Thursday, July 14, 2016

Tanzia ramsa ya ni tanzia inayoishia kwa furaha, vipi kauli hii inaaksi tamthiliya ya Orodha ya Steve Reynolds kwa mujibu wa nadharia ya uhalisia?



Tanzia ramsa ya ni tanzia inayoishia kwa furaha, vipi kauli hii inaaksi tamthiliya ya Orodha ya Steve Reynolds kwa mujibu wa nadharia ya uhalisia?
Maana ya tanzia ramsa
Wamitila (2003:219) anaeleza tanzia ramsa kama aina ya tanzia ambayo inahusisha mbinu za futuhi aghalabu kwa kuishia kwa furaha. Hali hii inaweza kupatikana kwa kuwepo kwa hasidi au muwi anayetubu na kuyajutia makosa au msimamo wake au kuwepo kwa mandhari ya kiulimbwende. Anaendelea kufafanua kuwa tanzia ramsa huweza kutumiwa pia kwa tanzia ambayo ina kisuko cha kuchekesha ambacho kinakuwa kama kijalizo cha msuko mkuu wa kitanzia.
Kutokana na maana hiyo, tunaweza kufafanua tanzia ramsa kuwa ni mchezo wa kuigiza wenye visa au matukio mazito ya kitanzia ambayo kadri ya mchezo unavyoendelea matukio hayo hugeuka ghafla na kuwa ya furaha. Mara nyingi mgeuko huo wa matukio hutokea kipindi ambacho wahusika wake wapo katika kipindi cha kuendewa na mambo vibaya na hatimaye kugeuka na mambo kuenda vizuri, na huwa ni mwishoni mwa mchezo.
Sifa za tanzia ramsa
Tanzia ramsa ina sifa zake ambazo huitofautisha na aina zingine za tamthilia. Baadhi ya sifa hizo ni kama zifuatazo:
  1. Hukejeli ujinga wa binadamu na kuonesha udanganyifu au uovu alionao binadamu.
  2. Matukio katika tanzia ramsa hugeuka gafla kutoka katika hali ya kitanzia kwenda katika hali ya furaha na ugeukaji huu wa matukio haubashiriki. Kwa mfano, katika tamthlia ya Orodha.
  3. Uongo mwingi hutumika, yaani wahusika wake wengi huchorwa na mwandishi kuwa na tabia ya uongo. Kwa mfano Padri James katika tanzia ramsa ya Orodha.
  4. Hadhira haiwaonei huruma wahusika wakuu kutokana na matendo yao maovu wanayofanya bali hukejeliwa na kuchekwa.
  5. Wahusika wakuu huonekana kuendewa na mambo vizuri ingawa hukumbwa na matatizo mengi.
  6. Aghalabu tanzia ramsa huishia kwa furaha.
  7. Wahusika wakuu hufanya harakati mbalimbali za kijikomboa kutokana na tatizo linalowakumba ili kuficha maovu yao, yaani wasionekane waovu kwa jamii yao. Kwa mfano Bwana Ecko katika tamthilia ya Orodha ambaye alijitihadi kwa hali na mali kuitafuta orodha ili asionekane muovu mbele ya mkewe na jamii kwa ujumla, lakini pia padri James, Salim na Juma wanadhihirisha harakati hizo.
Maana ya nadharia ya uhalisia
Malenya, (2012:197) anafafanua kuwa uhalisia unatumika kama njia ya kutathimini hali ya uhalisia wa maisha kiuyakinifu au uhakika wa maisha. Uhalisia unahusu uigaji wa maisha anapopatikana mwandamu. Mwanafalsafa Hegel katika kitabu chake cha Aesthetics alitumia neno uhalisia kumaanisha kazi ya saana iliyo na wahusika ambao matendo yao yanayochochewa na hali ya kisaikolojia iliyowazunguka. Waandishi huzungumzia, huchambua, na kuchagua mambo anayotaka kuyasema huku akisuta maovu katika jamii.
Wafula na Njogu (2007:62) katika kitabu chao cha Nadharia za Uhakiki wa Fasihi wanadai kuwa, uhalisia wa kifasihi unaashiria uwezo wa kusawiri au kuelezea hali kwa kuzingatia uyakinifu au uhakika wa maisha. Vilevile wanaendelea kusema kwamba, uhalisia unahusu uigaji wa mazingira anamopatikana mwanadamu.
Wamitila (2003:272) anafafanua kuwa uhalisia ni mkondo unaosisitiza usawiri wa matukio au maisha katika fasihi kama yalivyo katika maisha ya kila siku. Mmoja kati ya wataalamu wanaohusishwa na dhana hii ni mfuasi wa Marx kutoka Hungary aliyejulikana kama George Lucas ambaye aliamini mambo kadha wa kadha kama vile usawiri wa uhalisia katika ukamilifu wake, kuchunguza undani wa picha inayoonekana ya uhalisia na kugundua sheria za mabadiliko ya kihistoria zinazosababisha hali fulani.
Pia tumkimfasili Senkoro (1987) akirejelea maelezo ya Engles juu ya dhana ya uhalisia anadokeza zaidi na kueleza jambo katika undani na ukweli wake na usawilishaji wa kiukweli wa wahusika katika mazingira yao na matendo yao.
Kwa hiyo, isitilahi uhalisia katika taaluma ya falsafa ilimanisha uhalisia au ukweli wa mawazo dhidi ya falsafa zilizochukuliwa za majitu au dhana tu za kidhahania. Kwa upande wa fasihi na sanaa istilahi uhalisia ilikita mizizi enzi za utawala wa Malkia Victoria wa Uingereza na mapinduzi ya viwanda. Katika nadharia hii maisha yanaelezwa kama yalivyo katika uhalisia wake.
Kwa ujumla nadharia hii imejikita katika mawazo makuu yafuatayo kama yalivyojadiliwa na wataalam mbalimbali wakiwemo Malenya (2012) na Wafula na Njogu (2007):
  • Wanauhalisia hutambua maisha yanayomzunguka binadamu kama chanzo cha ubunifu.
  • Uzingativu wa hali ya juu wa maisha jinsi yalivyo.
  • Jukumu la kazi yoyote ya fasihi (sanaa) ni kuelimisha na kufunza jamii.
  • Wahusika wa kiuhalisia husawiriwa kwa kazi zao za kila siku ili kuonesha uhalisia wa shughuli zao.
  • Tukio la kiuhalisia hutumika huku likitafutiwa sheria za kisayansi ambazo zilisababisha tukio hilo kutokea.
Jinsi ambavyo tanzia ramsa huishia kwa furaha kwa kuzingatia nadharia ya uhalisia.
Tanzia ramsa ni tanzia ambayo kwa kawaida huishia kwa furaha kutokana na mgeuko wa ghafla wa matukio, kwa kuzingatia nadharia ya uhalisia, ufuatao ni ushahidi unaothibitisha kauli hii kwa kurejelea tamthilia ya Orodha ya S.Reynolds:
Tamthiliya ya Orodha ni tanzia ramsa ambayo mtiririko wa hadithi unaanza kujengeka katika tukio la baba Furaha na mama Furaha kujadiliana juu ya malezi na mwenendo wa binti yao Furaha (uk.5). Hali hii inaaksi maisha ndani ya jamii ambapo inaonekana wazazi hukaa na kujadili kuhusiana na mienendo ya watoto wao pale wanapoonekana kutoenenda vyema, lengo kuu likiwa ni kutaka kuwajenga katika njia bora za kuishi katika jamii. Hali hii inasawiri mawazo ya wanauhalisia pale wanaposema kuwa jukumu la kazi yoyote ya fasihi ni kuelimisha na kufunza jamii.
Ni usiku, furaha akiwa amelala na wadogo zake chumbani, sauti ya Mary inasikika dirishani ikimuita Furaha ili waende baa kukutana na akina Bw. Ecko na Juma waliokuwa wakiwasubiria. Wakiwa baa Bw. Ecko anaanza kumtongoza Furaha kwa kumsifia uzuri wake pamoja na kumpa pombe iliyomsababisha kulewa na hatimaye kwenda kulala naye. Kitendo hiki kinasadifu maisha ndani ya jamii kwani vijana wengi huonekana kuingia katika matendo yasiyofaa kutokana na ushawishi wa marafiki na tamaa zisizofaa, hali ambayo huwapelekea kuishia katika matatizo kama vile maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU). Hali hii inasawiri wazo la wanauhalisia linalojikita katika uzingativu wa hali ya juu ya maisha jinsi yalivyo.
Baaada ya Furaha kutembea na Bw. Ecko anaamua kwenda kutubu kwa Padri James. Kutokana na uzuri wa Furaha Padri James anajawa na ushawishi wa kimapenzi dhidi ya binti huyu mrembo. Na siku iliyofuata wakiwa katika chumba cha maombezi, Padri James na Furaha wanaingia katika dimbwi la mahaba na hatimaye kuzini. Kitendo hiki kinasadifu hali halisi ndani ya jamii zetu kwani watu wanapofanya maovu hutafuta njia ya kujitakasa mfano kwenda kanisani kutubu. Lakini pia katika jamii kuna viongozi wa dini ambao si waaminifu kwani hujikuta wakiangukia katika vitendo visivyofaa na waumini wao kwa kisingizio cha kwamba wao nao ni binadamu. Mfano Padri James anasema…Kuna shinikizo kubwa, vishawishi vingi! kwa watu hawa, mimi ndiye Padri wao… lakini mimi pia ni mwanadamu! Mahitaji yote haya ni ya mwanadamu. Hali hii pia inadhihirisha wazo la wanauhalisia kwamba wahusika wa kiuhalisia husawiriwa kwa kazi zao za kila siku ili kuonesha uhalisia wa shughuli zao, mfano Padri James.
Siku moja Furaha akiwa njiani kuelekea sokoni anakutana na Kitunda akiwa na sterio yake begani. Kitunda anaanza kumtongoza kwa kumsifu na kujinadi yeye mwenyewe kupitia sterio yake na uzuri wa mji wa Dar es Salaam. Mfano mazungumzo ya Kitunda na Furaha (uk.13) “Kitunda: Unakwenda wapi; mshikaji?
Furaha: Nimetumwa sokoni na mama.
Kitunda: Wewe, mtoto bomba kichizi. Hee, kwanini hupumziki kidogo na kufaidi
midundo?
Furaha: Siwezi, nitachelewa nyumbani.
Kitunda: Aaa mshikaji, mi sikwambii uwe binti mbaya. Kaa kidogo tu. Yaani
kama hilo unaliona noma. Unaogopa, sivyo?
Furaha: Siogopi…
Kitunda: Hii nimeipata kutoka Dar es Salaam, mshikaji!
Furaha: Dar! Napenda sana nami siku moja nifike huko!
Kitunda: Ni bomu, mshikaji wangu...
Furaha: (Akija karibu zaidi – sasa amevutiwa) Eenh! Na umefika huko?
Kitunda: (Anamtania) Kisura, ni kama jiji la New York ya Afrika Mashariki!
Nakwambia, mwanangu, kule kuna majengo makubwa kiasi…”
Kitushi hiki kinasadifu maisha halisi ndani ya jamii zetu ambapo vijana wa kiume hutumia maneno ya kuwavutia mabinti ili waweze kuwashawishi na hatimaye kutimiza malengo yao ya kuwaingiza katika vitendo vya ngono zembe, hali ambayo hupelekea athari mbalimbali za kiafya kwa vijana hao. Hali hii inadhihirisha wazo la wanauhalisia la uzingatiaji wa maisha ya binadamu jinsi yalivyo.
Salim (mchumba wake Furaha) anarudi kutoka masomoni Dar es Salaam na kukutana na mchumba wake baaada ya kipindi cha miaka miwili. Salim anaamua kumuuliza Furaha kama kaweza kumsubiri kwa muda ambao yeye alikuwa masomoni. Furaha anamjibu kwa kumtoa hofu kuwa kamsubiri na asiwe na hofu juu yake; japo kiukweli Furaha kashavunja ahadi kwa kutembea na wanaume wengine kijijini. Baada ya mazungumzo yao wanaamua kukutana usiku nyuma ya nyumba bila ya Furaha kumueleza ukweli mchumba wake juu ya yale aliyoyatenda na akina Bw. Ecko, Padri James na Kitunda. Mfano mazungumzo ya Furaha na Salim (uk.16-17). Kupitia hali hii ya kutokuwa na uaminifu kati ya Furaha na Salimu wazo la wanauhalisia la kwamba jukumu la kazi yoyote ya fasihi (sanaa) ni kuelimisha na kufunza jamii linadhihirika kwani elimu inapatikana kupitia hali iliyomfika Furaha na Salim.
Wanakijiji wanazungumzia kuhusu tabia ya furaha, wanasema kuwa Furaha amekuwa kama punda kila mtu anampanda pale kijijini. Wakiwa katika mazungumzo hayo, mama Furaha anawakuta na wanaamua kutawanyika isipokuwa mwanakijiji wa tatu ambaye anabaki na mama Furaha. Mwanakijiji huyo anamueleza mama Furaha kuhusu tabia za Furaha. Baada ya mama Furaha kurudi nyumbani alitaka kuyathibitisha kwa mtoto wake yale aliyoyasikia kwa mwanakijiji, lakini Furaha alikataa katakata. Dalili za kuugua Furaha zinaanza kuonekana baada ya kuanza kukohoa mfululizo, kuishiwa nguvu na kupungua uzito. Baada ya kupimwa, vipimo vinathibitisha kuwa Furaha ana VVU/UKIMWI. Katika jamii yetu ya sasa kuna akina Furaha wengi ambao wao wanapoulizwa na kuonywa kuhusu tabia mbaya wao hawataki kusema ukweli wala kusikiliza mwishowe kuishia katika matatizo kama ya Furaha. Hali hii husawiri wazo la wanaualisia ambalo ni uzingativu wa hali ya juu ya maisha jinsi yalivyo.
Habari za ugonjwa wa Furaha zinaenea kijijini pale ambapo wanakijiji wanazungumza kuhusu ugonjwa wake huku wakiwa hawajui ni ugonjwa gani na kaupataje. Wengine wanasema unaambukizwa kwa kugusana (uk 25-26), wengine wanasema hata kwa kuwa na mgonjwa katika chumba kimoja. Pia habari zinaenea kuwa Furaha ameandika barua ambayo ina orodha ya majina ya wanaume waliotembea naye, kitu knaichomfanya Salim kwenda kwa Furaha ili kujua ukweli huo na ikiwezekana aione hiyo barua lakini Furaha anakataa kumpatia. Salim anafukuzwa na Mama Furaha bila kufanikiwa kuiona ile barua. Baada ya pale Furaha anakata roho mikononi mwa mama yake baada ya kuugua kwa muda mrefu. Baada ya kifo cha Furaha, Bw. Ecko, Juma na Kitunda wanaingiwa na wasiwasi kuhusu ile orodha iliyoachwa na Furaha huenda ikawa na majina yao. Hali hii inasadifu uhalisia katika jamii yetu kwani watu wengi wamekuwa wakieneza taarifa za wagonjwa hasa kwa wale ambao wanakuwa na gonjwa la UKIMWI bila hata kuwa na uelewa wa nini chanzo cha ugonjwa huo. Imani za kishirikina pia zimekuwa zikihusishwa na ugonjwa huo. Kitushi hiki kinasawiri wazo la wanauhalisia kuwa tukio la kiuhalisia hujadiliwa huku likitafutiwa sheria za kisayansi.
Baada ya kupata taarifa hizo za Orodha iliyoandikwa na Furaha, Bw. Ecko, Kitunda na Padri James nao wanaanza harakati za kuisaka ili kujiepusha na aibu katika kijiji chao. Bw. Ecko na Juma wanaingia kwenye chumba chenye maiti ya Furaha na kuanza kutafuta ile barua, wanakutwa na baba Furaha lakini wanajificha kwenye jeneza lenye maiti. Baadaye Kitunda anaingia na wote watatu wanaisaka ile barua bila mafanikio na hatimaye kukimbia baada ya kukutwa kwa mara nyingine tena. Siku ya mazishi Padri James naye anajitahidi kuisaka orodha sehemu mbalimbali ndani kwa akina Furaha baada ya kuomba aachwe peke yake ili akusanye mawazo matakatifu. Padri James anatafuta barua kabatini, kwenye makochi, hadi kwenye chungu kidogo ambacho kinang`ang`ania mkononi mwake bila kufanikiwa kuipata barua, na anapokutwa anadai anatafuta rozali ilihali ipo shingoni mwake. Vivyo hivyo watu katika jamii zetu hutafuta mbinu mbalimbali za kutatua tatizo ili kuficha aibu baada ya kufanya mambo yasiyokubalika katika jamii. Hali hii inasawiri wazo la wanaualisia kuwa, wanaualisia hutambua maisha yanayomzuka binadamu kama chanzo cha ubunifu.
Tamthiliya hii inaishia kwa mazishi ya Furaha ambapo siku hiyo asubuhi akina Bw.Ecko, Juma na Kitunda wanaonekana wakiwa baa wakisimuliana msako wa barua siku iliyopita. Pia wakiwa mazishini wanaonekana wakiwa na wasiwasi wa majina yao kusomwa kwani bado hawajafanikiwa kuipata ile orodha. Mama Furaha anapojiandaa kusoma ile barua, Salim anaikwapua na kuichanachana. Baada ya hapo akina Bw. Ecko, Juma, Kitunda na Salim wanajawa na furaha na hata Padri James kwani yeye mwenyewe ndiye mmoja wa wahusika hao waliokuwa wakiisaka ile orodha. Hii inadhihirisha ukamilifu wa tanzia ramsa kuishia kwa furaha. Isitoshe hata baada ya vile vipande kuokotwa na ujumbe ulioachwa na Furaha kusomwa wanakijiji wanajawa na furaha kwani wamepata elimu kuhusu gonjwa la UKIMWI. Ujumbe huo ni orodha ya mambo kumi ambayo yanaweza kumsababishia mtu kupata au kuepuka maambukizi ya VVU/UKIMWI, mambo hayo ni kondomu, uaminifu, uelewa, elimu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo, na msamaha. Kupitia orodha hii wazo la wanauhalisia linadhihirika kwamba jukumu la kazi yoyote ya fasihi (Sanaa) ni kuelimisha na kufunza jamii.
Hivyo tunaweza kuhitimsha kuwa tamthiliya ya Orodha imejikita zaidi katika uhalisia ambao umejitokeza kupitia wahusika waliotumika, kwni wapo walioamini ushirikina kama mama Furaha, usaliti katika mapenzi kama vile Bw.Ecko, Salim, na Furaha, na ukahaba ambao katika jamii umeshamiri hasa maeneo ya mjini. Pia katika jamii yetu kuna watu kama akina Juma, Padri James na Salim ambao hawapendi ukweli na uwazi. Fauka ya hayo, ukosefu wa adabu kwa vijana, kuziba masikio na kutopokea ushauri wa wazazi, ulevi na matumizi ya madawa ni tatizo lingine linalowakumba vijana kwa mfano Kitunda katika tamthiliya hii. Hivyo basi, ufahamu wa mambo haya mwishoni mwa tanzia ramsa hukamilisha sifa yake ya kuishia kwa furaha ikiwa ni sifa muhimu ya kuitofautisha tanzia ramsa na tamthiliya zingine.




MAREJEO.
Malenya, M.M. (2012). Matumizi ya Lugha Katika Fasihi Simulizi. Mwanza: Inland
Press.
Reynolds, S. (2006). Orodha. Dar es Salaam: Macmillan Aidan Ltd.
Senkoro, F.E.M.K. (1987). Fasihi na Jamii. Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.
Wafula, R. M. & Njogu, K. (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: The Jomo
Kenyata Foundation.
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: English press.
Focus Publications Ltd.




No comments:

Post a Comment

hakiki na tuma maoni au mapendekezo kuhusu makala hii ya andiko langu la uchunguandiko langu

ANDIKO LA UCHUNGU (Kwa shemeji zangu na wanangu)           NYAMBUYA OGUCHU,                            S.L.P 777666,       ...