kama ‘Cambridge Summer Conference’. Mkutano huu uliongelea suala la kutumia maonyesho kama kipengengele kimoja cha kueneza utamaduni wa Kiingereza kwenye makoloni. Kwa hiyo, matombola, brass bendi na tamthiliya vikatiliwa mkazo. Matokeo ya mkutano huu kwenye makoloni ikawa ni uanzishwaji wa mashindano ya tamthiliya shuleni. Mnamo mwaka wa 1957, Baraza la Kiingereza (British Council) lilianzisha mashindano ya uigizaji wa tamthiliya za Kiingereza nchini Tanzania, yaliyoitwa ‘School Drama
Competition’. Tamthiliya zote zilibidi kuwa kwenye lugha fasaha ya Kiingereza. Mashindano hayo yaliendelea hadi 1963, yalipoanza kusimamiwa na Youth Drama Association. Kuanzia wakati huo, tamthliya za Kiswahili zilianza kuhusishwa katika mashindano hayo, na hivyo kuchochea utuzi wa tamthiliya katika lugha hiyo.
Vichekesho
Vichekesho1 ni aina ya tamthiliya-gezwa (zilizotungwa papo kwa hapo bila kuandikwa). Zilianza miaka ya 1920 kwa lengo la kuburudisha wenyeji. Tamthiliya hizo kwa kawaida zilikuwa na vituko vya kuchekesha na ziliwasuta watu waliofikiriwa kuwa ‘washamba’, ‘wajinga’ au ‘wasiostaarabika’. Tamthiliya hizo zilimwonyesha mhusika anayetoka shamba na kwenda kuzuzuka mjini. Vichekesho viliendelea hata baada ya uhuru (na bado vipo) ila dhamira
zake zilibailika.
Tamthiliya-Andishi ya Kiswahili

 Kipindi cha Uhuru

Tamthiliya ya Kizungu
Tamthiliya ya kizungu iliendelea kuigizwa hata baada ya uhuru, hasa mashuleni na katika kumbi maalumu za maonyesho kama Little Theatres. Hata hivyo, umaarufu wake ulipungua kiasi, hususan upande wa Tanzania. Baadhi ya tamtiliya muhimu za kizungu zilianza kutafsiriwa na kuigizwa kwa lugha ya Kiswahili ili zieleweke zaidi na wananchi km. tafsiri za J.K. Nyerere za Shakespeare, Juliasi Kaisari (OUP, 1964) na Mabepari wa Venisi (OUP, 1969); tafsiri za S.S. Mushi za michezo ya Shakespeare ya Makbeth (TPH, 1968) na Tufani (TPH, 1969); Moliere, Mchuuzi Muungwana (A. Morrison, EALB 1961) na Mnafiki (L. Taguaba, TPH 1973); Sophocles, Mfalme Edipode (S.S. Mushi OUP, 1971); Gogol, Mkaguzi Mkuu wa Serikali (C. Mwakasaka, HEB 1979), nk. Licha ya tamthiliya za kizungu, kadhalika tamthiliya za Kiafrika zilizoandikwa kwa lugha za kigeni na lugha nyingine za kiafrika, zilifasiriwa kwa Kiswahili km. Mtawa Mweusi (Ngugi wa Thiong’o, HEB, 1978); Soyinka W. Masaibu ya Ndugu Jero (Mf. A.S. Yahya OUP 1974); O. Ijimere, Kifungo cha Obatala (HEB, 1978); Ngugi wa Thing’o na Ngugi Mirii, Nitaolewa Nikipenda (HEB, 1982); M. Mulokozi (1968), The Tragedy of Mkwawa (Mf. Kahingi, 1970).

Vichekesho
Baada ya uhuru vichekesho vilichua sura tofauti kidogo. Badala ya kuwasuta ‘washamba’ vilianza kuwasuta ‘wazungu weusi’, yaani waafrika wanaoringia elimu au vyeo na kudharau utamaduni wao (Darlite 2/2: 133-152). Vipengele kama matendo, maonyesho na maongezi vilitumiwa katika uundaji wa vichekesho hivi. Baadhi ya vichekesho, hasa vinavyoonyeshwa kwenye mabaa na sehemu nyingine za burudani na starehe, hujaribu kuzungumzia matatizo ya watu wa kawaida, km. matatizo ya familia, ukosefu wa kazi, ukimwi, uhalifu, udanganyifu wa waganga wa jadi, nk.Vipo pia vichekesho vya kisiasa vyenye kuzungumzia kadhia za kisiasa, ubinafsi wa viongozi, matatizo yanayokumba watu vijijini, mijini, nk. Baadhi ya vichekesho vya redio Tanzania, km. “Mahoka” (kipindi kilichoanza mwaka 1974) na “Pwagu na Pwaguzi” (kilianza mwaka 1978), hukejeli na kukemea tabia mbovu za baadhi ya watu, wakiwemo viongozi wa kiasa. Siku hizi vichekesho hutangazwa na vituo vya redio na televisheni, na huonyeshwa mijini kwenye kumbi za starehe.
 Tamthiliya-Andishi ya Kiswahili
Baada ya uhuru utunzi wa tamthiliya ulipamba moto zaidi, hasa upande wa Tanzania. Uhuru uliwafanya waandishi wa tamthiliya kuandika mambo ambayo wasingeweza kuyaandika hapo awali. Waandishi walitumia tamthiliya kuelezea matatizo yanayokabili jamii. Mashindano ya utunzi na uigizaji yaliyoendeshwa na Youth Drama Association nchini Tanzania yaliwawezesha watunzi chipukizi kujitokeza, akiwemo Ebrahim Hussein ambaye tamthiliya yake ya kwanza, Wakati Ukuta (EAPH,1969) ilishinda tuzo katika mashindano hayo. Wengine walikuwa Uhinga na Katalambula ambao walitunga tamthiliya za Kiswahili zilizoonyesha maadili katika jamii. Wakati huo pia ndipo walipoanza kutokea watunzi waliohitimu fani ya sanaa za maonyesho katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam km. E. Hussein, P. Muhando, N. Ngahyoma na G. Uhinga. Kwa mujibu wa Mulama (1983) watunzi walianza kuifungamanisha tamthiya na mahitaji ya nchi ya Tanzania. Uzukaji wa tamthiliya ukaambatana na hali maalumu za kiuchumi na kijamii.

MAREJELEO.

Dhana na historia ya sarufi mapokeo


Dhana ya Sarufi
Sarufi ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala lugha katika matumizi yake ambayo hujumuisha matamshi, maumbo, miundo na maana (Saluhaya, 2010:72).
Massamba na wenzake (1999) Sarufi ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala kila moja kati ya viwango vinne vya lugha ambavyo ni umbo-sauti (fonolojia), umbo-neno (mofolojia), miundo maneno (sintaksia) na umbo maana (semantiki).
Matinde (2012:211) Sarufi ni taaluma ya lugha inayochunguza na kuchanganua vipashio na kanuni mbalimbali zinazotawala muundo wa lugha.
Massamba (2004) anasema, sarufi ni taaluma ya lugha inayohusu uchunguzi na uchanganuzi wa kanuni za vipengele mbalimbali vya lugha.
Kwa ujumla sarufi inaweza kuelezwa kama kanuni, sheria na taratibu zinazomuongoza mzungumzaji au mwandishi kuzungumza au kuandika tungo sahihi zinzoeleweka kwa msikilizaji wa lugha ileile. Kama ni mzawa wa lugha, mtumiaji huwa tayari anazo kanuni hizo (hata katika uzungumzaji), yaani kanuni anakuwa nazo akilini baada ya kusomaau kuishi na watu wa lugha hiyo.
Dhana na historia ya sarufi mapokeo
Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999) wanaeleza kuwa, sarufi mapokeo ni sarufi elekezi ikisisitiza usahihi wa lugha kwa kuonesha sheria ambazo hazina budi kufuatwa, mathalani kufanya muundo fulani wa sentensi usomeke kwa usahihi au sheria ambazo hazina budi kufuatwa ili kufanya matamshi fulani yakubalike kuwa ndio sahihi.
Matinde (2012:211) anaeleza kuwa, mkabala huu wa sarufi mapokeo ni mkabala wa awali ulioshughulikia sarufi ya lugha. Waasisi wake walikuwa wanafalsafa wa Ugiriki. Habwe na Karanja (2004:129) anataja wanafalsafa hao kuwa ni Plato, Aristotle, Dionysus Thrax, na Priscian. Katika kipindi hiki sarufi ilishughulikiwa sambamba na falsafa, dini, fasihi, balagha na mantiki. Plato alikuwa wa kwanza kugawa sentensi katika sehemu kuu mbili mtenda (subject) na kitendwa (object). Hatimaye Aristotle akaendeleza kazi ya mwalimu wake kwa kugawa sentensi katika sehemu kuu tano ambazo pia ndizo aina za maneno; nomino, kitenzi, kivumishi, kiunganishi na kielezi.
Miaka ya 100 K.K, mwanasarufi Myunani Dionysus Thrax aliandika kitabu cha sarufi ambacho ni cha awali kabisa kilichoitwa “Techne Grammatike (The Art of Grammar)”. Mwanasarufi huyu aliainisha sehemu saba za sentensi ambazo ni nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kiunganishi, kielezi na kiingizi.
Dhana ya Neno
Habwe na Karanja (2007:71) wanafafanua kuwa, neno ni kipashio cha kiisimu kinachoundwa na mofimu moja au zaidi.
Saluhaya (2010:135) anadai kuwa, neno ni mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa kwa pamoja na kuleta maana.
Massamba na wenzake (1999:43) katika samikisa wakitilia maanani maelezo ya Lyons (1968:194-208), neno linaweza kufafanuliwa katika misingi ya kiumbo-sauti (yaani, kwa kuchunguza sauti zinazounda umbo zima), kiothografia (yaani kwa kuchunguza herufi zinazotumika katika kuliandika umbo hilo), na kisarufi (yaani kwa kuchunguza kile kinachowakilishwa na umbo husika katika lugha).
Hivyo basi, tunaweza kufasili neno kama silabi au mkusanyiko wa silabi (sauti) unaoandikwa au kutamkwa ili kuleta maana. Maana hiyo yaweza kuwa kamili, yaani inayotoa taarifa kamili au isiwe kamili, yaani ambayo haitoi taarifa kamili kwa msomaji au msikilizaji.
Dhana ya Sentensi
Matinde (2012:157) anafafanua sentensi kuwa ni neno au fungu la maneno lenye uarifishaji mkamilifu. Sentensi huwa na muundo uliokamilika na hujitegemea kimaana.
Kwa ujumla sentensi ni kipashio kikuu katika tungo chenye uwezo wa kutoa taarifa iliyo kamili au isiyo kamili na huwa na muundo wa kiima na kiarifu.


Ufafanuzi wa aina za maneno kwa mujibu wa wanasarufi wa kimapokeo
Wataalamu wengi wa sarufi ya Kiswahili sanifu wanaelekea kukubaliana kwamba katika lugha hii kuna aina za maneno zisizopungua saba. Aina hizi za maneno zimewahi kujadiliwa kwa kina katika vitabu kadhaa vya sarufi vinavyojishughulisha na sarufi miundo na sarufi maumbo. Baadhi ya wataalamu wa sarufi mapokeo waliojadili aina hizo ni Kapinga (1983), Nkwera, Tumi, Mohamed, Massamba na wenzake (1999) na Kihore na wenzake (1999). Aina hizo ni pamoja na:
Nomino
Nomino ni jina linalotaja kitu, kiumbe, hali, dhana au tendo lolote liwalo. Tukiyachunguza kwa makini maelezo haya tunaona kwamba yanaashiria kuwa katika uamilifu wake nomino hufanya kazi ya kukipambanua au kukibainisha kitajwa kwa madhumuni ya kukitofautisha na vitajwa vingine. Kwahiyo nomino si mtajwa tu bali pia ni mtajwa bainishi.
Katika sarufi za kimapokeo, nomino zilijulikana kama majina lakini katika sarufi za kisiku hizi neno jina au majina limeonekana kuwa la kawaida mno na kwamba haliwezi kuwa na mashiko yenye kukidhi mahitajio ya kiistilahi. Kwahiyo neno nomino limependekezwa litumike badala yake (Massamba na wenzake, 1999:39 katika samikisa. Wanasarufi mapokeo wameweka migawanyo ya nomino kama ifuatavyo:
a) Nomino jumuishi - hizi ni nomino zinazohusu majina ambayo hayakibainishi wazi kitu kinachotajwa. Kwa mfano mbuzi, gari, chuo, mtu, kalamu na nyumba.
b) Nomino mahususi – ni yale majina ambayo yanataja vitu, dhana, na viumbe fulani maalumu na kwa kutoa ubainishi ambao ni wa wazi zaidi. Baadhi ya nomino mahususi ni kama vile Masalu, Ijumaa, Februari, Mwanza, Mariam, Herman, Viktoria, Tanzania na Rufiji.
c) Nomino kikundi – hizi ni nimino ambazo huhusu majina yanayotaja vikundi kadhaa vya viumbe. Katika nomino hizi, jina moja huwa linataja jumuiya yenye sifa za namna moja. Kwa mfano baraza, jeshi, familia, shule, bunge, genge, mahakama, kombania na kwaya.
d) Nomino dhahania – ni nomino zinazohusu majina ya vitu, dhana, na viumbe ambavyo kiukweli tunaweza kuviona katika akili tu lakini hatuwezi kuvibainisha kwa macho. Kwa mfano Uchawi, uzee, malaika, mizimu, Mungu ,usingizi na uchovu.
e) Nomino mguso – ni nomino zinazohusu majina ya vitu ambavyo tunaweza kuviona kwa macho na kuvitambua katika uyakinifu wake, na utambumbuzi huu huweza kutokana na kuvigusa, kuvishika au kuvionja kama vile asali, chumvi, kiti, tofali, na tonge.
f) Nomino za hesabu – hili ni kundi la nomino ambalo hutumia kigezo cha uwezekano wa kuhesabika katika uainishaji wake. Hapa tunatofautisha kati ya nomino zinazowakilisha vitu vinavyohesabika na vile visivyohesabika. Nomino za vitu vinavyohesabika ni kama vile watoto, vitu, visu, mifuko na viatu. Nomino zisizohesabika hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haviwezi kugawika, kwa mfano makamasi, mafuta, maji, matope, sukari, mchanga, uji, na nywele.
Vitenzi.
Ni aina ya neno linalotoa taarifa juu ya tendo linalofanyika au linalotendwa na kiumbe au kitu. Wanasarufi mapokeo wamevigawa vitenzi katika aina kuu tatu ambazo ni:
a) Kitenzi kikuu – ni kitenzi ambacho kinaweza kujitokeza peke yake katika sentensi. Mfano anakula, anampiga, tunacheza, wamechoka na anaimba.
b) Kitenzi kisaidizi – ni kitenzi ambacho kinaandamana na kitenzi kikuu katika sentensi. Kwa mfano alikuwa analima, tunapenda kusoma, na amechoka kucheza. Hivyo, maneno yaliyo katika hati mlazo ni vitenzi visaidizi.
c) Kitenzi kishirikishi – ni kile cha umbo ni na si ambacho kinachukuliwa kuwa kinashirikisha vipashio vingine katika sentensi. Kwa mfano Kahigi ni mwalimu bora, huyu msichana si mwerevu.
Vuvumishi.
Ni kipashio ambacho hutoa maelezo zaisi juu ya nomino au kiwakilishi chake. Maelezo kama hayo kwa kawaida huwa namna au jinsi nomino ilivyo, yaani inavyoonekana, inavyofikiriwa, tabia, au idadi yake. Mfano wa vivumishi ni kama vile chafu, dogo, refu, vivu, zuri, embamba, na fupi. Vivumishi vimeweza kugawanywa katika aina kuu zifuatazo:
a) Vivumishi vya sifa – ni vivumishi vinavyotaja tabia au namna vitu vilivyo au vinavyoonekana. Kwa mfano ema, nyenyekevu, pole na katili.
b) Vivumishi vya idadi – ni vivumishi vinavyoonesha jumla au hesabu ya vitu. Aina hii ya vivumishi tunaweza kuigawa katika makundi mawili ambayo ni kundi linaloonesha idadi kwa jumla na kundi linaloonesha idadi kwa hesabu. Kwa mfano ingi, chache, haba na kidogo vilievile tano, tisini, elfu , milioni na tatu.
c) Vivumishi viulizi – ni vivumishi vinavyouliza maswali kuhusiana na nomino inayoandamana navyo. Mfano watu wangapi, miti mingapi, mayai mangapi, watoto wangapi, na viti vingapi.
d) Vivumishi vya pekee – ni maumbo enye na enyewe ambayo katika Kiswahili ndiyo tu huchanganya aina na viambishi vya upatanisho wa kisarufi vinavyojitokeza navyo kimatumizi. Mfano m-tu m-refu, m-ti mrefu, miti mirefu.
Viwakilishi.
Ni aina mojawapo ya maneno katika sarufi ya lugha ambayo uamilifu wake ni kuwakilisha nomino katika miktadha mbalimbali. Kwa mfano viwakilishi nafsi, viwakilishi viashirii, viwakilishi viulizi, viwakilishi vimikilishi, viwakilishi vya idadi na viwakilishi jumla.
Viunganishi.
Ni neno linalotumika kuviweka pamoja vipashio mbalimbali ili kuvifanya viwe kipashio kikuu kimoja. Kwa mfano na, au, wala, na lakini katika sentensi zifuatazo:
Baba na Mama wanalima.
Unapenda chai au uji.
Hana huruma wala upendo.
Wanasarufi mapokeo wamevigawa viunganishi katika makundi makuu mawili kwa kuzingatia msingi wa kimaana kama vile viunganishi vya hadhi sawa na viunganishi vihusishi.
Vielezi.
Ni neno linalotumika kuelezea zaidi juu ya kitenzi. Mfano sana, mno, kabisa, polepole, harakaharaka, zaidi, sawasawa na barabara. Wanasarufi mapokeo wameviainisha vielezi katika aina kuu mbili yaani vielezi halisi na vielezi viingizi. Mfano wa vilelezi halisi ni kama vile mno, sana, bure, hasa, kabisa, ovyo, haraka na sasa. Kwa upande wa vielezi viingizi ni kama vile pu, mwa, na bwe .
Viingizi.
Ni aina ya maneno inayodokeza hisia za msemaji kama vile ya hali yake ya kufurahi, kushangaa, kushtuka, na uchungu. Haya ni maneno kama vile Lo! Alaa! Lahaula! na Aa! Maneno kama haya kwa kawaida huwa yanatumika kabla ya sentensi na aghalabu huwa hayana mfungamano wa kisarufi na sentensi inayofuata. Aina hii ya neno pia huitwa vihisishi. Jina vihisishi limekitwa zaidi katika misingi ya kimaana yaani linahusu zaidi hisia mbalimbali zinazobebwa na maneno hayo. Viingizi navyo vimegawanywa katika makundi mawili nayo ni viingizi halisi na viingizi vya taswira.
Ufafanuzi wa aina za sentensi kwa mujibu wa wanasarufi mapokeo.
Kwa upande wa sentensi, wanasarufi mapokeo wanaainisha aina tatu za sentensi kwa kuzingatia uamilifu wake. Aina hizo ni kama zifuatazo:
i) Sentensi taarifa – hizi ni sentensi zenye kutoa taarifa fulani.
Kwa mfano: Kiranja amechelewa kufika shuleni.
Kahigi kaandika kitabu cha sarufi ya Kiswahili.
ii) Sentensi ulizi – aina hii ya sentensi huwa ina pengo katika sehemu yake ya taarifa. Sentensi hizi hutaka kupata taarifa fulani.
Kwa mfano: Adam ameweza kucheza mpira?
Kalamu yako ni ipi?
iii) Sentensi Agizi – aina hii ya sentensi humuingiza msikilizaji kutenda kitendo fulani. Aghalabu sentensi ya aina hii haina sehemu ya kiima.
Kwa mfano: Toka nyuma uende mbele.
Mwite kiranja wako.
Kwa ujumla, wanasarufi mapokeo kwa kiasi fulani wanatofautiana katika uainishaji wa aina za maneno kwani kuna wengine wametaja aina kumi za maneno badala ya saba. Kwa mfano Habwe na Karanja (2004:130-139) wao wanaainisha aina kumi za maneno ambazo ni nomino, vitenzi, viwakilishi, vivumishi, vielezi, vihusishi, viunganishi, vionyeshi, vihisishi na vibainishi. Hivyo ni vigumu kutambua idadi halisi ya aina za maneno kwa mujibu wa sarufi mapokeo.



MAREJELEO.
Habwe, J. & Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi: Phoenix Publishers.
Habwe, J. & Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi: Phoenix Publishers.
Kapinga, M.C. (1983). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Saalam: TUKI.
Massamba, D.P.B na Wenzake (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA); Sekondari na Vyuo. Dar es Saalam: TUKI.
Matinde, R.S. (2012). Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia; Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD.




Thursday, July 14, 2016

Tanzia ramsa ya ni tanzia inayoishia kwa furaha, vipi kauli hii inaaksi tamthiliya ya Orodha ya Steve Reynolds kwa mujibu wa nadharia ya uhalisia?



Tanzia ramsa ya ni tanzia inayoishia kwa furaha, vipi kauli hii inaaksi tamthiliya ya Orodha ya Steve Reynolds kwa mujibu wa nadharia ya uhalisia?
Maana ya tanzia ramsa
Wamitila (2003:219) anaeleza tanzia ramsa kama aina ya tanzia ambayo inahusisha mbinu za futuhi aghalabu kwa kuishia kwa furaha. Hali hii inaweza kupatikana kwa kuwepo kwa hasidi au muwi anayetubu na kuyajutia makosa au msimamo wake au kuwepo kwa mandhari ya kiulimbwende. Anaendelea kufafanua kuwa tanzia ramsa huweza kutumiwa pia kwa tanzia ambayo ina kisuko cha kuchekesha ambacho kinakuwa kama kijalizo cha msuko mkuu wa kitanzia.
Kutokana na maana hiyo, tunaweza kufafanua tanzia ramsa kuwa ni mchezo wa kuigiza wenye visa au matukio mazito ya kitanzia ambayo kadri ya mchezo unavyoendelea matukio hayo hugeuka ghafla na kuwa ya furaha. Mara nyingi mgeuko huo wa matukio hutokea kipindi ambacho wahusika wake wapo katika kipindi cha kuendewa na mambo vibaya na hatimaye kugeuka na mambo kuenda vizuri, na huwa ni mwishoni mwa mchezo.
Sifa za tanzia ramsa
Tanzia ramsa ina sifa zake ambazo huitofautisha na aina zingine za tamthilia. Baadhi ya sifa hizo ni kama zifuatazo:
  1. Hukejeli ujinga wa binadamu na kuonesha udanganyifu au uovu alionao binadamu.
  2. Matukio katika tanzia ramsa hugeuka gafla kutoka katika hali ya kitanzia kwenda katika hali ya furaha na ugeukaji huu wa matukio haubashiriki. Kwa mfano, katika tamthlia ya Orodha.
  3. Uongo mwingi hutumika, yaani wahusika wake wengi huchorwa na mwandishi kuwa na tabia ya uongo. Kwa mfano Padri James katika tanzia ramsa ya Orodha.
  4. Hadhira haiwaonei huruma wahusika wakuu kutokana na matendo yao maovu wanayofanya bali hukejeliwa na kuchekwa.
  5. Wahusika wakuu huonekana kuendewa na mambo vizuri ingawa hukumbwa na matatizo mengi.
  6. Aghalabu tanzia ramsa huishia kwa furaha.
  7. Wahusika wakuu hufanya harakati mbalimbali za kijikomboa kutokana na tatizo linalowakumba ili kuficha maovu yao, yaani wasionekane waovu kwa jamii yao. Kwa mfano Bwana Ecko katika tamthilia ya Orodha ambaye alijitihadi kwa hali na mali kuitafuta orodha ili asionekane muovu mbele ya mkewe na jamii kwa ujumla, lakini pia padri James, Salim na Juma wanadhihirisha harakati hizo.
Maana ya nadharia ya uhalisia
Malenya, (2012:197) anafafanua kuwa uhalisia unatumika kama njia ya kutathimini hali ya uhalisia wa maisha kiuyakinifu au uhakika wa maisha. Uhalisia unahusu uigaji wa maisha anapopatikana mwandamu. Mwanafalsafa Hegel katika kitabu chake cha Aesthetics alitumia neno uhalisia kumaanisha kazi ya saana iliyo na wahusika ambao matendo yao yanayochochewa na hali ya kisaikolojia iliyowazunguka. Waandishi huzungumzia, huchambua, na kuchagua mambo anayotaka kuyasema huku akisuta maovu katika jamii.
Wafula na Njogu (2007:62) katika kitabu chao cha Nadharia za Uhakiki wa Fasihi wanadai kuwa, uhalisia wa kifasihi unaashiria uwezo wa kusawiri au kuelezea hali kwa kuzingatia uyakinifu au uhakika wa maisha. Vilevile wanaendelea kusema kwamba, uhalisia unahusu uigaji wa mazingira anamopatikana mwanadamu.
Wamitila (2003:272) anafafanua kuwa uhalisia ni mkondo unaosisitiza usawiri wa matukio au maisha katika fasihi kama yalivyo katika maisha ya kila siku. Mmoja kati ya wataalamu wanaohusishwa na dhana hii ni mfuasi wa Marx kutoka Hungary aliyejulikana kama George Lucas ambaye aliamini mambo kadha wa kadha kama vile usawiri wa uhalisia katika ukamilifu wake, kuchunguza undani wa picha inayoonekana ya uhalisia na kugundua sheria za mabadiliko ya kihistoria zinazosababisha hali fulani.
Pia tumkimfasili Senkoro (1987) akirejelea maelezo ya Engles juu ya dhana ya uhalisia anadokeza zaidi na kueleza jambo katika undani na ukweli wake na usawilishaji wa kiukweli wa wahusika katika mazingira yao na matendo yao.
Kwa hiyo, isitilahi uhalisia katika taaluma ya falsafa ilimanisha uhalisia au ukweli wa mawazo dhidi ya falsafa zilizochukuliwa za majitu au dhana tu za kidhahania. Kwa upande wa fasihi na sanaa istilahi uhalisia ilikita mizizi enzi za utawala wa Malkia Victoria wa Uingereza na mapinduzi ya viwanda. Katika nadharia hii maisha yanaelezwa kama yalivyo katika uhalisia wake.
Kwa ujumla nadharia hii imejikita katika mawazo makuu yafuatayo kama yalivyojadiliwa na wataalam mbalimbali wakiwemo Malenya (2012) na Wafula na Njogu (2007):
  • Wanauhalisia hutambua maisha yanayomzunguka binadamu kama chanzo cha ubunifu.
  • Uzingativu wa hali ya juu wa maisha jinsi yalivyo.
  • Jukumu la kazi yoyote ya fasihi (sanaa) ni kuelimisha na kufunza jamii.
  • Wahusika wa kiuhalisia husawiriwa kwa kazi zao za kila siku ili kuonesha uhalisia wa shughuli zao.
  • Tukio la kiuhalisia hutumika huku likitafutiwa sheria za kisayansi ambazo zilisababisha tukio hilo kutokea.
Jinsi ambavyo tanzia ramsa huishia kwa furaha kwa kuzingatia nadharia ya uhalisia.
Tanzia ramsa ni tanzia ambayo kwa kawaida huishia kwa furaha kutokana na mgeuko wa ghafla wa matukio, kwa kuzingatia nadharia ya uhalisia, ufuatao ni ushahidi unaothibitisha kauli hii kwa kurejelea tamthilia ya Orodha ya S.Reynolds:
Tamthiliya ya Orodha ni tanzia ramsa ambayo mtiririko wa hadithi unaanza kujengeka katika tukio la baba Furaha na mama Furaha kujadiliana juu ya malezi na mwenendo wa binti yao Furaha (uk.5). Hali hii inaaksi maisha ndani ya jamii ambapo inaonekana wazazi hukaa na kujadili kuhusiana na mienendo ya watoto wao pale wanapoonekana kutoenenda vyema, lengo kuu likiwa ni kutaka kuwajenga katika njia bora za kuishi katika jamii. Hali hii inasawiri mawazo ya wanauhalisia pale wanaposema kuwa jukumu la kazi yoyote ya fasihi ni kuelimisha na kufunza jamii.
Ni usiku, furaha akiwa amelala na wadogo zake chumbani, sauti ya Mary inasikika dirishani ikimuita Furaha ili waende baa kukutana na akina Bw. Ecko na Juma waliokuwa wakiwasubiria. Wakiwa baa Bw. Ecko anaanza kumtongoza Furaha kwa kumsifia uzuri wake pamoja na kumpa pombe iliyomsababisha kulewa na hatimaye kwenda kulala naye. Kitendo hiki kinasadifu maisha ndani ya jamii kwani vijana wengi huonekana kuingia katika matendo yasiyofaa kutokana na ushawishi wa marafiki na tamaa zisizofaa, hali ambayo huwapelekea kuishia katika matatizo kama vile maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU). Hali hii inasawiri wazo la wanauhalisia linalojikita katika uzingativu wa hali ya juu ya maisha jinsi yalivyo.
Baaada ya Furaha kutembea na Bw. Ecko anaamua kwenda kutubu kwa Padri James. Kutokana na uzuri wa Furaha Padri James anajawa na ushawishi wa kimapenzi dhidi ya binti huyu mrembo. Na siku iliyofuata wakiwa katika chumba cha maombezi, Padri James na Furaha wanaingia katika dimbwi la mahaba na hatimaye kuzini. Kitendo hiki kinasadifu hali halisi ndani ya jamii zetu kwani watu wanapofanya maovu hutafuta njia ya kujitakasa mfano kwenda kanisani kutubu. Lakini pia katika jamii kuna viongozi wa dini ambao si waaminifu kwani hujikuta wakiangukia katika vitendo visivyofaa na waumini wao kwa kisingizio cha kwamba wao nao ni binadamu. Mfano Padri James anasema…Kuna shinikizo kubwa, vishawishi vingi! kwa watu hawa, mimi ndiye Padri wao… lakini mimi pia ni mwanadamu! Mahitaji yote haya ni ya mwanadamu. Hali hii pia inadhihirisha wazo la wanauhalisia kwamba wahusika wa kiuhalisia husawiriwa kwa kazi zao za kila siku ili kuonesha uhalisia wa shughuli zao, mfano Padri James.
Siku moja Furaha akiwa njiani kuelekea sokoni anakutana na Kitunda akiwa na sterio yake begani. Kitunda anaanza kumtongoza kwa kumsifu na kujinadi yeye mwenyewe kupitia sterio yake na uzuri wa mji wa Dar es Salaam. Mfano mazungumzo ya Kitunda na Furaha (uk.13) “Kitunda: Unakwenda wapi; mshikaji?
Furaha: Nimetumwa sokoni na mama.
Kitunda: Wewe, mtoto bomba kichizi. Hee, kwanini hupumziki kidogo na kufaidi
midundo?
Furaha: Siwezi, nitachelewa nyumbani.
Kitunda: Aaa mshikaji, mi sikwambii uwe binti mbaya. Kaa kidogo tu. Yaani
kama hilo unaliona noma. Unaogopa, sivyo?
Furaha: Siogopi…
Kitunda: Hii nimeipata kutoka Dar es Salaam, mshikaji!
Furaha: Dar! Napenda sana nami siku moja nifike huko!
Kitunda: Ni bomu, mshikaji wangu...
Furaha: (Akija karibu zaidi – sasa amevutiwa) Eenh! Na umefika huko?
Kitunda: (Anamtania) Kisura, ni kama jiji la New York ya Afrika Mashariki!
Nakwambia, mwanangu, kule kuna majengo makubwa kiasi…”
Kitushi hiki kinasadifu maisha halisi ndani ya jamii zetu ambapo vijana wa kiume hutumia maneno ya kuwavutia mabinti ili waweze kuwashawishi na hatimaye kutimiza malengo yao ya kuwaingiza katika vitendo vya ngono zembe, hali ambayo hupelekea athari mbalimbali za kiafya kwa vijana hao. Hali hii inadhihirisha wazo la wanauhalisia la uzingatiaji wa maisha ya binadamu jinsi yalivyo.
Salim (mchumba wake Furaha) anarudi kutoka masomoni Dar es Salaam na kukutana na mchumba wake baaada ya kipindi cha miaka miwili. Salim anaamua kumuuliza Furaha kama kaweza kumsubiri kwa muda ambao yeye alikuwa masomoni. Furaha anamjibu kwa kumtoa hofu kuwa kamsubiri na asiwe na hofu juu yake; japo kiukweli Furaha kashavunja ahadi kwa kutembea na wanaume wengine kijijini. Baada ya mazungumzo yao wanaamua kukutana usiku nyuma ya nyumba bila ya Furaha kumueleza ukweli mchumba wake juu ya yale aliyoyatenda na akina Bw. Ecko, Padri James na Kitunda. Mfano mazungumzo ya Furaha na Salim (uk.16-17). Kupitia hali hii ya kutokuwa na uaminifu kati ya Furaha na Salimu wazo la wanauhalisia la kwamba jukumu la kazi yoyote ya fasihi (sanaa) ni kuelimisha na kufunza jamii linadhihirika kwani elimu inapatikana kupitia hali iliyomfika Furaha na Salim.
Wanakijiji wanazungumzia kuhusu tabia ya furaha, wanasema kuwa Furaha amekuwa kama punda kila mtu anampanda pale kijijini. Wakiwa katika mazungumzo hayo, mama Furaha anawakuta na wanaamua kutawanyika isipokuwa mwanakijiji wa tatu ambaye anabaki na mama Furaha. Mwanakijiji huyo anamueleza mama Furaha kuhusu tabia za Furaha. Baada ya mama Furaha kurudi nyumbani alitaka kuyathibitisha kwa mtoto wake yale aliyoyasikia kwa mwanakijiji, lakini Furaha alikataa katakata. Dalili za kuugua Furaha zinaanza kuonekana baada ya kuanza kukohoa mfululizo, kuishiwa nguvu na kupungua uzito. Baada ya kupimwa, vipimo vinathibitisha kuwa Furaha ana VVU/UKIMWI. Katika jamii yetu ya sasa kuna akina Furaha wengi ambao wao wanapoulizwa na kuonywa kuhusu tabia mbaya wao hawataki kusema ukweli wala kusikiliza mwishowe kuishia katika matatizo kama ya Furaha. Hali hii husawiri wazo la wanaualisia ambalo ni uzingativu wa hali ya juu ya maisha jinsi yalivyo.
Habari za ugonjwa wa Furaha zinaenea kijijini pale ambapo wanakijiji wanazungumza kuhusu ugonjwa wake huku wakiwa hawajui ni ugonjwa gani na kaupataje. Wengine wanasema unaambukizwa kwa kugusana (uk 25-26), wengine wanasema hata kwa kuwa na mgonjwa katika chumba kimoja. Pia habari zinaenea kuwa Furaha ameandika barua ambayo ina orodha ya majina ya wanaume waliotembea naye, kitu knaichomfanya Salim kwenda kwa Furaha ili kujua ukweli huo na ikiwezekana aione hiyo barua lakini Furaha anakataa kumpatia. Salim anafukuzwa na Mama Furaha bila kufanikiwa kuiona ile barua. Baada ya pale Furaha anakata roho mikononi mwa mama yake baada ya kuugua kwa muda mrefu. Baada ya kifo cha Furaha, Bw. Ecko, Juma na Kitunda wanaingiwa na wasiwasi kuhusu ile orodha iliyoachwa na Furaha huenda ikawa na majina yao. Hali hii inasadifu uhalisia katika jamii yetu kwani watu wengi wamekuwa wakieneza taarifa za wagonjwa hasa kwa wale ambao wanakuwa na gonjwa la UKIMWI bila hata kuwa na uelewa wa nini chanzo cha ugonjwa huo. Imani za kishirikina pia zimekuwa zikihusishwa na ugonjwa huo. Kitushi hiki kinasawiri wazo la wanauhalisia kuwa tukio la kiuhalisia hujadiliwa huku likitafutiwa sheria za kisayansi.
Baada ya kupata taarifa hizo za Orodha iliyoandikwa na Furaha, Bw. Ecko, Kitunda na Padri James nao wanaanza harakati za kuisaka ili kujiepusha na aibu katika kijiji chao. Bw. Ecko na Juma wanaingia kwenye chumba chenye maiti ya Furaha na kuanza kutafuta ile barua, wanakutwa na baba Furaha lakini wanajificha kwenye jeneza lenye maiti. Baadaye Kitunda anaingia na wote watatu wanaisaka ile barua bila mafanikio na hatimaye kukimbia baada ya kukutwa kwa mara nyingine tena. Siku ya mazishi Padri James naye anajitahidi kuisaka orodha sehemu mbalimbali ndani kwa akina Furaha baada ya kuomba aachwe peke yake ili akusanye mawazo matakatifu. Padri James anatafuta barua kabatini, kwenye makochi, hadi kwenye chungu kidogo ambacho kinang`ang`ania mkononi mwake bila kufanikiwa kuipata barua, na anapokutwa anadai anatafuta rozali ilihali ipo shingoni mwake. Vivyo hivyo watu katika jamii zetu hutafuta mbinu mbalimbali za kutatua tatizo ili kuficha aibu baada ya kufanya mambo yasiyokubalika katika jamii. Hali hii inasawiri wazo la wanaualisia kuwa, wanaualisia hutambua maisha yanayomzuka binadamu kama chanzo cha ubunifu.
Tamthiliya hii inaishia kwa mazishi ya Furaha ambapo siku hiyo asubuhi akina Bw.Ecko, Juma na Kitunda wanaonekana wakiwa baa wakisimuliana msako wa barua siku iliyopita. Pia wakiwa mazishini wanaonekana wakiwa na wasiwasi wa majina yao kusomwa kwani bado hawajafanikiwa kuipata ile orodha. Mama Furaha anapojiandaa kusoma ile barua, Salim anaikwapua na kuichanachana. Baada ya hapo akina Bw. Ecko, Juma, Kitunda na Salim wanajawa na furaha na hata Padri James kwani yeye mwenyewe ndiye mmoja wa wahusika hao waliokuwa wakiisaka ile orodha. Hii inadhihirisha ukamilifu wa tanzia ramsa kuishia kwa furaha. Isitoshe hata baada ya vile vipande kuokotwa na ujumbe ulioachwa na Furaha kusomwa wanakijiji wanajawa na furaha kwani wamepata elimu kuhusu gonjwa la UKIMWI. Ujumbe huo ni orodha ya mambo kumi ambayo yanaweza kumsababishia mtu kupata au kuepuka maambukizi ya VVU/UKIMWI, mambo hayo ni kondomu, uaminifu, uelewa, elimu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo, na msamaha. Kupitia orodha hii wazo la wanauhalisia linadhihirika kwamba jukumu la kazi yoyote ya fasihi (Sanaa) ni kuelimisha na kufunza jamii.
Hivyo tunaweza kuhitimsha kuwa tamthiliya ya Orodha imejikita zaidi katika uhalisia ambao umejitokeza kupitia wahusika waliotumika, kwni wapo walioamini ushirikina kama mama Furaha, usaliti katika mapenzi kama vile Bw.Ecko, Salim, na Furaha, na ukahaba ambao katika jamii umeshamiri hasa maeneo ya mjini. Pia katika jamii yetu kuna watu kama akina Juma, Padri James na Salim ambao hawapendi ukweli na uwazi. Fauka ya hayo, ukosefu wa adabu kwa vijana, kuziba masikio na kutopokea ushauri wa wazazi, ulevi na matumizi ya madawa ni tatizo lingine linalowakumba vijana kwa mfano Kitunda katika tamthiliya hii. Hivyo basi, ufahamu wa mambo haya mwishoni mwa tanzia ramsa hukamilisha sifa yake ya kuishia kwa furaha ikiwa ni sifa muhimu ya kuitofautisha tanzia ramsa na tamthiliya zingine.




MAREJEO.
Malenya, M.M. (2012). Matumizi ya Lugha Katika Fasihi Simulizi. Mwanza: Inland
Press.
Reynolds, S. (2006). Orodha. Dar es Salaam: Macmillan Aidan Ltd.
Senkoro, F.E.M.K. (1987). Fasihi na Jamii. Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.
Wafula, R. M. & Njogu, K. (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: The Jomo
Kenyata Foundation.
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: English press.
Focus Publications Ltd.




hakiki na tuma maoni au mapendekezo kuhusu makala hii ya andiko langu la uchunguandiko langu

ANDIKO LA UCHUNGU (Kwa shemeji zangu na wanangu)           NYAMBUYA OGUCHU,                            S.L.P 777666,       ...