Maana
ya riwaya
Wamitila
(2003) anafafanua riwaya kuwa ni kazi ya fasihi andishi ambayo kwa
kawaida ni ndefu kuliko hadithi fupi. Urefu wa riwaya maana yake ni
kwamba msuko wa simulizi umejengeka vizuri, kuna wahusika wengi,
unaenea muda mrefu, na mada zake ni nzito na pana kiasi.
Muhando
na Balisidya (1976) wanaeleza kuwa riwaya ni kazi ya kubuni kama
hadithi ambayo hutungwa na kuibua mambo mengi katika mazingira
wanayoishi watu.
Maana
ya Tamthiliya
Tamthiliya
ni utanzu ambao hutegemea mazungumzo na uigizaji ili kuwasilisha
ujumbe wake. Huu ni utanzu ambao huandikwa kwa mtindo wa mazungumzo
ya wahusika, (Wamitila, 2007).
Tamthiliya
ni mchezo wa kuigiza au utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani
katika matendo na mazungumzo
Muhtasari
wa Riwaya ya “Siku
Njema.”
Siku
njema ni
riwaya ya kitawasifu inazungumzia maisha ya Msifuni Kombo (Kongowe
Mswahili) iliyoandikwa na mwandishi Ken
Walibora
mnamo mwaka 1996. Riwaya hii imejikita katika kuzungumzia mambo
yanayoendelea katika jamii zetu za Kiswahili kama vile changamoto za
magonjwa, ndoa na familiya pamoja na malezi ya watoto. Mwandishi
kamtumia mhusika mkuu Msifuni Kombo maarufu kama Kongowea Msawahili
kuonesha namna alivyopitia changamoto mbalimbali zikiwemo kufiwa na
mama yake, kulelewa na mzazi mmoja (mama yake) baada ya mama kumkataa
baba yake Kongowea aliyejulikana kwa jina la Juma Mukosi. Kongowea
anapitia mateso mengi hata kutiliwa sumu kwenye chai na mkaza-mjomba
(Mwanasaumu) ili afe.
Wasifu
wa Prof. Ken Walibora
Ken
Walibora alizaliwa Magharibi mwa Kenya na alisoma elimu ya msingi
katika shule ya St. Joseph iliyoko wa mji wa Kitale. Alihitimu elimu
ya kidato cha nne katika shule ya upili ya Olkejuado, mjini Kajiado.
Na alihitimu mtihani wa kidato cha sita katika shule ya upili ya
Koelel, mjini Gilgil. Walibora baadae alisomea masuala ya Maendeleo
ya Jamii katika Taasisi ya Utawala, Kenya (KIA). Alihitimu shahada ya
kwanza katika fasihi na Kiswahili katika chuo kikuu cha Nairobi.
Prof. Walibora ni msomi mwenye PhD aliyoipatia nchini Kenya katika
Chuo kikuu cha Ohio State nchini Amerika. Riwaya yake ya kwanza
kuandika ni “Siku Njema” iliyochapishwa mwaka 1996 na amekwisha
andika zaidi ya vitabu arobaini baada ya riwaya hiyo.
Ufafanuzi
wa vipengele vya ulinganishaji katika riwaya ya “Siku njema”
Vipengele
tulivyochunguza ni plot (muundo), mandhari, wahusika na migogoro.
Vipengele hivyo vimefafanuliwa kwa kina kama ifuatavyo:
Ploti
(muundo); ni
namna matukio katika kazi ya fasihi yalivyopangwa na kuleta mtiririko
wa kazi husika ya fasihi (Senkoro, 2011). Katika riwaya ya “Siku
njema” iliyoandikwa na Ken
Walibora,
mwandishi amejenga visa na matukio katika mtiririko unaoeleweka kwa
urahisi kwa msomaji. Kwa hiyo ni dhahiri kusema kuwa mwandishi wa
riwaya hii ametumia muundo
wa msago (muundo
wa moja kwa moja) ambapo ameonesha mtiririko ufuatao:
Katika sura ya
kwanza; ameonesha historia na asili ya Zainabu Makame ambayo
imejengeka kupitia familiya ya Mzee Makame iliyoishi mjini Mwanza
kabla ya mzee Makame kufariki.
Sura
ya pili; Bibi yake Kongowea amerudi Tanga na Zainabu anajiunga na
kikundi cha Mbelewele
taarabu na kupata umaarufu kutokana na sauti yake nzuri katika
uimbaji.
Katika
sura hii pia kuzaliwa kwa Msifuni Kombo (Kongowea mswahili)
kunadhihirika. Pia katika sura hii inaonesha Zainabu Makame anaanza
kuugua.
Sura
ya tatu; mwandishi anaonesha Zainabu akiaga dunia baada ya kuugua
muda mrefu na kukosa tiba ya maradhi yaliyomsumbua. Lakini mama huyu
anafariki bila kumuonesha mwanae baba yake.
Sura ya nne na
kuendelea inadokeza changamoto alizopitia Kongowea hasa baada ya
kwenda kuishi kwa mkaza-mjomba wake (Mwanasaumu).
Katika
sura ya tano na kuendelea mwandishi ameonesha harakati za Kongowea
kumtafuta baba yake na hatimaye anafanikiwa kukutana naye kama
mwandishi anavyoonesha kuanzia mwishoni mwa sura ya kumi na tatu
mpaka kumi na nne.
Baada
ya Kongowea kukutana na baba yake aliyejulikana kwa jina la Juma
Mukosi, baba huyo anafariki kabla ya mwanaye kumtambua na kuacha
wosia unaomuongoza mwanae kutambua mali alizotakiwa kuzirithi kutoka
kwa baba yake. Baada ya kuupata wosia ule maisha ya Kongowea
yanabadilika baada ya mahangaiko ya muda mrefu tangu kuzaliwa kwake.
Mandhari;
huwa
ni mahali hususani jinsi panavyoonekana katika hali halisi ya maisha
(Williady, 2015). Mtunzi anaweza kutumia mandhari kuelezea mazingira
halisi ya kisa anachosimulia. Pia mtunzi huweza kusawili mazingira
mbalimbali akiyasawiri matukio tofautitofauti ikiwa ni mbinu mojawapo
ya kufikisha ujumbe wake kwa jamii husika. Hivyo mandhari humsaidia
msomaji kung’amua ujumbe akirejelea tukio husika.
Mwandishi Ken
Walibora
katika riwaya hii ameweza kujenga visa na matukio katika mazingira
halisi (mandhari
halisi). Mandhari aliyotumia imejumuisha maeneo ya nchi mbili za
Afrika ya Mashariki ambazo ni Tanzania akirejelea maeneno ya Mwanza-
huku ndipo alipozaliwa Zainabu Makame mnamo mwaka 1927 (uk.15),
Chongoleani- mkoani Tanga ambako walizaliwa babu na bibi zake Zainabu
(uk.2), Tabora-mahali pa makazi ya Enock Minja mpwa wa Mwanasaumu
(uk.23), Hospitalini (Holelaholela) ni pale alipopelekwa Bi. Rahma
kwa ajili ya matibabu (uk.28), Arusha ni sehemu Vumilia alikuwa
anasoma (uk. 45), Buguruni-Dar es Salaam-mahali alipokuwa anafanya
kazi mama yake Alicia (uk.109). Nchini Kenya mwandishi amerejelea
maeneo ya Mombasa- mahali alipokuwa anakaa Salimu ambaye ni mjomba
wake Kongowea (uk.18), pia ni sehemu ambapo Enock Minja alifikwa na
mauti baada ya kupata ajali ya gari, vilevile ndiko alikohamia baba
yake Kongowea katika ule mji wa Kitale (uk.33).
Wahusika;
ni
viumbe hai au viumbe visivyo hai ambavyo hubebeshwa majukumu na
msanii ili kuifikishia hadhira ujumbe uliokusudiwa na mwandishi
(Williady, 2015). Mwandishi Ken Walibora katika riwaya ya “Siku
Njema”
amadhihirisha wahusika ambao tunaweza kuwaweka katika makundi matatu
kutokana na hadhi ya uhusika wao, makundi hayo ni wahusika wakuu,
wahusika wasaidizi na wahusika wajenzi kama yalivyofafanuliwa hapa
chini:
- Mhusika mkuu; katika riwaya hii mhusika mkuu ni Msifuni Kombo maarufu kwa jina la Kongowea Mswahili kwani ndiye aliyebeba dhamira kuu ambayo ni familia na malezi akiwa kama mtoto aliyekosa malezi ya baba na kulelewa na mama, lakini mama yake naye anafariki na kulelew na mjomba. Pia mhusika huyu ndiye alidhihirisha mantiki ya tawasifu katika riwaya hii kwani mtiririko wake unadokeza historia yake toka kuzaliwa mpaka kufiwa na wazazi wote wawili.
- Wahusika wajenzi; hawa huwa ni wahusika wanaoibuliwa na mwandishi ili kujenga dhamira na baadae hutoweka. Katika riwaya hii wahusika wajenzi ni pamoja na Bi. Mack Donald ambaye ameibua dhamira ya upendo baada ya kumsaidia Kongowea katika mkahawa; Enock Minja ambaye ameibua dhamira ya dhuluma ya urithi na tamaa ya mali baada ya kukubali kujifanya mtoto wa Juma Mukosi ili akarithi mali na matokeo yake anafariki kwa ajali ya gari kabla hajafika kwa Juma Mukosi.
- Wahusika wasaidizi; hawa ni wahusika ambao humsaidia mhusika mkuu katika ujengaji wa dhamira. Kwa mfano Ken Walibora amemtumia Bi. Zainabu Makame kama mama yake Kongowea Mswahili ili kuibua dhamira ya malezi ya watoto; Kitwana ametumiwa kama mjomba wake Kongowea anayemchukua na kuishi naye baada ya kufiwa na mama yake. Alikuwa mshauri mkuu wa Kongowea; Vumilia pia ni mhusika aliyeshiriki kama msaidizi kwani alichorwa kama rafiki yake Kongowea na baadaye akaja kuwa mke wake. Huyu ndiye aliyemdokeza Kongowea kuwa kuna mpango wa kutiliwa sumu kwenye ili afe uliopangwa na mkaza-mjomba wake.
Mgogoro;
ni
hali ya kutoelewana baina ya pande mbili yaani mtu na mtu, mtu na
kundi, mtu mwenyewe na nafsi yake. Mgogoro ni mivutano na misuguano
mbalimbali katika kazi ya fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya
wahusika na familia zao, au matabaka yao. Pia migogoro inaweza
kugawanyika katika vipengele vikuu viwili ambavyo ni mgogoro wa
nafsia na mgogoro wa mtu na mtu au kundi kama ilivyodhihirishwa na
Ken Walibora katika riwaya ya “Siku Njema”.
- Mgogoro wa Nafsia; ni aina ya mgogoro unaotokea baina ya mtu na akili au nafsi yake mwenyewe pale anapojikuta katika wakati mgumu kutokana na jambo fulani na asijue nini cha kufanya.
Mgogoro
huu umedhihirika kwa Kongowea baada ya kifo cha mama yake akibaki
hajui ni namna gani atampata baba yake. Suluhisho la mgogoro huu pale
alipoambiwa na Bi. Rahma baba yake aliko;
pia mgogoro wa aina
hii unadhihirika kwa Juma Mukosi maarufu kwa jina la Kazikwisha baada
ya kukataliwa na Zainabu hali hii ilimpelekea kuacha kazi. Suluhisho
la mgogoro huu ni yeye kuamua kuishi maisha ya ukiwa mpaka siku yake
ya mwisho (uk.132)… Baada
ya zawadi kunikata maisha yalikosa maana na kazumu kuishi maisha ya
ukiwa mpaka siku yangu ya mauko. Nikaacha kazi na kughunia huku
makutano kwa ngozi baada ya kununua shamba hili…. Kuishi ukiwa
ndiko kumekuwa faraja yangu.
- Migogoro kati ya mtu na mtu; ni migogoro inayotokea baina ya mtu na mtu au mtu na kikundi au hata familia. Migogoro ya aina hii imejitokeza kati ya wahusika wafuatao;
Mwanasaumu
na Kongowea (uk.20-25)
Chanzo
cha mgogoro baina ya wahusika hawa ni kufaulu kwa Kongowea katika
mtihani wa darasa la saba huku watoto wa Mwanasaumu wakiwa hawajiwezi
kimasomo, hivyo hakupenda Kongowea afaulu hali iliyopeleka chuki
mpaka akamtilia sumu kwenye chai ili afe. Suluhisho la mgogoro huu
ilikuwa Kongowea kuondoka kwa Mkaza-mjomba na kwenda kumtafuta baba
yake Kenya.
Kongowea
na Selemani Mapunda (uk.21)
Chanzo
cha mgogoro huu ni baada ya Selemani Mapunda kubaini kuwa Kongowea
ndiye aliyepeleka taarifa polisi kuwa Selemani na wenzake
aliwashuhudia wakimpiga Hedimasta. Suluhisho la mgogoro huu ni
Selemani Mapunda na Bakari kuuawa (uk.131).
Alice
na mama yake (Bi. Mack Donald)
Chanzo
cha mgogogoro huu ni mama Alicia kumsaidia Kongowea Mswahili baada ya
kumkuta mgonjwa katika mkahawa ulioitwa Saidia
Khala,
Alice alikasirishwa na kitendo hicho cha mama yake. Alice anasema
“…mama
huyu mtu unampeleka wapi, akamuuliza bintiye. ‘Shut up’ alifoka
mama mtu”
(uk.107). Suluhisho la mgogoro huu ni pale tu Alicia anapokuja
kutambua kuwa Kongowea ni mahiri wa mashairi na kujikuta wanakuwa
marafiki.
Muhtasari
wa Tamthiliya ya “Natala”
Tamthilia ya
“Natala” ni tamthiliya iliyoandikwa na Profesa Kithaka Wa Mberia
mwaka 1997 ambayo imemulika baadhi ya masuala ya kijamii yanayoleta
mabishano makubwa. Baadhi ya masuala hayo ni pamoja na kuoza kwa
mfumo wa uadilifu na utamaduni unaozivuta jamii nyuma kama vile
kurithi wajane na ukatili kwa wanawake (udhalilishaji wa kijinsia)
ambao msanii kauchora kupitia mhudumu wa jengo la ufuo kumtaka Natala
kimapenzi kwa nguvu wakati amefuata mwili wa marehemu mumewe baada ya
kudhaniwa kuwa amefariki kwa ajali ya gari.
Wasifu
wa Prof. Kithaka Wa Mberia
Kithaka
Wa Mberia alizaliwa mwaka 1955 nchini Keya. Ni mshairi mbunifu wa
mashairi huru (mashairi ya kisasa). Amewahi kuchapisha vitabu vinne
vya ushairi ambavyo ni Mchezo wa Karata (1997), Bara Jingine (2001),
Redio na Mwezi (2005) na Msimu wa Tisa (2007). Maashairi yake
yamekuwa mashairi ya kwanza ya Kiswahili kuigizwa katika tamsha la
maonesho la kitaifa nchini Kenya mwaka 1988. Wa Mberia pia ni
mtaaluma na mwandishi wa tamthiliya. Ni prof. wa lugha katika chuo
kikuu cha Nairobi. Ameandika tamthiliya tatu ambapo mojawapo
imefanikiwa kurushwa katika runinga nchini Kenya.
Ufafanuzi
wa vipengele vya ulinganishaji katika tamthiliya ya “Natala”
Ploti
(muundo); kama
tulivyoona katika maelezo ya awali, ploti ni namna matukio katika
kazi ya fasihi yalivyopangwa na kuleta mtirirko wa kazi husika ya
fasihi. Ni jinsi mwandishi alivyoipanga kazi yake (Senkoro, 2011).
Mwandishi wa tamthiliya hii amejenga matukio yake katika mtiririko wa
matukio kufuatana (muundo wa moja kwa moja) kama inavyodhihirika
katika muhtasari ufuatao kuanzia onesho la kwanza hadi la mwisho (la
tano):
Onyesho
la Kwanza; linadokeza nyumbani kwa Natala akiendelea na shughuli
zake. Baadaye Tila anaingia kuomba chumvi, na baadaye kuzua tafrani
akidai chumvi aliyopewa ni kidogo.
Onyesho
la Pili; linadokeza Chifu akileta taarifa za kufariki kwa Tango
nyumbani kwa Natala. Vilevile mwandishi anaonesha Natala na Bala
wakiigiza mambo yale waliyokumbana nayo kule kwenye jengo la ufuo
baada ya kufuata mwili wa marehemu mochwari (jingo la ufuo).
Onyesho
la tatu; mwandishi anaonesha mazishi ya Tango na vikwazo
wanavyopambana navyo ndugu wa marehemukutoka kwa chifu ikiwa ni
pamoja na kuomba rushwa ili wapate kibari cha kukusanyika kwa ajili
ya maziko.
Onyesho
la nne; linamuonesha Mama Lime akiwa anamshawishi Natala akubali
kuolewa na Wakene lakini anakataa.
Onyesho
la Tano; linamshuhudia Wakene akiwa nyumbani kwa Natala akimwambia
juu ya suala la kumrithi akiwa kama mke wa marehemu kaka yake lakini
Natala anapokataa Wakane anaamua kuchukua cheti cha shamba kwa nguvu.
Natala anaamua kusimama kidete na kumzuia Wakene kitendo
kilichopelekea wazozane Natala na Wakene. Mwisho katika onesho hili
Tango aliyesadikika kuwa amefariki anarejea nyumbani na kukuta vurugu
sebuleni kwake Natala na Wakene wakiwa wameshikana kuashiria kuna
ugomvi. Wanapomuona wote wanaduwaa na kuishiwa nguvu, baadaye Natala
anaamini kuwa Tango hakufa na anamsimulia mumewe yote yaliyokuwa
yanamsibu pindi imesemekana amekufa na kuzikwa.
Mandhari;
katika tamthiliya hii mandhari halisi imechorwa kama ifuatavyo;
nyumbani-
mahali ambapo walikuwa wakiishi Natala, Tango Mwina na watoto wao
wawili ambao ni Bwanu na Alika; makaburini-
ni mahali ambapo maziko ya mtu aliyezaniwa kuwa Tango yalifanyika;
Gerezani-
ni mahali alipofungwa Tango baada kukamatwa na polisi kwa kosa la
uzururaji; mjini-hapa
ndipo Tango alipokamatwa pamoja na watu wengine wakiwa wamelewa;
mochwari (jengo la ufuo)-ndipo ilipokuwa imehifadhiwa maiti ya mtu
aliyesadikika kuwa ni Tango Mwina.
Wahusika;
mwandishi wa tamthiliya hii ameonesha wahusika ambao tumeweza
kuwatenga katika makundi makuu matatu kutokana na uhusika wao kama
inavyofafanuliwa hapa chini:
- Mhusika mkuu; katika tamthiliya hii Natala ndiye mhusika mkuu kwani ndiye aliyebeba dhamira kuu ya ukombozi wa mwanamke kiutamaduni. Pia inatokana na ujasiri wake wa kuweza kupiga dhuluma yake na kupigana na wanaume waliotaka kuudhalilisha utu wake.
- Wahusika wajenzi; hawa ni wahusika kama Kasisi-aliyeongoza mazishi kule makaburini; Chifu- huyu ni kiongozi anayependa rushwa hivyo anawakilisha viongozi wasiotenda haki kwa watu wao na hivyo anaibua dhamira kama rushwa na uongozi mbaya; mhudumu wa jengo la ufuo-amechorwa kama mtumishi asiyethamini utu wa mwanamke pale anapotaka kumbaka Natala.
- Wahusika wasaidizi; mwandishi Kachora wahusika wanaomsaidia Natala katika kutimiza dhamira yake kuu baadhi yao ni Wakene- ambaye ni shemeji yake anayetaka kumdhulumu mali Natala baada ya kukataa kurithiwa; Mama Lime-aliyekuwa akimshawishi Natala akubali kuolewa na Wakene; Tango- amechorwa kama mume wa Natala na inaposemekana kuwa amefariki Natala anapangiwa kurithiwa na Wakene; Bwanu na Alika- ni watoto wa Natala na Tango Mwina. Wamemsaidia Natala kujenga dhamira ya malezi ya wototo; wahusika wengine wasaidizi ni pamoja na Bala, Mzee Balu na Tila ambaye ndiye mke halali wa Wakene.
Migogoro;
Profesa
Kithaka
Wa Mberia
katika tamthiliya hii ya “Natala” pia ameonesha migogoro amabayo
tumeijadili katika makundi makuu mawili yani mgogoro wa nafsia na
migogoro ya mtu na mtu au kikundi:
- Mgogoro wa nafsi
Mgogoro huu
unamkumba Natala baada ya kupata taarifa kuwa mumewe Tango amefariki
na kuanza kuwaza/kufikiri jinsi atakavyoweza kuwalea watoto peke yake
akawa analalamika moyoni akisema;
“Dhiki gani
hii? Kwanini ninyang’anywe mume? Msiba juu ya msiba! Majonzi juu ya
majonzi…”
(uk.9). Suluhisho la mgogoro huu ni Tango kurejea nyumbani na wote
kujua Tango bado yu hai.
- Mgogoro wa mtu na mtu
Natala na Wakene
Mgogoro huu
ulitokana na Wakene kutaka kumrithi mke wa kaka yake ambaye ni Natala
ili achukue mali zote pamoja na shamba. Natala anapokataa ndipo
wanapoanza kunyang’nayana cheti cha shamba (uk.53-55) wanabishana
wakisema;
“Natala: kilete
cheti!
Wakene:
Nitakutwanga!
Natala: niguse
uone! Tia mkono motoni.
Mama Lime: Wakene
mtie adabu huyo mwanamke!”
suluhisho la
mgogoro huu ni Tango kurejea nyumbani.
Natala na mhudumu
wa jengo la ufuo (mochwari)
Mgogoro huu unatokea
pale mhudumu anapomtaka kimapenzi Natala ili aweze kumpa maiti ya
mume wake. Natala alipokataa akataka kumbaka na ndipo ugomvi
ulipoanza na wawili hao kusukumana hali iliyopelekea mhudumu
kuangushwa chini. Ukurasa wa (16-23) Natala akiigiza na Bala
wanasema;
Natala: Haja
yangu ni kuchukua maiti. Si kuona ofisi.
Bala: Kuona ofisi
ni kuchukua maiti.
Natala: Yaani iko
ofsini?”
Suluhisho la
mgogoro huu ni zamu ya mhudumu yule kuisha na kuingia mhudumu
mwingine aliyewapa maiti bila kuwadai chochote
Natala
na Chifu
Mgogoro unatokana na
kitendo cha Chifu kuzuia mazishi ya mwili wa mtu aliyesemekana kuwa
Tango Mwina mumewe Natala akidai hawana kibari cha kuzika la sivyo
watoe pesa (uk.30-35) chifu anasema;
“Chifu:
Mnafanya nini? Hamkumupata ujumbe wangu? Nilisema maiti isizikwe
mpaka nifike… Mbona mnaidharau serikali namna hii?...
Natala: Tuliupata
Chifu: …kisha
ikawaje?
Natala: Baada ya
kukungoja kwa kitambo kirefu tulionelea tuendelee na mazishi.”
Suluhisho la mgogoro huu lilipatikana baada ya mzee Palipali
kuzungumza na chifu na kuahidi watamuona wakimaliza maziko.
Kwa
ujumla Prof. Ken Walibora na Prof. Wa Mberia wameweza kuyatazama
mambo kiyakinifu ikiwa na maana kuwa wanayazungumzia matatizo ya
jamii za Afrika ya mashariki kama yalivyo bila kutumia mbinu ya
kuficha. Wote kwa ujumla wameweza kuibua na kero zinazozikumba
familia nyingi za kiafrika ikiwa ni sambamba na mila na tamaduni
kandamizi kwa mwanamke mfano urithi wa mjane na mali zake.
MAREJELEO
Muhando,
P na Balisidya, N. (1976). Fasihi na Sanaa za Maonesho. Dar es
Salaam: T.P.H
Senkoro,
F.E.M.K. (2011). Fasihi; Mfululizo wa lugha na Fasihi. Dar es Salaam:
KAUTTU
Wamitila,
K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi; Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus
publication limited.
Kitabu
cha NATALA na kitabu cha SIKU NJEMA