Tuesday, July 5, 2016

Ulinganishaji wa kitabu cha 'natala' na kile cha 'siku njema'


Maana ya riwaya
Wamitila (2003) anafafanua riwaya kuwa ni kazi ya fasihi andishi ambayo kwa kawaida ni ndefu kuliko hadithi fupi. Urefu wa riwaya maana yake ni kwamba msuko wa simulizi umejengeka vizuri, kuna wahusika wengi, unaenea muda mrefu, na mada zake ni nzito na pana kiasi.
Muhando na Balisidya (1976) wanaeleza kuwa riwaya ni kazi ya kubuni kama hadithi ambayo hutungwa na kuibua mambo mengi katika mazingira wanayoishi watu.
Maana ya Tamthiliya
Tamthiliya ni utanzu ambao hutegemea mazungumzo na uigizaji ili kuwasilisha ujumbe wake. Huu ni utanzu ambao huandikwa kwa mtindo wa mazungumzo ya wahusika, (Wamitila, 2007).
Tamthiliya ni mchezo wa kuigiza au utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo
Muhtasari wa Riwaya ya “Siku Njema.”
Siku njema ni riwaya ya kitawasifu inazungumzia maisha ya Msifuni Kombo (Kongowe Mswahili) iliyoandikwa na mwandishi Ken Walibora mnamo mwaka 1996. Riwaya hii imejikita katika kuzungumzia mambo yanayoendelea katika jamii zetu za Kiswahili kama vile changamoto za magonjwa, ndoa na familiya pamoja na malezi ya watoto. Mwandishi kamtumia mhusika mkuu Msifuni Kombo maarufu kama Kongowea Msawahili kuonesha namna alivyopitia changamoto mbalimbali zikiwemo kufiwa na mama yake, kulelewa na mzazi mmoja (mama yake) baada ya mama kumkataa baba yake Kongowea aliyejulikana kwa jina la Juma Mukosi. Kongowea anapitia mateso mengi hata kutiliwa sumu kwenye chai na mkaza-mjomba (Mwanasaumu) ili afe.
Wasifu wa Prof. Ken Walibora
Ken Walibora alizaliwa Magharibi mwa Kenya na alisoma elimu ya msingi katika shule ya St. Joseph iliyoko wa mji wa Kitale. Alihitimu elimu ya kidato cha nne katika shule ya upili ya Olkejuado, mjini Kajiado. Na alihitimu mtihani wa kidato cha sita katika shule ya upili ya Koelel, mjini Gilgil. Walibora baadae alisomea masuala ya Maendeleo ya Jamii katika Taasisi ya Utawala, Kenya (KIA). Alihitimu shahada ya kwanza katika fasihi na Kiswahili katika chuo kikuu cha Nairobi. Prof. Walibora ni msomi mwenye PhD aliyoipatia nchini Kenya katika Chuo kikuu cha Ohio State nchini Amerika. Riwaya yake ya kwanza kuandika ni “Siku Njema” iliyochapishwa mwaka 1996 na amekwisha andika zaidi ya vitabu arobaini baada ya riwaya hiyo.
Ufafanuzi wa vipengele vya ulinganishaji katika riwaya ya “Siku njema”
Vipengele tulivyochunguza ni plot (muundo), mandhari, wahusika na migogoro. Vipengele hivyo vimefafanuliwa kwa kina kama ifuatavyo:
Ploti (muundo); ni namna matukio katika kazi ya fasihi yalivyopangwa na kuleta mtiririko wa kazi husika ya fasihi (Senkoro, 2011). Katika riwaya ya “Siku njema” iliyoandikwa na Ken Walibora, mwandishi amejenga visa na matukio katika mtiririko unaoeleweka kwa urahisi kwa msomaji. Kwa hiyo ni dhahiri kusema kuwa mwandishi wa riwaya hii ametumia muundo wa msago (muundo wa moja kwa moja) ambapo ameonesha mtiririko ufuatao:
Katika sura ya kwanza; ameonesha historia na asili ya Zainabu Makame ambayo imejengeka kupitia familiya ya Mzee Makame iliyoishi mjini Mwanza kabla ya mzee Makame kufariki.
Sura ya pili; Bibi yake Kongowea amerudi Tanga na Zainabu anajiunga na kikundi cha Mbelewele taarabu na kupata umaarufu kutokana na sauti yake nzuri katika uimbaji.
Katika sura hii pia kuzaliwa kwa Msifuni Kombo (Kongowea mswahili) kunadhihirika. Pia katika sura hii inaonesha Zainabu Makame anaanza kuugua.
Sura ya tatu; mwandishi anaonesha Zainabu akiaga dunia baada ya kuugua muda mrefu na kukosa tiba ya maradhi yaliyomsumbua. Lakini mama huyu anafariki bila kumuonesha mwanae baba yake.
Sura ya nne na kuendelea inadokeza changamoto alizopitia Kongowea hasa baada ya kwenda kuishi kwa mkaza-mjomba wake (Mwanasaumu).
Katika sura ya tano na kuendelea mwandishi ameonesha harakati za Kongowea kumtafuta baba yake na hatimaye anafanikiwa kukutana naye kama mwandishi anavyoonesha kuanzia mwishoni mwa sura ya kumi na tatu mpaka kumi na nne.
Baada ya Kongowea kukutana na baba yake aliyejulikana kwa jina la Juma Mukosi, baba huyo anafariki kabla ya mwanaye kumtambua na kuacha wosia unaomuongoza mwanae kutambua mali alizotakiwa kuzirithi kutoka kwa baba yake. Baada ya kuupata wosia ule maisha ya Kongowea yanabadilika baada ya mahangaiko ya muda mrefu tangu kuzaliwa kwake.
Mandhari; huwa ni mahali hususani jinsi panavyoonekana katika hali halisi ya maisha (Williady, 2015). Mtunzi anaweza kutumia mandhari kuelezea mazingira halisi ya kisa anachosimulia. Pia mtunzi huweza kusawili mazingira mbalimbali akiyasawiri matukio tofautitofauti ikiwa ni mbinu mojawapo ya kufikisha ujumbe wake kwa jamii husika. Hivyo mandhari humsaidia msomaji kung’amua ujumbe akirejelea tukio husika.
Mwandishi Ken Walibora katika riwaya hii ameweza kujenga visa na matukio katika mazingira halisi (mandhari halisi). Mandhari aliyotumia imejumuisha maeneo ya nchi mbili za Afrika ya Mashariki ambazo ni Tanzania akirejelea maeneno ya Mwanza- huku ndipo alipozaliwa Zainabu Makame mnamo mwaka 1927 (uk.15), Chongoleani- mkoani Tanga ambako walizaliwa babu na bibi zake Zainabu (uk.2), Tabora-mahali pa makazi ya Enock Minja mpwa wa Mwanasaumu (uk.23), Hospitalini (Holelaholela) ni pale alipopelekwa Bi. Rahma kwa ajili ya matibabu (uk.28), Arusha ni sehemu Vumilia alikuwa anasoma (uk. 45), Buguruni-Dar es Salaam-mahali alipokuwa anafanya kazi mama yake Alicia (uk.109). Nchini Kenya mwandishi amerejelea maeneo ya Mombasa- mahali alipokuwa anakaa Salimu ambaye ni mjomba wake Kongowea (uk.18), pia ni sehemu ambapo Enock Minja alifikwa na mauti baada ya kupata ajali ya gari, vilevile ndiko alikohamia baba yake Kongowea katika ule mji wa Kitale (uk.33).
Wahusika; ni viumbe hai au viumbe visivyo hai ambavyo hubebeshwa majukumu na msanii ili kuifikishia hadhira ujumbe uliokusudiwa na mwandishi (Williady, 2015). Mwandishi Ken Walibora katika riwaya ya “Siku Njema” amadhihirisha wahusika ambao tunaweza kuwaweka katika makundi matatu kutokana na hadhi ya uhusika wao, makundi hayo ni wahusika wakuu, wahusika wasaidizi na wahusika wajenzi kama yalivyofafanuliwa hapa chini:
  • Mhusika mkuu; katika riwaya hii mhusika mkuu ni Msifuni Kombo maarufu kwa jina la Kongowea Mswahili kwani ndiye aliyebeba dhamira kuu ambayo ni familia na malezi akiwa kama mtoto aliyekosa malezi ya baba na kulelewa na mama, lakini mama yake naye anafariki na kulelew na mjomba. Pia mhusika huyu ndiye alidhihirisha mantiki ya tawasifu katika riwaya hii kwani mtiririko wake unadokeza historia yake toka kuzaliwa mpaka kufiwa na wazazi wote wawili.
  • Wahusika wajenzi; hawa huwa ni wahusika wanaoibuliwa na mwandishi ili kujenga dhamira na baadae hutoweka. Katika riwaya hii wahusika wajenzi ni pamoja na Bi. Mack Donald ambaye ameibua dhamira ya upendo baada ya kumsaidia Kongowea katika mkahawa; Enock Minja ambaye ameibua dhamira ya dhuluma ya urithi na tamaa ya mali baada ya kukubali kujifanya mtoto wa Juma Mukosi ili akarithi mali na matokeo yake anafariki kwa ajali ya gari kabla hajafika kwa Juma Mukosi.
  • Wahusika wasaidizi; hawa ni wahusika ambao humsaidia mhusika mkuu katika ujengaji wa dhamira. Kwa mfano Ken Walibora amemtumia Bi. Zainabu Makame kama mama yake Kongowea Mswahili ili kuibua dhamira ya malezi ya watoto; Kitwana ametumiwa kama mjomba wake Kongowea anayemchukua na kuishi naye baada ya kufiwa na mama yake. Alikuwa mshauri mkuu wa Kongowea; Vumilia pia ni mhusika aliyeshiriki kama msaidizi kwani alichorwa kama rafiki yake Kongowea na baadaye akaja kuwa mke wake. Huyu ndiye aliyemdokeza Kongowea kuwa kuna mpango wa kutiliwa sumu kwenye ili afe uliopangwa na mkaza-mjomba wake.
Mgogoro; ni hali ya kutoelewana baina ya pande mbili yaani mtu na mtu, mtu na kundi, mtu mwenyewe na nafsi yake. Mgogoro ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi ya fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika na familia zao, au matabaka yao. Pia migogoro inaweza kugawanyika katika vipengele vikuu viwili ambavyo ni mgogoro wa nafsia na mgogoro wa mtu na mtu au kundi kama ilivyodhihirishwa na Ken Walibora katika riwaya ya “Siku Njema”.
  • Mgogoro wa Nafsia; ni aina ya mgogoro unaotokea baina ya mtu na akili au nafsi yake mwenyewe pale anapojikuta katika wakati mgumu kutokana na jambo fulani na asijue nini cha kufanya.
Mgogoro huu umedhihirika kwa Kongowea baada ya kifo cha mama yake akibaki hajui ni namna gani atampata baba yake. Suluhisho la mgogoro huu pale alipoambiwa na Bi. Rahma baba yake aliko;
pia mgogoro wa aina hii unadhihirika kwa Juma Mukosi maarufu kwa jina la Kazikwisha baada ya kukataliwa na Zainabu hali hii ilimpelekea kuacha kazi. Suluhisho la mgogoro huu ni yeye kuamua kuishi maisha ya ukiwa mpaka siku yake ya mwisho (uk.132)… Baada ya zawadi kunikata maisha yalikosa maana na kazumu kuishi maisha ya ukiwa mpaka siku yangu ya mauko. Nikaacha kazi na kughunia huku makutano kwa ngozi baada ya kununua shamba hili…. Kuishi ukiwa ndiko kumekuwa faraja yangu.
  • Migogoro kati ya mtu na mtu; ni migogoro inayotokea baina ya mtu na mtu au mtu na kikundi au hata familia. Migogoro ya aina hii imejitokeza kati ya wahusika wafuatao;
Mwanasaumu na Kongowea (uk.20-25)
Chanzo cha mgogoro baina ya wahusika hawa ni kufaulu kwa Kongowea katika mtihani wa darasa la saba huku watoto wa Mwanasaumu wakiwa hawajiwezi kimasomo, hivyo hakupenda Kongowea afaulu hali iliyopeleka chuki mpaka akamtilia sumu kwenye chai ili afe. Suluhisho la mgogoro huu ilikuwa Kongowea kuondoka kwa Mkaza-mjomba na kwenda kumtafuta baba yake Kenya.
Kongowea na Selemani Mapunda (uk.21)
Chanzo cha mgogoro huu ni baada ya Selemani Mapunda kubaini kuwa Kongowea ndiye aliyepeleka taarifa polisi kuwa Selemani na wenzake aliwashuhudia wakimpiga Hedimasta. Suluhisho la mgogoro huu ni Selemani Mapunda na Bakari kuuawa (uk.131).
Alice na mama yake (Bi. Mack Donald)
Chanzo cha mgogogoro huu ni mama Alicia kumsaidia Kongowea Mswahili baada ya kumkuta mgonjwa katika mkahawa ulioitwa Saidia Khala, Alice alikasirishwa na kitendo hicho cha mama yake. Alice anasema “…mama huyu mtu unampeleka wapi, akamuuliza bintiye. ‘Shut up’ alifoka mama mtu” (uk.107). Suluhisho la mgogoro huu ni pale tu Alicia anapokuja kutambua kuwa Kongowea ni mahiri wa mashairi na kujikuta wanakuwa marafiki.
Muhtasari wa Tamthiliya ya “Natala”
Tamthilia ya “Natala” ni tamthiliya iliyoandikwa na Profesa Kithaka Wa Mberia mwaka 1997 ambayo imemulika baadhi ya masuala ya kijamii yanayoleta mabishano makubwa. Baadhi ya masuala hayo ni pamoja na kuoza kwa mfumo wa uadilifu na utamaduni unaozivuta jamii nyuma kama vile kurithi wajane na ukatili kwa wanawake (udhalilishaji wa kijinsia) ambao msanii kauchora kupitia mhudumu wa jengo la ufuo kumtaka Natala kimapenzi kwa nguvu wakati amefuata mwili wa marehemu mumewe baada ya kudhaniwa kuwa amefariki kwa ajali ya gari.


Wasifu wa Prof. Kithaka Wa Mberia
Kithaka Wa Mberia alizaliwa mwaka 1955 nchini Keya. Ni mshairi mbunifu wa mashairi huru (mashairi ya kisasa). Amewahi kuchapisha vitabu vinne vya ushairi ambavyo ni Mchezo wa Karata (1997), Bara Jingine (2001), Redio na Mwezi (2005) na Msimu wa Tisa (2007). Maashairi yake yamekuwa mashairi ya kwanza ya Kiswahili kuigizwa katika tamsha la maonesho la kitaifa nchini Kenya mwaka 1988. Wa Mberia pia ni mtaaluma na mwandishi wa tamthiliya. Ni prof. wa lugha katika chuo kikuu cha Nairobi. Ameandika tamthiliya tatu ambapo mojawapo imefanikiwa kurushwa katika runinga nchini Kenya.
Ufafanuzi wa vipengele vya ulinganishaji katika tamthiliya ya “Natala”
Ploti (muundo); kama tulivyoona katika maelezo ya awali, ploti ni namna matukio katika kazi ya fasihi yalivyopangwa na kuleta mtirirko wa kazi husika ya fasihi. Ni jinsi mwandishi alivyoipanga kazi yake (Senkoro, 2011). Mwandishi wa tamthiliya hii amejenga matukio yake katika mtiririko wa matukio kufuatana (muundo wa moja kwa moja) kama inavyodhihirika katika muhtasari ufuatao kuanzia onesho la kwanza hadi la mwisho (la tano):
Onyesho la Kwanza; linadokeza nyumbani kwa Natala akiendelea na shughuli zake. Baadaye Tila anaingia kuomba chumvi, na baadaye kuzua tafrani akidai chumvi aliyopewa ni kidogo.
Onyesho la Pili; linadokeza Chifu akileta taarifa za kufariki kwa Tango nyumbani kwa Natala. Vilevile mwandishi anaonesha Natala na Bala wakiigiza mambo yale waliyokumbana nayo kule kwenye jengo la ufuo baada ya kufuata mwili wa marehemu mochwari (jingo la ufuo).
Onyesho la tatu; mwandishi anaonesha mazishi ya Tango na vikwazo wanavyopambana navyo ndugu wa marehemukutoka kwa chifu ikiwa ni pamoja na kuomba rushwa ili wapate kibari cha kukusanyika kwa ajili ya maziko.
Onyesho la nne; linamuonesha Mama Lime akiwa anamshawishi Natala akubali kuolewa na Wakene lakini anakataa.
Onyesho la Tano; linamshuhudia Wakene akiwa nyumbani kwa Natala akimwambia juu ya suala la kumrithi akiwa kama mke wa marehemu kaka yake lakini Natala anapokataa Wakane anaamua kuchukua cheti cha shamba kwa nguvu. Natala anaamua kusimama kidete na kumzuia Wakene kitendo kilichopelekea wazozane Natala na Wakene. Mwisho katika onesho hili Tango aliyesadikika kuwa amefariki anarejea nyumbani na kukuta vurugu sebuleni kwake Natala na Wakene wakiwa wameshikana kuashiria kuna ugomvi. Wanapomuona wote wanaduwaa na kuishiwa nguvu, baadaye Natala anaamini kuwa Tango hakufa na anamsimulia mumewe yote yaliyokuwa yanamsibu pindi imesemekana amekufa na kuzikwa.
Mandhari; katika tamthiliya hii mandhari halisi imechorwa kama ifuatavyo; nyumbani- mahali ambapo walikuwa wakiishi Natala, Tango Mwina na watoto wao wawili ambao ni Bwanu na Alika; makaburini- ni mahali ambapo maziko ya mtu aliyezaniwa kuwa Tango yalifanyika; Gerezani- ni mahali alipofungwa Tango baada kukamatwa na polisi kwa kosa la uzururaji; mjini-hapa ndipo Tango alipokamatwa pamoja na watu wengine wakiwa wamelewa; mochwari (jengo la ufuo)-ndipo ilipokuwa imehifadhiwa maiti ya mtu aliyesadikika kuwa ni Tango Mwina.
Wahusika; mwandishi wa tamthiliya hii ameonesha wahusika ambao tumeweza kuwatenga katika makundi makuu matatu kutokana na uhusika wao kama inavyofafanuliwa hapa chini:
  • Mhusika mkuu; katika tamthiliya hii Natala ndiye mhusika mkuu kwani ndiye aliyebeba dhamira kuu ya ukombozi wa mwanamke kiutamaduni. Pia inatokana na ujasiri wake wa kuweza kupiga dhuluma yake na kupigana na wanaume waliotaka kuudhalilisha utu wake.
  • Wahusika wajenzi; hawa ni wahusika kama Kasisi-aliyeongoza mazishi kule makaburini; Chifu- huyu ni kiongozi anayependa rushwa hivyo anawakilisha viongozi wasiotenda haki kwa watu wao na hivyo anaibua dhamira kama rushwa na uongozi mbaya; mhudumu wa jengo la ufuo-amechorwa kama mtumishi asiyethamini utu wa mwanamke pale anapotaka kumbaka Natala.
  • Wahusika wasaidizi; mwandishi Kachora wahusika wanaomsaidia Natala katika kutimiza dhamira yake kuu baadhi yao ni Wakene- ambaye ni shemeji yake anayetaka kumdhulumu mali Natala baada ya kukataa kurithiwa; Mama Lime-aliyekuwa akimshawishi Natala akubali kuolewa na Wakene; Tango- amechorwa kama mume wa Natala na inaposemekana kuwa amefariki Natala anapangiwa kurithiwa na Wakene; Bwanu na Alika- ni watoto wa Natala na Tango Mwina. Wamemsaidia Natala kujenga dhamira ya malezi ya wototo; wahusika wengine wasaidizi ni pamoja na Bala, Mzee Balu na Tila ambaye ndiye mke halali wa Wakene.
Migogoro; Profesa Kithaka Wa Mberia katika tamthiliya hii ya “Natala” pia ameonesha migogoro amabayo tumeijadili katika makundi makuu mawili yani mgogoro wa nafsia na migogoro ya mtu na mtu au kikundi:
  • Mgogoro wa nafsi
Mgogoro huu unamkumba Natala baada ya kupata taarifa kuwa mumewe Tango amefariki na kuanza kuwaza/kufikiri jinsi atakavyoweza kuwalea watoto peke yake akawa analalamika moyoni akisema;
Dhiki gani hii? Kwanini ninyang’anywe mume? Msiba juu ya msiba! Majonzi juu ya majonzi…” (uk.9). Suluhisho la mgogoro huu ni Tango kurejea nyumbani na wote kujua Tango bado yu hai.
  • Mgogoro wa mtu na mtu
Natala na Wakene
Mgogoro huu ulitokana na Wakene kutaka kumrithi mke wa kaka yake ambaye ni Natala ili achukue mali zote pamoja na shamba. Natala anapokataa ndipo wanapoanza kunyang’nayana cheti cha shamba (uk.53-55) wanabishana wakisema;
Natala: kilete cheti!
Wakene: Nitakutwanga!
Natala: niguse uone! Tia mkono motoni.
Mama Lime: Wakene mtie adabu huyo mwanamke!”
suluhisho la mgogoro huu ni Tango kurejea nyumbani.
Natala na mhudumu wa jengo la ufuo (mochwari)
Mgogoro huu unatokea pale mhudumu anapomtaka kimapenzi Natala ili aweze kumpa maiti ya mume wake. Natala alipokataa akataka kumbaka na ndipo ugomvi ulipoanza na wawili hao kusukumana hali iliyopelekea mhudumu kuangushwa chini. Ukurasa wa (16-23) Natala akiigiza na Bala wanasema;
Natala: Haja yangu ni kuchukua maiti. Si kuona ofisi.
Bala: Kuona ofisi ni kuchukua maiti.
Natala: Yaani iko ofsini?”
Suluhisho la mgogoro huu ni zamu ya mhudumu yule kuisha na kuingia mhudumu mwingine aliyewapa maiti bila kuwadai chochote
Natala na Chifu
Mgogoro unatokana na kitendo cha Chifu kuzuia mazishi ya mwili wa mtu aliyesemekana kuwa Tango Mwina mumewe Natala akidai hawana kibari cha kuzika la sivyo watoe pesa (uk.30-35) chifu anasema;
Chifu: Mnafanya nini? Hamkumupata ujumbe wangu? Nilisema maiti isizikwe mpaka nifike… Mbona mnaidharau serikali namna hii?...
Natala: Tuliupata
Chifu: …kisha ikawaje?
Natala: Baada ya kukungoja kwa kitambo kirefu tulionelea tuendelee na mazishi.” Suluhisho la mgogoro huu lilipatikana baada ya mzee Palipali kuzungumza na chifu na kuahidi watamuona wakimaliza maziko.
Kwa ujumla Prof. Ken Walibora na Prof. Wa Mberia wameweza kuyatazama mambo kiyakinifu ikiwa na maana kuwa wanayazungumzia matatizo ya jamii za Afrika ya mashariki kama yalivyo bila kutumia mbinu ya kuficha. Wote kwa ujumla wameweza kuibua na kero zinazozikumba familia nyingi za kiafrika ikiwa ni sambamba na mila na tamaduni kandamizi kwa mwanamke mfano urithi wa mjane na mali zake.


MAREJELEO
Muhando, P na Balisidya, N. (1976). Fasihi na Sanaa za Maonesho. Dar es Salaam: T.P.H
Senkoro, F.E.M.K. (2011). Fasihi; Mfululizo wa lugha na Fasihi. Dar es Salaam: KAUTTU
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi; Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus publication limited.
Kitabu cha NATALA na kitabu cha SIKU NJEMA































No comments:

Post a Comment

hakiki na tuma maoni au mapendekezo kuhusu makala hii ya andiko langu la uchunguandiko langu

ANDIKO LA UCHUNGU (Kwa shemeji zangu na wanangu)           NYAMBUYA OGUCHU,                            S.L.P 777666,       ...