Maana
ya fasihi simulizi
Fasihi
simulizi ni sanaa ya matumizi ya lugha ya kubuni inayosambazwa kwa
mdomo kwa njia ya kuimbwa, kughaniwa, kuigizwa, kusimuliwa, kuumbwa,
kufumba au kutegeana mafumbo na vitendawili (Syambo na Mazrui,
1992:2) katika King’ei na Kisozi, (2005:7).
Mulokozi,
(1996:24) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni fasihi iliyotungwa au
kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na
vitendo bila kutumia maandishi. Ni tukio linalofungamana na muktadha
(mazingira) fulani wa kijamii au wa kutawaliwa na mwingiliano wa
mambo kadhaa wa kadhaa kama vile, fanani, hadhira, fani, na maudhui
yaliyokisudiwa na mwasilishaji.
TUKI,
(2004) fasihi simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na
kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama
vile, hadithi, ngoma na vitendawili. Aidha, fasihi simulizi ni ile
ambayo inapitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kupitia neno la
mdomo (Ngure, 2003:1).
Kwa
ujumla, tunaweza kusema kuwa fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa na
kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo ambapo kuna uambatanishaji
wa utendaji katika uwasilishaji huo. Fanani na hadhira huonana ana
kwa ana jambo ambalo huwafanya hadhira kushiriki katika baadhi ya
utendaji. Kwa mfano, kuimba, kucheza, au kupiga makofi na vigelegele.
Tanzu
za fasihi simulizi
Wamitila,
(2003) anadai kuwa tanzu ni istilahi inayotumika kuelezea au
kurejelea aina za kazi mbalimbali za kifasihi.
Hivyo
basi, kutokana na maana ya tanzu iliyotolewa na Wamitila, (2003)
tunaweza kusema kuwa tanzu ni istilahi ya kifasihi inayotumika
kumaanisha matawi au mafungu katika kazi za fasihi. Tanzu za fasihi
simulizi zimeainishwa kwa namna tofauti tofauti kwa mujibu wa
wataalamu mbalimbali kama ifuatavvyo:
Wamitila,
(2008) katika uainishaji wake wa fasihi simulizi anazigawa tanzu za
fasihi simulizi katika makundi yafuatayo:
Simulizi au
hadithi;
huu ni utngo wenye visa vya kubuni au halisi unaowasilishwa kwa lugha
ya nathari kwa kusudi la kuburudisha, kukuza maadili na kuunganisha
jamii. Katika usimuliaji wa hadithi fanani huwa mfaraguzi ili
asiwachoshe watazamaji wake kwa kuingiza utendaji unaowashirikisha
watazamaji wake.
Maigizo;
ni sanaa inayotumia utendaji kuiga tabia au matendo ya watu wengine
au viumbe wengine ili kuburudisha au kutoa ujumbe kwa jamii. Maigizo
ni sanaa inayopatikana katika makabila mengi ya kiafrika na
huambatana na utambaji wa ngoma. Kwa mfano, jando na unyago,
malumabno ya watani na vichekesho.
Ushairi (nyimbo);
ni sanaa ya uimbaji inayoambatana na mdundo wa ngoma au mziki ili
kufikisha ujumbe kwa hadhira. Katika fasihi simulizi nyimbo
huambatana na mdundo wa ngoma na mara nyingi nyimbo hizi huwa na
mkutdha kulingana na ujumbe uliolengwa. Hivyo basi, tunapata nyimbo
za ndoa/arusi, jando/tohara, hodiya, kimai, nyimbo za mazishi, nyimbo
za kidini, nyimbo za kizalendo na nyimbo na mapenzi.
Semi;
ni mafungu ya maneno ambayo hutumiwa kuleta maana nyingine badala ya
maneno halisi ya maneno yaliyotumika. Katika fasihi ya Kiswahili semi
hujumuisha nahau, misemo na methali. Kwa mfano, tukisema mtu amegonga
mwamba hatumanishi kwamba amepiga jiwe kubwa kwa mkono au kwa kifaa
chochote, bali tunamanisha kwamba ameshindwa kuendelea katika jambo
fulani.
Mazrui
& Syambo, (1992) wanasema kuwa fasihi simulizi ina tanzu zake
ambazo ni tofauti na zile za fasihi andishi ingawa kuna baadhi
amabazo zinafanana na zile za fasihi andishi. Fasihi simulizi ina
tanzu kuu nne ambazo tunaziainisha kama ifuatavyo:
Ngano au hadithi;
ni tungo yoyote ya kubuni inayosimuliwa kwa lugha ya nathari. Katika
fasihi ya Kiswahili ngano ni za aina nyingi lakini zote huanza kwa
njia inayofuata mtindo huu:
Msimulizi
: Paukwa!
Msikilizaji
: Pakawa!
Msimulizi
: hapo zamani za kale palitokea…
Nyimbo au
mashairi;
kuna nyimbo za aina nyingi katika fasihi ya Kiswahili lakini
zinazokusudiwa hapa ni zile zilizotungwa kwa mdomo (bila maandishi)
na kusambazwa kwa mdomo. Nyimbo za aina hii zimeenea katika maisha ya
Kiswahili na huwafata tangu wanapozaliwa mpaka kufa kwao. Nyimbo hizi
kwa kawaida huwa zinafungamana na ngoma au michezo fulani na mara
nyingine huimbwa pamoja na mziki kwa mfano, nyimbo za sherehe, nyimbo
za watoto, nyimbo za taarabu na bembezi.
Methali;
hii ni misemo mifupi yenye hekima fulani ndani yake. Methali
hudhihirisha mkusanyiko wa mafunzo waliopata watu wa vizazi vingi vya
jumuia fulani katika maisha yao. Methali hutumiwa sana katika
mazungumzo ya kawaida ya waswahili na ni sehemu moja muhimu katika
fasihi simulizi ya Kiswahili. Methali nyingi za Kiswahili huwa na
mdundo maalumu wa kishairi na mara nyingine huwa na vina.
Vitendawili;
ni tungo fupi ambazo huwa na swali fupi lisili wasi na jibu kwa
makusudi ya kupima ufahamu wa hadhira kuhusu mazingira yake. Anayetoa
kitendawili huuliza swali lake kwa kutoa maelezo mafupi yanayorejelea
umbo la kitu hicho, sauti harufu au kukifananisha na kitu kingine.
Anayejibu huhitaji kufkiria haraka na kutoa jawabu ambalo huwa na
neno moja au maneno mawili hivi. Vitendawili huwa na mianzo maalumu
kulingana na jamii yake. Katika fasihi simulizi vitendawili huwalenga
watoto ili kuchochea fikra na kuwazoeaza mazingira yanayowazunguka.
Mulokozi
katika makala yake ya tanzu za fasihi simulizi iliyo katika jarida la
Mulika Na 21 (1989) amezigawa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kwa
kutumia vigezo viwili ambavyo ni:
Umbile
na tabia ya kazi inayohusika; katika kigezo hiki, Mulokozi
ameangalia vipengele vya ndani vinavyounda sanaa hiyo na kuipa
mwelekeo au mwenendo. Baadhi ya vipengele hivyo vya ndani ni namna
lugha inavyotumika kishairi, kinathari, kimafumbo, kiwingo au
kughani, muundo wa fani hiyo na wahusika.
Muktadha;
ambapo amezingatia kuwa fasihi simulizi ni tukio, hivyo huambatana
na mwingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha, watu na mahali.
Mwingiliano huu ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio unaoamua
fani fulani ya fasihi simulizi ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi
kwa hadhira kwenye wakati na mahali hapo. Hivyo hadithi inaweza
kugeuzwa wimbo, utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo unaweza
kugeuzwa ghani au usemi kutegemea muktadha unaohusika. Kwa hiyo,
Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kama
ifuatavyo:
Masimulizi;
hii ni tanzu ya fasihi simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika
kugawa utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha
ambapo lugha iliyotumika katika masimulizi ni ya kinathari. Pia
kigezo cha muundo kimetumika mara nyingi masimulizi huwa na muundo
unaojitofautisha na tanzu nyingine kama vile ushairi. Mara nyingi
katika masimulizi muundo wake huwa ni wa moja kwa moja yaani
mtiririko wa visa na matukio. Vile vile kigezo kingine ni cha
wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusishwa wahusika wa pande mbili
ambao ni mtendaji na watendwaji. Kigezo kingine ni kigezo cha namna
ya uwasilishwaji. Katika uwasilishwaji, huwasilishwa na msimuliaji
mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni mandhari ambayo huwa ni maalumu
kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika
katika muda maalumu, kwa mfano baada ya kazi. Masimulizi yamegawnyika
katika tanzu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu
za kisa huwa (kihistoria).
Utanzu wa semi;
semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au
mafunzo. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya
mkato na kigezo kingine ni cha kidhima ambacho hufunza. Utanzu huu
umegawanyika katika vipera vifuatavyo: methali, vitendawili, misimu,
mafumbo na lakabu.
Ushairi;
huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia
ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo
vinavyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha
ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika
ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji wa ughani.
Vipera vya utanzu huu ni nyimbo na maghani.
Utanzu wa
mazungumzo;
mazungumzo ni maongezi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida
juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi, ili
mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii fulani. Vigezo
vinavyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo
lugha inayotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha
kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayolojia. Vipera vya utanzu
huu ni hotuba, soga, mawaidha, malumbano ya watani na ulumbi.
Maigizo;
ni michezo ambayo hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu
au viumbe wengine ili kuburudisha na hutoa ujumbe fulani kwa hadhira.
Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya
uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu na
wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha,
kuelimisha au kuonya. Pia kinatumika kigezo cha mandhari ambapo
maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya
sherehe fulani na katika matukio ya kijamii.
Ngomezi;
ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo
vinavyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kidhima ambapo dhima
yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Kwa mfano, taarifa hiyo
yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.
Vile
vile Okpewho, (1992) amazigawa tanzu za fasihi simulizi kwa
kuzingatia vigezo vinne kama ifuatavyo:
Kigezo
cha unguli; katika kigezo hiki kuna jitokeza ngano zosozohusu
wanadamu. Kuna ngano za wanyama, ngano za vichimbakazi na ngano za
miungo. Hata hivyo kigezo hiki kinaonekana kuwa na matatizo kadha wa
kadha kama vile kufanana kitabia kati ya jamii moja na nyingine,
kupuuza namna mbalimbali katika ngano ambazo vichimbakazi, wanadamu
na wanyama huhusiana.
Kigezo
cha lengo la ngano husika; katika kigezo hiki ngano zinaainishwa kwa
kuzingatia lengo la simulizi husika. Hapa panajitokeza ngano za
kimaadili, ngano za kuhimiza kazi na zinginenzo.
Kigezo
cha sifa ya ubora wa ngano; ni kigezo ambacho ndicho kinaonekana
kubeba kundi kubwa la ngano. Katika kigezo hiki kuna ngano ayari
(ambazo huambatana na uelevu au ulaghai wa wahusika) ngano za
mtanziko kama vile zinazohusu vita , vizazi, mashujaa na zinginezo.
Kigezo
cha muktadha au utendaji wa ngano husika; katika kigezo hiki
kinachoangaliwa ni ngano inatendwa wakati gani na katika mazingira
gani. Kwa mfano, kwa kutumia kigezo hiki tunaweza kupata ngano za
mbalamwezi, ngano za ibada, ngano zinazotendwa wakati wa mapumziko
ya wawindaji na zinginezo.
Hivyo
basi, Okpewho, (1992) amezigawa tanzu za fasihi simulizi katika
makundi yafuatayo:
Nyimbo na
maghani;
ni sanaa ya kuwasilisha ujumbe kwa hadhira inayoambatana na mdundo wa
ngoma au mziki. Katika uimbaji fanani hutoa sauti inayoendana na
mapigo ya ngoma au mziki. Aghalabu nyimbo hizi huweza kuimbwa katika
tukio maalumu. Hivyo basi, tunaweza kuainisha nyimbo katika makundi
mablimbali kama vile bembezi, mbolezi, sifo na zinginezo.
Masimulizi;
ni visa vya kubuni au halisi vinavyowasilishwa kwa hadhira kwa
kutukia lugha ya nathari. Katika masimulizi fanani huwasilisha ujumbe
wake kwa njia ya kuisimulia hadhira yake kwa kutumia mbinu mbalimbali
zinazoambatana na utendaji.
Semi;
ni tungo fupi fupi zenye hekima na busara ndani yake. Mara nyingi
kinachozungumzwa ni tofauti na kilichokusudiwa. Wakati mwingine tungo
hizi hutumika ili kuipa adabu lugha ya mzungumzaji. Kwa mfano, Juma
ana mkono wa birika katika tungo hii tukifasili kuwa juma anamkono
unaofanana na wa birika tunapoteza maana ya tungo hiyo.
Ngonjera;
ni nyimbo ambazo huhusisha waimbaji zaidi ya mmoja, uimbaji wao huwa
katika mfumo wa majibizano. Aidha utanzu huu huweza kuitwa kuwa ni
ushairi wa maigizo maan huwa kuna jambo ambalo waimbaji hawa
hulumbana ingawa mwishoni hufika hitimisho kwa mmjo wao kukubaliana
na mawazo yaw engine.
Aidha,
Balisidya, (1987) anaigawa fasihi simulizi katika tanzu tatu kama
ifuatavyo:
Nathari;
katika nathari anatoa vipera kama vile ngano-istiara, harafa na
hekaya, tarihi-kumbukumbu, shajara, hadithi za kihistoria pamoja na
epiki, visaasili- kumbukumbu na tenzi.
Ushairi;
katika ushairi kuna vipera kama vile nyimbo-tahlili, bembea,
tumbuizo, ngoma, miviga, watoto na kwaya, maghani, majigambo,
vijighani, shajara, pamoja na tenzi.
Semi;
katika utanzu huu kuna vipera kama vitendawili, misimu, mafumbo,
methali-msemo na nahau, misimu-utani, masaguo na soga.
Tukiwaangalia
wataalamu hawa wanatofautina katika ugawaji wa tanzu za fasihi
simulizi jambo ambalo linaleta mkanganyo mkubwa sana kwa wagenzi na
wasomi wa fasihi simulizi. Hata hivyo mtazamao unaoelekea kuwa na
mshiko zaidi ni ule wa Mulokozi ambaye anazigawa tanzu za fasihi
simulizi katika aina sita ambazo ni masimulizi (hadithi), semi,
ushairi, mazungumzo ya kisanaa, maigizo na ngomezi.
Utata
katika uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi
Vigezo vya
uainishaji;
baadhi ya wataalamu wametumia vigezo vya uainishajia mbavyo
vinatofautina kati ya mwandishi mmoja na mwingine. Lakini pia
watalaamu weingine kama kama vile Wamitila, (2008), mazrui &
Syambo, (1992) hawajaonesha vigezo vyovyote vya uanishaji wa tanzu za
fasihi simulizi jambo ambalo linaleta utata katika uainishaji kwani
ni vigumu kubaini ni yupi uainishaji wake upo sahihi.
Utofauti wa Idadi
katika tanzu zinazoainishwa;
uainishaji wa tanzu hizi unatofautiana katika idadi wanazoainshisha
wataalamu mbalimbali. Kwa mfano, Mulokozi katika jarida la Mulika Na
21 (1989) anadai kuna tanzu sita (6), Balisidya, Matteru(1987)
anainisha tanzu tatu (3), Wamitila, (2008) na Okpewho, (1992)
wanaainisha tanzu nne (4) za fasihi simulizi. Hivyo kutofautina kwa
idadi za tanzu zinazoainishwa na watalaamu mbalimbali kunazua utata
kwani ni vigumu kuhitimisha kuwa ni nani yupo sahihi.
Kuingiliana kwa
tanzu;
katika uainishaji wa watalamu mbalimbali baadhi ya tanzu
zinaingiliana ingawa hutofautiana katika vigezo vya uainishaji wao na
wengine kukosa vigezo kabisa. Hivyo basi kuingiliana kwa tanzu hizo
huweza kuleta utata. Kwa mfano, Okpewho, (1992) ameainisha utanzu wa
ngojera ambao unaingia katika utanzu wa ushairi kama ilivyoainishwa
na Wamitila, (2008), Mulokozi, (1989). Lakini pia utanzu wa semi
umeonekana katika kila uainishaji ingawa kuna utofati unaojitokeza
katika uainishaji wao.
Utofauti wa
isitlahi za uainishaji;
baadhi ya wataalamu wametofautina katika isitilahi za uainishaji
ingawa hurejelea utanzu mmoja au dhana moja. Kwa mfano, Balisidya &
Matteru, (1987) anatumia istlahi nathari, Wamitila, (2008) ametumia
hadithi, Okpewho, (1992) na Mulokozi, (1989) ametumia istilahi
masimulizi. Tukichunguza istalahi hizo, tunapata dhana moja tu
inayorejelewa na kuleta utata katika uainishaji.
Tanzu za fasihi
simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui;
baadhi ya tanzu za fasihi na vipera vyake huweza kubadilika kulingana
na wakati. Kwa mfano utanzu wa hadithi katika kipindi cha sasa
huwasilishwa tofauti na ulivyowasilishwa zamani, hivyo basi hukosa
uhalithia wa hadithi kama utanzu wa fasihi simulizi kitendo ambacho
waainshaji hushindwa kutengeza kigezo cha kuainisha utanzu huu.
Hivyo basi,
tunahitimisha kwa kusema kuwa, fasihi simulizi kama fasihi zingine
ina dhima muhimu katika jamii. Dhima za fasihi simulizi ni kama vile
kuelimisha jamii, kufundisha jamii, kutabirii na kutoa mwelekeo wa
jamii, kuhifadhi historia ya jamii na kuonya jamii. Pia kupitia
fasihi simulizi wasimuliaji hukuza ubunifu wao kwa kutongoa
masimulizi au hadithi mbalimbali. Fasihi simulizi ni chanzo kikubwa
cha fasihi andishi kwani karibu vipengee au tanzu zote za fasihi
andishi zimetokana na fasihi simulizi. Kwa mfano, riwaya chanzo chake
ni hadithi, tamthiliya hutokana na sanaa za maonesho, semi mbalimbali
za fasihi simulizi hupatikana katika fasihi andishi. Utanzu wa
ushairi umetokana na ushairi simulizi ambao zamani ulikuwa
ukiwasilishwa kwa uimbaji au kughani fasihi simulizi hukuza upeo wa
kufikiri na ubunifu kwa hadhira kupitia elimu inayopatikana kupitia
masimulizi mbalimbali.
MAREJELEO
Balisidya,
M. L (1987). Tanzu
na Fasihi Simulizi Katika Mulika Nambari 19.
Dar es salaam:
TUKI
Kirumbi,
P. S (1975). Misingi
ya Fasihi Simulizi.
Nairobi: Shungwaya Publishers Ltd
Mazrui,
A & Syambo, B (1992).
Uchambuzi wa Fasihi.
Nairobi: East African Educational
Publishers.
Masebo,
J. A & Nyangwine, N (2008). Nadharia
ya Fasihi.
Dar es salaa: Nyambari Nyangwine
Publishers.
Msokile,
M (1992). Kunga
za Fasihi na Lugha.
Dar es salaam: DUP
Mulokozi,
M. M (1989). Tanzu
za Fasihi Simulizi Katika Mulika 21.
Dar es salaam: TUKI
Mulokozi,
M. M (1996). Utangulizi
wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili.
Dar es salaam: TUKI
Ngure,
A (2003). Fasihi
Simulizi kwa Shule za Sekondari.
Nairobi: Phoenix Publishers Ltd
TUKI,
(2004). Kamusi
ya Kiswahili Sanifu (Toleo la pili).
East Africa:
Oxford University
Press na TUKI
Wamitila,
K. W (2003). Kamusi
ya Fasihi, Istilahi na Nadharia.
Nairobo: Focus Publication Ltd
Wamitila,
K. W (2008) Kanzi
ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi.
Nairobi: Vide-
Muwa Publishers Ltd.
Okpewho,
I (1992) African
Oral Literature. Backgrounds Character and Coninuity.
Bloomington: Indian
University Press.