SWALI:
Sarufi miundo virai inatofautianaje na Sarufi geuzi?
Sarufi
ni nini ?
Kihore na wenzake
(2008) wakimnukuu Gaynor (1968:88) wanaeleza kuwa sarufi ni sayansi
ya muundo wa lugha pamoja na sheria, kanuni na matumizi yake ambayo
kwa kawaida hukubalika kwa watumiaji wake.
Massamba na wenzake
(2009:31) wanaeleza kuwa sarufi ni kanuni, sheria au taratibu za
uchambuzi zinazotawala lugha.
Saluhaya (2010:72)
anadai kuwa sarufi ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala lugha
katika matumizi yake ambayo hujumuisha matamshi, maumbo, miundo na
maana. Taaluma hii husisitiza kanuni zitumikazo katika uchambuzi wa
lugha katika viwango vinne vilivyotajwa hapo juu.
Sarufi miundo virai
Hiki ni kitengo cha
sarufi geuza maumbo zalishi ambacho hujikita katika matumizi ya
sheria chache kuzalisha sentensi nyingi zisizo na kikomo ambazo zina
usarufi na hata zile ambazo hazijawahi kutungwa(Matinde, 2012:233).
Sarufi miundo virai
ni mkabala wa kuchambua lugha kwa kuigawa sentensi katika virai
vinavyoiunda na kasha kuvichanganua zaidi hadi kufikia neon moja moja
lililokiunda kirai.
Sarufi
Geuzi
Sarufi geuzi ni
utaratibu wa kubadili maumbo ya maneno kuwa maumbo mengine kwa
kufuata kanuni maalumu. Sarufi hii hujengwa kwa wazo kwamba katika
lugha kuna sentensi ambazo huwa ni za msingi, ambazo kutokana na
kaida mahususi sentensi zingine huweza kuzalishwa na sentensi hizo
(Matinde, 2012:231). Ugeuzaji huu huathiri muundo wa sentensi na wala
si maana ya sentensi. Kwa mfano;
(a) John amemchapa
Bigile.
(b) Bigile
amechapwa na John.
Hivyo basi, ugeuzaji
ni mbinu ya kisarufi ambayo hutumiwa katika sarufi geuza maumbo
zalishi kuzalisha sentensi lukuki kwa kufuta sheria au kanuni
maalumu.
Kwa mujibu wa Habwe
na Karanja (2007), Matinde, (2012) wanaonesha utofauti uliopo kati ya
sarufi miundo virai na sarufi geuzi kama ifuatavyo:
Tofauti katika
maana, sarufi geuzi maumbo ni utaratibu wa kubadili maumbo kuwa
maumbo mengine kwa kufuata kanuni maalumu. Ilhali sarufi miundo virai
ni kitengo cha sarufi geuzi maumbo zalishi ambacho hujikita katika
matumizi ya sheria chache kuzalisha sentensi nyingi zisizo na ukomo.
Tofauti katika
uchanganuzi wa sentensi, sarufi geuzi huweza kuchanganua sentensi
zenye maumbo tofauti. Kwa mfano sentensi sahili, changamano au
ambatano ilhali sarufi miundo virai hujikita katika kuchanganua
sentensi sahili peke yake.
Mfano; Rajabu ni
mwana wangu.
Tofauti katika
uchopekaji wa viambajengo, sarufi geuzi huweza kuchopeka viambajengo
katika sentensi na kuifanya sentensi hiyo kuwa tenda au tendwa. Kwa
mfano, sentensi ya kauli ya kutenda inapogeuzwa na kuwa katika hali
ya kutendwa kuna elementi ambazo huchopekwa.
Mfano; (a) Changwe
anampiga mtoto
(b)
Mtoto anapigwa na Alpha.
Hapa tunaona mofu
{-w} na kihusishi {na} huchopekwa katika sentensi (a) na kuifanya
sentensi hiyo kuwa ya kauli ya kutendwa katika (b). Ilhali sarufi
miundo virai uchopekaji huo haujitokezi na hivyo kutokuonyesha
mahusiano kati ya kauli tendi na tendwa.
Tofauti ya waasisi,
sarufi geuzi iliasisiwa na mwanasarufi aitwaye Noam Chomsky (1957)
ambaye anadai kuwa nadharia hii ya sarufi geuzi ilizuka ili
kurekebisha taratibu za sarufi za awali. Yeye alidai kuwa sarufi za
awali hazingeweza kuonyesha kuwa sentensi ya kauli ya kutenda na ile
ya kauli ya kutendwa zinatokana na muundo mmoja wa ndani. Pia sarufi
za awali hazingeweza kuonyesha mahusiano ya sentensi zinazotofautiana
kwa ndani lakini ambazo zilikuwa na muundo wan je mmoja. Kwa mfano;
Herman alinunuliwa shati na mwanawe.
Sura hii ya nje ya
sentensi huwa ina sentensi kadhaa katika muundo wake wa ndani. Wakati
sarufi miundo virai iliasisiwa na Bussmann (1996) ambaye anafafanua
kwamba sheria miundo virai ni sheria zinazoonyesha mpangilio na
ujenzi wa virai katika lugha, hivyo sheria hii huonyesha kuandikwa
tena kwa viambajengo. Sheria kama,
S = KN+KT
yaani
S = sentensi
KN
= kikundi nomino/kirai nomino
KT
= kikundi tenzi/kirai kitenzi
Inamaanisha kuwa
sentensi inaweza kuandikwa kama Kikundi Nomino kikifuatwa na Kikundi
Tenzi. Wakati mwingine sheria miundo virai huonyesha uhusiano wa
utawazi hivi kwamba nomino hutawala Kikundi Nomino (KN). Kwa mfano
sentensi kama; Amina ni mke wangu.
Suala la msingi
ambalo wanaumuundo walisisitiza ni kutazama na kuchunguza lugha
kisayansi. Hapa walisema kuwa masuala ilibidi yachunguzwe kwa uwazi
na kuonyesha vitu, kategoria na elementi kwa uwazi zaidi. Ilhali
sarufi geuzi hueleza ujuzi wa lugha ambao msemaji mzawa anao
unaomwezesha kutumia lugha. Huu ni ujuzi wa kutunga sentensi kwa njia
iliyo sahihi na vilevile namna sahihi ya kutamka na kueleza maana za
maneno na sentensi. Mfano mmilisi wa lugha ya Kizinza anaweza kutunga
sentensi zinazoeleweka na kutamka maneno ya lugha hiyo kwa usahihi
kabisa.
Kwa ujumla, sarufi
miundo virai na sarufi geuzi hufanana sana katika kuchunguza miundo
ya lugha husika japo katika utendaji wake hujitokeza baadhi ya
tofauti ambazo husababisha nadharia hizi za sarufi miundo
kutofautiana katika vipengele kadha wa kadha kama vile uchopekaji wa
viambajengo, maana zake pamoja na mfumo wa namna ya kuchanganua
sentensi.
MAREJELEO
Habwe, J. &
Karanja, P. (2004). Misingi
ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi:
Phoenix Publishers.
Habwe, J. &
Karanja, P. (2007).
Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi:
Phoenix Publishers.
Kihore, Y.M. na
wenzake. (2008). Sarufi
Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA). Sekondari na Vyuo.
Dar es Salaam: TUKI.
Massamba, D.P.B na
Wenzake (1999). Sarufi
Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA); Sekondari na Vyuo.
Dar es Saalam: TUKI.
Matinde, R.S.
(2012). Dafina
ya Lugha, Isimu na Nadharia; Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo
Vikuu.
Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD.
Saluhaya, M.C.
(2010).
Nadharia ya Lugha Kidato cha Tano na Sita.
Dar es Salaam: CHILDREN EDUCATION SOCIETY (CHESO).
No comments:
Post a Comment