Dhana
ya Sarufi
Sarufi
ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala lugha katika matumizi yake
ambayo hujumuisha matamshi, maumbo, miundo na maana (Saluhaya,
2010:72).
Massamba
na wenzake (1999) Sarufi ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala
kila moja kati ya viwango vinne vya lugha ambavyo ni umbo-sauti
(fonolojia),
umbo-neno (mofolojia),
miundo maneno (sintaksia)
na umbo maana (semantiki).
Matinde
(2012:211) Sarufi ni taaluma ya lugha inayochunguza na kuchanganua
vipashio na kanuni mbalimbali zinazotawala muundo wa lugha.
Massamba
(2004) anasema, sarufi ni taaluma ya lugha inayohusu uchunguzi na
uchanganuzi wa kanuni za vipengele mbalimbali vya lugha.
Kwa
ujumla sarufi inaweza kuelezwa kama kanuni, sheria na taratibu
zinazomuongoza mzungumzaji au mwandishi kuzungumza au kuandika tungo
sahihi zinzoeleweka kwa msikilizaji wa lugha ileile. Kama ni mzawa wa
lugha, mtumiaji huwa tayari anazo kanuni hizo (hata katika
uzungumzaji), yaani kanuni anakuwa nazo akilini baada ya kusomaau
kuishi na watu wa lugha hiyo.
Dhana
na historia ya sarufi mapokeo
Kwa
mujibu wa Massamba na wenzake (1999) wanaeleza kuwa, sarufi mapokeo
ni sarufi elekezi ikisisitiza usahihi wa lugha kwa kuonesha sheria
ambazo hazina budi kufuatwa, mathalani kufanya muundo fulani wa
sentensi usomeke kwa usahihi au sheria ambazo hazina budi kufuatwa
ili kufanya matamshi fulani yakubalike kuwa ndio sahihi.
Matinde
(2012:211) anaeleza kuwa, mkabala huu wa sarufi mapokeo ni mkabala wa
awali ulioshughulikia sarufi ya lugha. Waasisi wake walikuwa
wanafalsafa wa Ugiriki. Habwe na Karanja (2004:129) anataja
wanafalsafa hao kuwa ni Plato,
Aristotle, Dionysus Thrax, na Priscian.
Katika kipindi hiki sarufi ilishughulikiwa sambamba na falsafa, dini,
fasihi, balagha na mantiki. Plato alikuwa wa kwanza kugawa sentensi
katika sehemu kuu mbili mtenda (subject)
na kitendwa (object). Hatimaye Aristotle akaendeleza kazi ya mwalimu
wake kwa kugawa sentensi katika sehemu kuu tano ambazo pia ndizo aina
za maneno; nomino, kitenzi, kivumishi, kiunganishi na kielezi.
Miaka
ya 100 K.K, mwanasarufi Myunani Dionysus
Thrax
aliandika kitabu cha sarufi ambacho ni cha awali kabisa kilichoitwa
“Techne
Grammatike
(The
Art of Grammar)”.
Mwanasarufi huyu aliainisha sehemu saba za sentensi ambazo ni nomino,
kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kiunganishi, kielezi na kiingizi.
Dhana
ya Neno
Habwe
na Karanja (2007:71) wanafafanua kuwa, neno ni kipashio cha kiisimu
kinachoundwa na mofimu moja au zaidi.
Saluhaya
(2010:135) anadai kuwa, neno ni mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au
kuandikwa kwa pamoja na kuleta maana.
Massamba
na wenzake (1999:43) katika samikisa
wakitilia maanani maelezo ya Lyons
(1968:194-208), neno linaweza kufafanuliwa katika misingi ya
kiumbo-sauti (yaani,
kwa kuchunguza sauti zinazounda umbo zima),
kiothografia (yaani
kwa kuchunguza herufi zinazotumika katika kuliandika umbo hilo), na
kisarufi (yaani
kwa kuchunguza kile kinachowakilishwa na umbo husika katika lugha).
Hivyo
basi, tunaweza kufasili neno kama silabi au mkusanyiko wa silabi
(sauti) unaoandikwa au kutamkwa ili kuleta maana. Maana hiyo yaweza
kuwa kamili, yaani inayotoa taarifa kamili au isiwe kamili, yaani
ambayo haitoi taarifa kamili kwa msomaji au msikilizaji.
Dhana
ya Sentensi
Matinde
(2012:157) anafafanua sentensi kuwa ni neno au fungu la maneno lenye
uarifishaji mkamilifu. Sentensi huwa na muundo uliokamilika na
hujitegemea kimaana.
Kwa
ujumla sentensi ni kipashio kikuu katika tungo chenye uwezo wa kutoa
taarifa iliyo kamili au isiyo kamili na huwa na muundo wa kiima na
kiarifu.
Ufafanuzi
wa aina za maneno kwa mujibu wa wanasarufi wa kimapokeo
Wataalamu
wengi wa sarufi ya Kiswahili sanifu wanaelekea kukubaliana kwamba
katika lugha hii kuna aina za maneno zisizopungua saba. Aina hizi za
maneno zimewahi kujadiliwa kwa kina katika vitabu kadhaa vya sarufi
vinavyojishughulisha na sarufi miundo na sarufi maumbo. Baadhi ya
wataalamu wa sarufi mapokeo waliojadili aina hizo ni Kapinga (1983),
Nkwera, Tumi, Mohamed, Massamba na wenzake (1999) na Kihore na
wenzake (1999). Aina hizo ni pamoja na:
Nomino
Nomino
ni jina linalotaja kitu, kiumbe, hali, dhana au tendo lolote liwalo.
Tukiyachunguza kwa makini maelezo haya tunaona kwamba yanaashiria
kuwa katika uamilifu wake nomino hufanya kazi ya kukipambanua au
kukibainisha kitajwa kwa madhumuni ya kukitofautisha na vitajwa
vingine. Kwahiyo nomino si mtajwa tu bali pia ni mtajwa bainishi.
Katika
sarufi za kimapokeo, nomino zilijulikana kama majina lakini katika
sarufi za kisiku hizi neno jina au majina limeonekana kuwa la kawaida
mno na kwamba haliwezi kuwa na mashiko yenye kukidhi mahitajio ya
kiistilahi. Kwahiyo neno nomino limependekezwa litumike badala yake
(Massamba na wenzake, 1999:39 katika samikisa.
Wanasarufi mapokeo wameweka migawanyo ya nomino kama ifuatavyo:
a)
Nomino
jumuishi
-
hizi ni nomino zinazohusu majina ambayo hayakibainishi wazi kitu
kinachotajwa. Kwa mfano mbuzi, gari, chuo, mtu, kalamu na nyumba.
b)
Nomino
mahususi
– ni yale majina ambayo yanataja vitu, dhana, na viumbe fulani
maalumu na kwa kutoa ubainishi ambao ni wa wazi zaidi. Baadhi ya
nomino mahususi ni kama vile Masalu, Ijumaa, Februari, Mwanza,
Mariam, Herman, Viktoria, Tanzania na Rufiji.
c)
Nomino
kikundi –
hizi ni nimino ambazo huhusu majina yanayotaja vikundi kadhaa vya
viumbe. Katika nomino hizi, jina moja huwa linataja jumuiya yenye
sifa za namna moja. Kwa mfano baraza, jeshi, familia, shule, bunge,
genge, mahakama, kombania na kwaya.
d)
Nomino
dhahania
– ni nomino zinazohusu majina ya vitu, dhana, na viumbe ambavyo
kiukweli tunaweza kuviona katika akili tu lakini hatuwezi
kuvibainisha kwa macho. Kwa mfano Uchawi, uzee, malaika, mizimu,
Mungu ,usingizi na uchovu.
e)
Nomino
mguso –
ni nomino zinazohusu majina ya vitu ambavyo tunaweza kuviona kwa
macho na kuvitambua katika uyakinifu wake, na utambumbuzi huu huweza
kutokana na kuvigusa, kuvishika au kuvionja kama vile asali, chumvi,
kiti, tofali, na tonge.
f)
Nomino
za hesabu
– hili ni kundi la nomino ambalo hutumia kigezo cha uwezekano wa
kuhesabika katika uainishaji wake. Hapa tunatofautisha kati ya nomino
zinazowakilisha vitu vinavyohesabika na vile visivyohesabika. Nomino
za vitu vinavyohesabika ni kama vile watoto, vitu, visu, mifuko na
viatu. Nomino zisizohesabika hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi
na haviwezi kugawika, kwa mfano makamasi, mafuta, maji, matope,
sukari, mchanga, uji, na nywele.
Vitenzi.
Ni
aina ya neno linalotoa taarifa juu ya tendo linalofanyika au
linalotendwa na kiumbe au kitu. Wanasarufi mapokeo wamevigawa vitenzi
katika aina kuu tatu ambazo ni:
a)
Kitenzi
kikuu
– ni kitenzi ambacho kinaweza kujitokeza peke yake katika sentensi.
Mfano anakula, anampiga, tunacheza, wamechoka na anaimba.
b)
Kitenzi
kisaidizi
– ni kitenzi ambacho kinaandamana na kitenzi kikuu katika sentensi.
Kwa mfano alikuwa
analima, tunapenda
kusoma, na amechoka
kucheza.
Hivyo, maneno yaliyo katika hati mlazo ni vitenzi visaidizi.
c)
Kitenzi
kishirikishi
– ni kile cha umbo ni
na si
ambacho kinachukuliwa kuwa kinashirikisha vipashio vingine katika
sentensi. Kwa mfano Kahigi ni
mwalimu
bora, huyu msichana si
mwerevu.
Vuvumishi.
Ni
kipashio ambacho hutoa maelezo zaisi juu ya nomino au kiwakilishi
chake. Maelezo kama hayo kwa kawaida huwa namna au jinsi nomino
ilivyo, yaani inavyoonekana, inavyofikiriwa, tabia, au idadi yake.
Mfano wa vivumishi ni kama vile chafu, dogo, refu, vivu, zuri,
embamba, na fupi. Vivumishi vimeweza kugawanywa katika aina kuu
zifuatazo:
a)
Vivumishi
vya sifa
– ni vivumishi vinavyotaja tabia au namna vitu vilivyo au
vinavyoonekana. Kwa mfano ema, nyenyekevu, pole na katili.
b)
Vivumishi
vya idadi –
ni vivumishi vinavyoonesha jumla au hesabu ya vitu. Aina hii ya
vivumishi tunaweza kuigawa katika makundi mawili ambayo ni kundi
linaloonesha idadi kwa jumla na kundi linaloonesha idadi kwa hesabu.
Kwa mfano ingi, chache, haba na kidogo vilievile tano, tisini, elfu ,
milioni na tatu.
c)
Vivumishi
viulizi
– ni vivumishi vinavyouliza maswali kuhusiana na nomino
inayoandamana navyo. Mfano watu wangapi, miti mingapi, mayai mangapi,
watoto wangapi, na viti vingapi.
d)
Vivumishi
vya pekee
– ni maumbo enye
na enyewe
ambayo katika Kiswahili ndiyo tu huchanganya aina na viambishi vya
upatanisho wa kisarufi vinavyojitokeza navyo kimatumizi. Mfano m-tu
m-refu, m-ti mrefu, miti mirefu.
Viwakilishi.
Ni
aina mojawapo ya maneno katika sarufi ya lugha ambayo uamilifu wake
ni kuwakilisha nomino katika miktadha mbalimbali. Kwa mfano
viwakilishi nafsi, viwakilishi viashirii, viwakilishi viulizi,
viwakilishi vimikilishi, viwakilishi vya idadi na viwakilishi jumla.
Viunganishi.
Ni
neno linalotumika kuviweka pamoja vipashio mbalimbali ili kuvifanya
viwe kipashio kikuu kimoja. Kwa mfano na,
au,
wala,
na lakini
katika sentensi zifuatazo:
Baba
na Mama
wanalima.
Unapenda
chai au
uji.
Hana
huruma wala
upendo.
Wanasarufi
mapokeo wamevigawa viunganishi katika makundi makuu mawili kwa
kuzingatia msingi wa kimaana kama vile viunganishi vya hadhi sawa na
viunganishi vihusishi.
Vielezi.
Ni
neno linalotumika kuelezea zaidi juu ya kitenzi. Mfano sana, mno,
kabisa, polepole, harakaharaka, zaidi, sawasawa na barabara.
Wanasarufi mapokeo wameviainisha vielezi katika aina kuu mbili yaani
vielezi halisi na vielezi viingizi. Mfano wa vilelezi halisi ni kama
vile mno, sana, bure, hasa, kabisa, ovyo, haraka na sasa. Kwa upande
wa vielezi viingizi ni kama vile pu, mwa, na bwe .
Viingizi.
Ni
aina ya maneno inayodokeza hisia za msemaji kama vile ya hali yake ya
kufurahi, kushangaa, kushtuka, na uchungu. Haya ni maneno kama vile
Lo! Alaa! Lahaula! na Aa! Maneno kama haya kwa kawaida huwa
yanatumika kabla ya sentensi na aghalabu huwa hayana mfungamano wa
kisarufi na sentensi inayofuata. Aina hii ya neno pia huitwa
vihisishi. Jina vihisishi limekitwa zaidi katika misingi ya kimaana
yaani linahusu zaidi hisia mbalimbali zinazobebwa na maneno hayo.
Viingizi navyo vimegawanywa katika makundi mawili nayo ni viingizi
halisi na viingizi vya taswira.
Ufafanuzi
wa aina za sentensi kwa mujibu wa wanasarufi mapokeo.
Kwa
upande wa sentensi, wanasarufi
mapokeo wanaainisha
aina
tatu za sentensi kwa
kuzingatia uamilifu
wake.
Aina hizo ni kama zifuatazo:
i)
Sentensi
taarifa
– hizi ni sentensi zenye kutoa taarifa fulani.
Kwa
mfano: Kiranja amechelewa kufika shuleni.
Kahigi
kaandika kitabu cha sarufi ya Kiswahili.
ii)
Sentensi
ulizi
– aina hii ya sentensi huwa ina pengo katika sehemu yake ya
taarifa. Sentensi hizi hutaka kupata taarifa fulani.
Kwa
mfano: Adam ameweza kucheza mpira?
Kalamu
yako ni ipi?
iii)
Sentensi
Agizi
– aina hii ya sentensi humuingiza msikilizaji kutenda kitendo
fulani. Aghalabu sentensi ya aina hii haina sehemu ya kiima.
Kwa
mfano: Toka nyuma uende mbele.
Mwite
kiranja wako.
Kwa
ujumla, wanasarufi mapokeo kwa kiasi fulani wanatofautiana katika
uainishaji wa aina za maneno kwani kuna wengine wametaja aina kumi za
maneno badala ya saba. Kwa mfano Habwe na Karanja (2004:130-139) wao
wanaainisha aina kumi za maneno ambazo ni nomino, vitenzi,
viwakilishi, vivumishi, vielezi, vihusishi, viunganishi, vionyeshi,
vihisishi na vibainishi. Hivyo ni vigumu kutambua idadi halisi ya
aina za maneno kwa mujibu wa sarufi mapokeo.
MAREJELEO.
Habwe,
J. & Karanja, P. (2004). Misingi
ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi:
Phoenix Publishers.
Habwe,
J. & Karanja, P. (2007).
Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi:
Phoenix Publishers.
Kapinga,
M.C. (1983). Sarufi
Maumbo ya Kiswahili Sanifu.
Dar es Saalam: TUKI.
Massamba,
D.P.B na Wenzake (1999). Sarufi
Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA); Sekondari na Vyuo.
Dar es Saalam: TUKI.
Matinde,
R.S. (2012). Dafina
ya Lugha, Isimu na Nadharia; Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo
Vikuu.
Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD.